Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona. Fursa kwetu kwenda kufanya yale yanayoweka alama njema duniani na mbinguni, alama hiyo ni kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.

Kuna vitu vingi huwa tunavitazama kwa nje vikatuvunja moyo wa kushindwa kuvifanya, lakini ukiamua kuchukua hatua ya kuanza kukifanya kile ulichoona kina ugumu. Utaona kadri unavyozidi kufanya, ndivyo ule ukubwa unavyozidi kupungua kabisa.

Wengi sana tumeitazama biblia kwa nje ikatuvunja moyo jinsi ilivyo, tofauti na vitabu vingine vya hadithi/riwaya. Huwa tunaviona havina shida, tunavisoma kuanzia sura ya kwanza mpaka nukta ya mwisho, tena inafika wakati tunasitisha na zoezi la kula kwa muda fulani ili tuweze kukimalizaharaka.

Biblia inashindikana kuisoma kwa sababu tunakuwa na mtazamo tofauti, tunataka iwe kama vitabu vya hadithi. Tumeshindwa kuelewa biblia ni zaidi ya vitabu vyote unavyovijua wewe duniani, tena ukiwa na muda wa kuisoma kila siku. Hata yule aliyekuwa anasoma vitabu vyake vya hadithi hatakufikia kiwango chako cha farijiko unalolipata ndani ya biblia.

Sikuambii uache kujifunza vitabu vingine vinavyokufundisha mambo mazuri, najaribu kukupa hali halisi jinsi ilivyo kwa wengi wetu kuhusu biblia. Maana tukijua thamani inayopatikana ndani ya maandiko matakatifu, hatutaona mzingo wa kusoma Neno la Mungu.

Unachotakiwa kujua ni kuacha kufikiria ukubwa wa biblia, ni kuacha kufikiria ukianza Mathayo utafika lini Ufunuo na ukianza Mwanzo utafika lini Malaki. Badala yake tengeneza picha kubwa ya kile unachoenda kukifanya, na kisha anza kukifanya kwa hatua ndogo ndogo bila kufikiri utamaliza lini.

Usikimbilie umalize kitabu chote, ondoa kabisa hiyo picha kichwani mwako. Unachopaswa kukimbilia na kuwa na kiu nacho ni kupata kitu cha kukusaidia katika maisha yako ya kiroho na kimwili. Na usitazame ukianza kusoma Mathayo utaimaliza lini, hiyo ondoa kabisa na weka mpango wa kusoma Neno la Mungu kila siku. Yaani uwe unajisikia vizuri au uwe unajisikia vibaya au uwe umechoka sana, hakikisha siku haipiti bila kusoma Neno la Mungu.

Utakapojiwekea utaratibu huu wa kusoma Neno la Mungu kila siku bila kuangalia utamaliza lini, utajikuta biblia ndio kinakuwa kitabu chako cha pekee sana. Utaona matokeo makubwa sana ambayo hapo awali hukuyaona, utaona biblia ni nzuri sana na muhimu kwako.

Mizigo mingi huwa tunaamua kujibebesha wenyewe kwa kutengeneza mtazamo hasi juu ya hilo jambo. Lakini wewe umebahatika kupata maarifa haya ya kuweza kukufanya ukafikia lengo lako la kuisoma biblia yako bila shida yeyote.

Binafsi nimeachaga kuangalia wingi wa mistari ya biblia, ukiachana na changamoto ya kuangalia ukubwa/ujazo/unene wa biblia, namshukuru Mungu nilivuka hilo. Ilikuja changamoto ya kutazama kitabu fulani kina sura nyingi sana, nilvyoona hilo linataka kuniondoa kwenye mpango wangu wa kusoma Neno la Mungu. Nilichoamua na kukubaliana nacho, nitaacha kufikiri idadi ya siku nitakazosoma hizo sura, si unajua ilivyo kazi kusoma sura moja au mbili ya kitabu mpaka ukimalize chote inahitaji nidhamu ya hali ya juu sana!

Lakini ukiamua kutoka ndani ya moyo wako, hakuna kinachoweza kushindikana, na uzuri wa kufanya jambo ni kwamba utakapokutana na changamoto ni rahisi kuifanya darasa la kuvuka hatua nyingine bora zaidi. Itakuwia vigumu pale utapokuwa unakiwaza kitu bila kukianza, nakwambia utajikatia tamaa humo humo kwenye mawazo pasipo hata kuanza kukifanya.

Angalia lengo lako ni nini, bila shaka ni kusoma Neno la Mungu, ukishajua hilo jiulize unataka kusoma mpaka lini. Mfano mimi nimejiwekea kusoma Neno la Mungu itakuwa ni utaratibu wangu wa maisha yangu yote nikiwa hapa duniani. Kujua kuwa ni mpango wangu wa maisha yangu yote, inanipa nguvu na nidhamu ya kutofikiri jinsi biblia ilivyo kubwa.

Unaweza kuchukua mfano wangu halisi niliokupa, ambao umenifanya nione suala la kusoma Neno la Mungu ni maisha yangu. Tangu nianze mpango huu mwaka 2015 wa kusoma Neno la Mungu kwa sura moja kila siku isipokuwa siku ya jumapili. Sikuwahi kuacha mpaka leo 2017, lakini huko nyuma kabla ya kuanza hili zoezi nilikuwa naona kitu kigumu sana kwangu.

Badili kufikiri kwako juu ya Neno la Mungu, utaona wepesi mkubwa sana katika usomaji wako wa Neno la Mungu. Hutojisikia umebeba mzigo mbaya, bali utaona ni wajibu wako kufanya hivyo, na utakuwa unajisikia hamasa kila ukiona wenzako wanasoma Neno la Mungu.

Nakukusisitiza tena na tena, achana na tabia ya kutazama ukubwa wa biblia kwa nje, anza kidogo kidogo kwa hatua. Utaona unafungua kitabu kimoja unakimaliza na kuhamia kingine, utaendelea hivyo mpaka utajikuta umemaliza biblia nzima ukiwa huwezi kusukumwa tena kuhusu usomaji wa Neno la Mungu.

Nisikupeleke mbele zaidi, nikuachia hapa ili upate muda wa kutafakari haya. Ili uweze kuchukua hatua za kuanza kusoma Neno la Mungu kwa mtazamo chanya, na kwa kuboresha yale maeneo uliyoona upo dhaifu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako, nikutakie siku njema utakayoimaliza kwa kutoa muda wako kusoma Neno la Mungu.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.