Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, zawadi nyingine tena nzuri kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona tena leo. Hakikisha unaitumia vizuri zawadi hii ya siku ya leo, sio ujanja ujanja uliotufikisha mahali hapa, ni kwa uwezo wake Mungu tu.
Wengi sana tumejipoteza na kujikuta ile bidii yetu tuliyoanza nayo mwanzo haipo tena, mwanzo wakati tunaanza kupoteza mwelekeo tuliona ni jambo la kawaida sana. Ukawaida huu umevuta wengi mpaka kufikia usugu na kutokuona tena ile hamu ya kiMungu ndani yao.
Maisha yetu yanaunganishwa na mambo mbalimbali ndipo yanakamilika kuitwa maisha ya wokovu, kuna muungano wa mambo mengi sana ambayo mengine upaswa kuwa nayo makini ili yasije kukurudisha nyuma.
Nakumbuka miaka ya nyuma kidogo, sikuenda kanisani karibia miezi nane hivi kutokana na mazingira niliyokuwepo. Mwanzo niliona kama napoteza jambo la muhimu sana, ila kadri siku zilivyozidi kwenda nilipoteza kabisa hata ile hamu ya kwenda kanisani. Hata kushtuka kuwa sikwenda kanisani wala sikuwa nashtuka kabisa, yaani ni kama usugu fulani uliniingia bila mimi mwenyewe kujielewa.
Wakati mwingine tena nikiwa mazingira ambayo hayanizuii kwenda kanisani, sikwenda kanisani jumapili moja hivi, ikatokea jumapili nyingine tena ya pili sikwenda mpaka ya tatu. Mwisho nikajiona hapa ninapoelekea ni kuacha kabisa, ilibidi nirudi haraka sana.
Nazungumza mambo ya miaka kadhaa iliyopita, kukuonyesha jinsi gani kuna mambo hayapaswi kuachwa wala kupuuzwa na kuona utafanya tu. Hili eneo wengi sana wamepotelea kwenye kushindwa kusoma Neno la Mungu, walianza vizuri sana ila walipojidanganya kwamba ngoja wapumzike kidogo. Hapo hapo ndipo walipopoteza kabisa ule mwelekeo wao wa kusoma Neno la Mungu.
Nakueleza kisa cha kweli ambacho nimeona watu wengi sana walioanza kusoma Neno la Mungu kwa kasi kubwa, ila baada ya muda fulani walipotezana kabisa. Kupotea huwa kunaanzia pale mtu anasema ngoja nipumzike kidogo mpaka nivuke changamoto hii, ngoja nipumzike kidogo mpaka uchovu wa safari uniishe, ngoja nipumzike kidogo mwezi ujao nitaanza tena.
Ahadi hizi zinatimizwa na wachache sana walio na msukumo mkubwa wa kufanya kile wamedhamiria, na ni wachache sana huwa wanakumbuka kurudi kufanya kile walikuwa wanafanya. Hasa hili la kusoma Neno la Mungu, kwa wengi wanarudi sana nyuma, kwa sababu ni jambo ambalo halijazoeleka kwa jamii ya waamini wengi.
Kuna vitu unapaswa kuelewa kabisa moyoni mwako kuwa hupaswi kupumzika, uwe umechoka sana unapaswa kujilazimisha kufanya hata sio kwa viwango vya juu sana, uwe unajisikia vibaya jitahidi kufanya hata hatua ambazo unaona sio ndefu sana. Usikubali kupumzika siku mbili mpaka inaenda ya tano wewe bado unapumzikaga tu.
Tabia hii ya kusoma Neno la Mungu umeianza ukubwani, nikiwa na maana umeanza kujifunza ukubwani. Utoto wako wote huenda hujawahi kukutana na himizo la kusoma Neno la Mungu mpaka unakuwa mtu mzima. Msisitizo mkubwa ulioupata ulikuwa wa kuamka asubuhi kwenda Sunday school, ndio maana leo tuna idadi kubwa za washirika wa siku za jumapili tu.
Tunaanza kutengenezwa tukiwa wadogo, usifikiri watu hawapendi kuja ibada zingine za katikati ya wiki, usifikiri watu wote huwa wanabanwa na shughuli mpaka kushindwa lisaa limoja la mafundisho ya Neno la Mungu katikati ya wiki. Ni picha ambayo imejengwa ukiwa bado mtoto mdogo, watoto wadogo huwa hawasisitizwi wahudhurie ibada zingine tofauti na jumapili au jumamosi tu.
Maana yake ukitaka kutengeneza kizazi cha wakristo wasio wa jumapili tu, anza sasa kwa watoto, hapa utazalisha washirika wapenda ibada zote. Usifikiri ndugu zetu waislamu huwa wanapenda sana kufunga biashara zao na kuwaacha wateja wao mpaka wakasali kwanza, ni mafundisho ya tangu utoto wao.
Sasa wewe umeanza kujifunza kusoma Neno la Mungu ukubwani, tena unaendea uzee na pengine umeshaufikia kabisa uzee. Alafu leo hii unaanza kusoma Neno la Mungu miezi miwili mitatu, unasema ngoja nipumzike kidogo nitaanza tena mwezi ujao. Nakwambia huo mwezi utafika na utajipa mwezi mwingine na mwingine mpaka utapoa na kuona sio lazima sana usome Neno la Mungu.
Waswahili walisema, mkunje samaki angali mbichi,ikiwa na maana usipofunzwa tabia njema ukiwa mtoto mdogo, itakuwa ngumu ukishakuwa mkubwa. Ndio maana ukionywa ukiwa mkubwa unamwona anayekuonya anakufuatilia maisha yako, wakati ana nia njema na wewe, ila kwa kuwa akili yako haijaona hayo marekebisho tangu utoto wako. Lazima mtu yeyote atakayejaribu kukuonya na kukurudisha kwenye mstari mzuri, utamwona ni adui yako.
Hakikisha hujipi mwanya wowote wa kutosoma Neno la Mungu, banana mpaka sehemu ambayo unaona ni ngumu kwako. Umekosa sana kusoma Neno la Mungu itokee dharura ya siku moja tu tena iwe siriaz haswa, kesho yake hakikisha huruhusu tena uzembe huo. Labda itokee umelazwa hospital hujitambui chochote, maana yake naaminisha maisha yako yatawaliwe na kusoma Neno la Mungu.
Kujivunia umeokoka miaka 5 au 10 au 20 iliyopita alafu bado una mambo ya kitoto kama aliyeokoka jana, huo ni msingi mbovu uliojiwekea. Husomi Neno la Mungu alafu unajivunia umeokoka siku nyingi, huwezi kumshuhudia mtu yeyote kuwa imeandikwa katika kitabu fulani hivi na vile.
Wakati mwingine unatolewa jasho na wapagani, yote hii ni kwa sababu huna neno, unaanguka dhambini kila siku huku unajivunia miaka ya kuwa kanisani, pombe kidogo, sigara kidogo, nyumba ndogo, kuonjaonja wadada kidogo, kuonjwaonjwa na wakaka kidogo. Alafu unasema mimi nimeokoka, huo ujinga ulioweka kichwani uondoe kwa kuweka maarifa ya Neno la Mungu moyoni mwako, uone kama utaona ni sahihi kufanya hayo, na uone kama utakuwa na ujasiri wa kufanya huo mchanganyo wako.
Jambo la kuanza kujifunza ukubwani lina changamoto zake, sasa usiruhusu uzembe wowote kukuondoa kwenye mpango wako wa kusoma Neno la Mungu. Ukianza anza kweli, jifunge mkanda kisawasawa kiuononi, kaza kamba za viatu vyako. Zamani niliwaona wamama wakiwa siriazi kwenye jambo utawoona wakifunga kanga/kitenge viunoni mwao, na wewe dada/mama wa leo unaweza kuchukulia huo mfano ukauweka moyoni mwako.
Bila shaka umepata kitu cha kukusaidia katika usomaji wako wa Neno la Mungu, lengo ni wewe uwe imara katika usomaji wako wa Neno la Mungu. Haijalishi umeokoka leo, haijalishi umeokoka siku nyingi, kama husomi Neno la Mungu hilo ni tatizo unapaswa kulikataa haraka sana.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu. Kwa masomo mengine mazuri zaidi ya kukusaidia kukua katika usomaji wako wa Neno la Mungu.
Imeandaliwa na Samson Ernest.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.