Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, Mungu wetu ni mwema sana kwetu ametupa kibali kingine cha kuiona siku leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.
Tumekosa uhuru wa fikira zetu na kujikuta tupo njia panda kwa mambo mengi sana yanayohusu ukristo wetu, badala ya kuendelea kufurahia wokovu wetu. Tumekuwa na mashaka na wokovu wetu na kujikuta tupo njia panda, kushindwa kuelewa tunachokifuata na kukifanya ni sahihi au sio sahihi.
Wengi tumebaki tunaenda tu kama mtu asiye na dira ya anapoelekea, yaani kama vile tunasema popote tutakapofikishwa ni hapohapo. Ila ndani yetu tunakuwa hatuna tumaini lolote la kuweza kusimama kusema kwa ujasiri tulipo na tunapoelekea ni sahihi.
Fikira zako zinaweza kufungwa kwenye jambo fulani likawa kitanzi kwanzo na vile vile fikira zako zinaweza kuwekwa huru kwako. Kuna wakati unaweza kuwa huru kifikira lakini wenzako wanaweza kuwa wamefungwa fikira zao kutokana na mapokeo mabaya waliyonayo.
Hebu tuangalie NENO LA MUNGU linasemaje kuhusu fikira za mtu;
1. Kukosa tumaini la kusonga mbele.
Kuna kukosa tumaini kwa kufedheheshwa ndani ya fikra zako, unapofedheshwa ndani ya fikira zako hata ile hamu/kiu ya kuendelea mbele kwa kile ulichokuwa unakifanya, au unakikusudia au unakitarajia kunakosekana tumaini.
Rejea; Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha; viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana. Danieli 5:6 SUV.
Unaweza kufedheheshwa fikira zako, kwa ndoto ambayo utashindwa kupata maana yake, unaweza kufedheheshwa fikira zako kwa kushindwa kung’amua jambo fulani linalohusu imani yako kwa kukosa Neno la Mungu. Unaweza kufedheheshwa fikira zako kwa jambo linalohusu ndoa yako kwa kukosa maarifa sahihi ya namna ya kuishi na mume/mke wako.
2. Kumkosea Mungu Pasipo Kujua.
Unaweza kujiona upo sahihi kutokana na fikira zako zinavyokutuma, na unaweza kuishi maisha ya kumtenda Mungu dhambi kutokana na fikira zako zinavyokutuma kufanya hilo jambo ni sahihi kwako.
Mfano; Vijana wengi wanasema kujichua sehemu za siri haina shida wala sio dhambi, hii ni kutokana na mafundisho potovu waliyopata. Wengi wamepata elimu hii kwa kusoma vitabu visivyofaa na wengine wamepata maarifa hata kwa wakristo wenzao wasio na Neno la Mungu mioyoni mwao.
Fikira zako zinaweza kukutuma unavyoenenda ni sahihi, na akija mtu mwingine kukuambia sio sahihi unavyofanya au unavyofikiri. Unaona haelewi kitu, hata kama akikupa andiko ndani ya biblia, bado utaona amekosea.
Rejea; Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wako. Matendo 8:22 SUV.
Umeona hapo, inasema tubia uovu wako ili usamehewe fikira mbovu uliyokuwa nayo moyoni mwako. Kumbe fikira zetu zinaweza kuponywa kwa kukubali kutubia ule uovu tuliokuwa tunaufanya, huku fikira zetu zikitutuma ni sahihi kufanya jambo hilo.
3. Utazitambua Fikira Za Kumtenda Mungu Dhambi.
Kabla hujajua Neno la Mungu huwezi kujua kila wazo linalokujia kwenye akili zako linaweza kukupelekea kumtenda Mungu dhambi. Ni rahisi kumsikiliza Roho Mtakatifu anapokuonya na kukupa tahadhari ya jambo fulani la hatari linalokuja mbele yako kama utaendelea na kile unafanya.
Lakini ukiwa huna Neno la Mungu la kutosha, unaweza kukaidi hilo onyo na ukaendelea na hicho unafanya. Ila mtu aliye na Neno la Mungu, ni rahisi kwake kuzitambua fikira za shetani ndani yake.
Rejea; Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake. 2 Wakorintho 2:11 SUV.
Kumbe shetani anaweza kutushinda kama hatutajua fikira zake, ila tukishazijua ni rahisi kujiondoa haraka kwake, kwa lile jambo tulilokuwa tunafanya au tulilokuwa tunaelekea kulifanya.
4. Kuwekwa Uzito Kwenye Fikira zako usiweze kuelewa.
Unaweza kusoma sana Neno la Mungu usilielewe vile ipasavyo kulielewa, kutokana na fikira zako kutiwa uzito ndani yake. Hili ni jambo la msingi sana kulijua na kuomba Mungu hata kwa watoto wako unapogundua hawaelewi masomo darasani.
Kufungwa kwa fikira ipo kabisa na unaweza usijue sana ila kama utakuwa msomaji wa Neno la Mungu utalijua hili. Maarifa yote yanayohusu ukristo wetu, tunayapata ndani ya biblia, usifikiri biblia ni maalum tu kwa siku za jumapili.
Rejea; Ila fikira zao zilitiwa uzito. Kwa maana hata leo hivi, wakati lisomwapo Agano la Kale, utaji uo huo wakaa; yaani, haikufunuliwa kwamba huondolewa katika Kristo; 2 Wakorintho 3:14 SUV.
Nafikiri umeanza kunielewa sasa kwa hichi ninachokueleza, nakupitisha kwenye mistari mingi ili uweze kuelewa zaidi hili ninalokueleza hapa.
5. Upofu wa fikira kwa wasiomjua Kristo.
Usije ukapata shida sana kujiuliza kwanini watu wanamkataa Yesu Kristo, unaweza kuwapa maandiko na maandiko ya biblia. Na wasiweze kukuelewa kabisa, unaweza kufikiri wanafanya makusudi kutokuelewa kile unawaeleza. Nakwambia hawafanyi makusudi, mungu wao amefunga fikira zao wasiweze kuelewa kabisa Neno la Mungu, wala ile injili ya kweli inayohubiriwa.
Rejea; Ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu. 2 Wakorintho 4:4 SUV.
Haleluya, kumbe upofu sio tu wa macho ya nyama. Hata upofu wa fikira zetu unaweza kuwepo ndani yetu, ni nani ataweza kutusaidia kutuondoa upofu huu kama sio kumruhusu Yesu Kristo ndani yetu afanye uchunguzi wa kina.
6. Fikira mbaya zinaweza kuondoshwa na zikamtii Kristo.
Kama tulivyoona huko juu fikira zetu zinavyoweza kuvaliwa na shetani, tunaweza kuziangusha zote. Chochote kilichoinuka ndani ya fikira zetu kinaangushwa, na tukawa na utii wa Mungu ndani yetu.
Rejea; Tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo; 2 Wakorintho 10:5 SUV.
Usipate hofu labda unajiuliza nitawezaje kuziondoa fikira mbaya na ukabaki na fikira safi, Neno la Mungu limesema zinaweza kuondolewa na ukawa unamtii Kristo katika roho na kweli.
7. Jihadhari na mafundisho ya upotoshaji.
Ili kuepuka kuharibiwa fikira zako, ni vizuri kujidhari sana na mahali pa kukusanyika pamoja na wenzako mkifanya ibada pamoja, ni vizuri kujihadhari mafundisho mbalimbali ili usije ukaharibika fikira zako.
Rejea; Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo. 2 Wakorintho 11:3 SUV.
Yapo mafundisho mengi sana yanapotosha kweli ya Mungu, na ili ulitambue hili unapaswa kujifunza Neno la Mungu kila siku. Wengi wameingia kwenye majuto ya maisha yao kwa sababu walipata mafundisho potofu.
Tafuta uhuru wako kwa kusoma Neno la Mungu, nimekuonyesha mistari mbalimbali kuhusu fikira, fikira zako zikiharibiwa ujue utamkosea tu Mungu. Unapaswa kulijaza Neno la Mungu kwa wingi moyoni mwako.
Nikuachie hayo ili uendelee kutafakari zaidi, muhimu sana kujiuliza kama fikira zako zipo salama, huenda unaenda kama mtu anayejua anapoenda kumbe hajui. Kuna kukosea njia, sasa kabla hujaenda sana mbali vizuri ukachunguza hali yako ya kiroho ipo ipi.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu. Kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.