Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, ashukuriwe Mungu mwenza wa yote kutupa kibali kingine cha kuiona tena leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana atupaye kushinda kila iitwapo leo.

Chapeo Ya Wokovu ni mtandao unaofanya kazi kuisambaza injili ya Kristo hasahasa kuhusu watu kuamka kusoma Neno la Mungu. Wengi sana wamebarikiwa na utaratibu huu na wengi maisha yao ya kiroho yamesogea hatua ambayo hawakuwa nayo hapo awali.

Tupo facebook, instagram na whatsApp, whatsApp ndio tumeweka nguvu kubwa kwa kusimamiana kila mmoja kuhakikisha anasoma Neno la Mungu kwa ule muda tuliokubaliana kila mmoja asome. Chapeo Ya Wokovu whatsApp group limekuwa baraka kwa wengi sana sana, hili group lipo na watu wenye rika tofauti tofauti nikiwa na maana wapo mama zetu, baba zetu na vijana pia.

Tunajua wote suala la kusoma Neno la Mungu ni jambo ambalo limekuwa ni changamoto kubwa kwa wakristo wengi, hii imetokana na kutowekewa misingi imara kuhusu hili jambo la usomaji wa maandiko Matakatifu. Tumekua katika hali ambazo hatukuweza kumwona mzazi akiwa anasoma Neno la Mungu, na hata kufundishwa na wazazi umhimu wa kusoma Neno la Mungu hatukuambiwa kabisa.

Hatuwezi kuwalaumu kwa hilo maana hata wao hawakuwahi kuambiwa umhimu wa kusoma Neno la Mungu, wala hakuwahi kujua sana kutokusoma Neno la Mungu ni hatari kubwa sana kwao. Tukianza kulaumu sana tutapata nafasi ya kuendelea kuwa wazembe na Kujitengenezea sababu nyingine ya kuja kulaumiwa na watoto/wajukuu zetu.

Kama unasoma ujumbe huu maana yake huna kisingizio cha kuja kusema sikujua umhimu wa kusoma Neno la Mungu. Umedumaa kiroho na huoni Mungu akitenda katika maisha yako kwa viwango vizuri kutokana na picha uliyonayo kuhusu Mungu. Umebeba mapokeo ya dini/dhehebu lako yameshindwa kukusaidia kuacha dhambi, ila ungebeba Neno la Mungu moyoni mwako lingekusaidia kutomtenda Mungu dhambi.

Sasa Chapeo Ya Wokovu amekuwa mwalimu mzuri wa kukusimamia na kukufuatilia hatua kwa hatua, kuhakikisha unasoma Neno la Mungu bila kuruka hata sura moja ya kitabu. Labda uamue mwenyewe kutokubali kuendana na wenzako, lakini wote waliosikiliza na kufuata maelekezo waliyopewa na wanayoendelea kupewa kuhusu kuimarisha usomaji wao wa biblia. Leo hii wamepanda viwango ambavyo hawakuwa navyo kabisa hapo mwanzo, na wengine wameanza kukolea kwenye Neno la Mungu. Kiasi kwamba siku kupita bila kusoma Neno la Mungu ni sawa na kujishindisha njaa siku nzima bila ya kula wakati alikuwa hajafunga.

Tabia yeyote unayoiona mtu anayo imejengwa, iwe nzuri au mbaya, fahamu kwamba hiyo tabia imeanza kwa msingi ambao muda mwingine ukisema uitoe. Utahitaji neema ya Mungu kukusaidia kuiondoa tabia mbaya iliyopandwa ndani ya mtu, na wakati mwingine hupendi kuwa hivyo ulivyo leo ila upo hivyo pamoja na hupendi. Unahitaji kusimama kweli ili kujenga tabia njema ambayo kila atakayekutazama atatamani kujifunza kitu kupitia wewe.

Kwanini nakuandikia haya yote? Na kukuchosha kwa maandiko mengi? Ninachotaka kwako ni upate kuelewa hichi ninachotaka kukueleza hapa.

Siku za mwanzo kabisa mitandao ya kijamii ilionekana kama ni uhuni ambao hasa vijana tulionekana ni wahuni tu pale utakapoonekana unatumia facebook, instagram, whatsApp...na mitandao mingine mingi ambayo sikutaja. Tena watumishi walisimama kukemea hili mara nyingi, bila kufahamu kwenye mitandao kuna mambo mazuri na humohumo kuna mambo mabaya. Kama ilivyo mitaani tunapotembea, tunakutana na vishawishi vya kumtenda Mungu dhambi, na mitaa hiyohiyo kuna mazuri ya kutushawishi kumrudia na kumpenda Mungu.

Watumishi wachache walielewa hili na walitumia mabadiliko ya teknolojia kuhubiri injili kwa mamilioni ya watu kwa muda mfupi. Na vijana wengi na watu wazima wameokoka kupitia mitandao hii hii ya kijamii iliyoonekana ni uhuni.

Lakini leo hii ninapokuandikia ujumbe huu, karibia makanisa yote ya mjini na watumishi wengi wana akaunti facebook, YouTube, instagram na whatsApp. Leo ukiwauliza vipi mbona haya ni mambo ya vijana wasiomjua Kristo vizuri, sijui watakujibu nini. Ila nakumbuka kuna siku nilikuwa naongea na baba yangu mmoja, yeye ni mtu wa Mungu na ni wale wazee wa zamani wa dini. Nilishangaa mtazamo alionao leo kuhusu mitandao, alichoniambia mwanangu kwenye mitandao ni wewe unachagua unataka nini yale usiyotaka unaachana nayo. Akaenda mbali kidogo na kuniambia hata mtaani kuna vitu vya kutazama na vingine visivyofaa unaachana navyo.

Nakushauri ujiunge na group hili la Chapeo Ya Wokovu whatsApp, ili likutengenezee utaratibu huu mzuri wa kusoma Neno la Mungu kila siku. Unachotakiwa kuwa nacho ni smartphone/tablet yako, hii nafikiri utakuwa nayo ndio maana umeweza kusoma hapa. Kama huna tafuta pesa ununue kwa matumizi ya kupata maarifa mbalimbali.

Chapeo Ya Wokovu whatsApp group ni kama familia, ukikubaliana kwenda na wenzako na ukafuata kanuni ambazo utazipewa kabla ya kuingia. Utafurahi kuwepo katika familia hii, yapo mengi tunasaidiana ya kiroho na kimwili. Pia utasimamiwa kuhakikisha unasoma Neno la Mungu, usiposoma muda uliopewa, utaondolewa ndani ya kundi.

Kwa hiyo ukijiunga Chapeo Ya Wokovu wasap group, utakuwa na ndugu mnaosoma Neno la Mungu, na kushirikishana tafakari mbalimbali kuhusu kile Roho Mtakatifu amekufundisha zaidi kwenye mistari uliyokuwa unasoma.

Labda unajiuliza utawajuaje wale wasiosoma na wanaosoma Neno la Mungu? Hilo ondoa shaka, kwa ambao tayari wapo Chapeo Ya Wokovu watakuwa shahidi kwa hili. Ila wewe ambaye haupo ukiingia utajionea mwenyewe jinsi tunavyoendesha darasa hili.

Kitu kingine labda unajiuliza utachajiwa gharama yeyote? Hapana gharama yako ni kuwa na smartphone/tablet yenye uwezo wa kuwa na Application ya whatsApp. Na kuweka bidii yako ya kusoma Neno la Mungu, na kama umezoea kuwa mtu wa sababu kukwepa kufanya wajibu wako, Chapeo Ya Wokovu utakwama.

Unachokitakiwa kufanya ni kutuma ujumbe wako mfupi wenye jina lako kamili kwa njia ya whatsApp kwenda +255759808081, hakikisha umeamua kweli na tumia whatsApp tu kuwasiliana nasi.

Hili zoezi la kujiunga whatsApp group tulilifunga karibia mwezi mzima, ila leo tunapoanza 01 July 2017 tumeona vyema wewe mwenye kiu ya kuungana na wakristo wenzako wenye nia moja, usiikose nafasi hii muhimu kwako. Mlango upo wazi na nafasi ni chache, hatutakuwa na makundi mawili ya whatsApp, likishajaa hili basi.

Usiogope na wala usiwe na hofu kuhusu utulivu wa group hili, wapo wazee wenye umri mkubwa ambao tupo nao tangu 2014. Ni group ambalo linamaanisha na halina mambo ya siasa na wala halina muda wa kujadili dhehebu/dini yako, unachokiwa wewe ni uwe tu unamwamini Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako.

Labda unajiuliza utawezaje kusoma Neno la Mungu na ukaelewa kile umejifunza, Usiogope kama umeweza kusoma hapa na umefikia hatua hii. Ambapo umesoma maneno yasiyopungua 900 na bado unaendelea kusoma, hutoshindwa kusoma Neno la Mungu kwa sura chache utakazopangiwa.

Kama tayari upo Chapeo Ya Wokovu, nikupe hongera na endelea kuweka bidii yako ya kusoma Neno la Mungu. Uwe balozi mwaminifu kuwavuta na wengine ili waweze kujua kusoma Neno la Mungu ni muhimu kwao.

Hongera kwa kuwa mvumilivu kusoma ujumbe huu, naamini kuna kitu umejifunza kupitia ujumbe huu, nakukumbusha tena kama hujajiunga Chapeo Ya Wokovu whatsApp group jiunge sasa kupitia namba hizi +255759808081.Sio lazima, ni hiari ya moyo wako, ila ni muhimu kwako kama mkristo kusoma Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma makala hii, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.