Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, tumepata kibali kingine cha kuiona siku ya leo, tunapaswa kumshukuru Mungu kwa zawadi hii njema.

Tunaweza kutembea na picha fulani ndani ya fahamu zetu kwa kufikiri tunavyoweza kufikiri, ila picha hiyo inaweza kutumika kama kitanzi kwetu kwa kufikiri ndio maisha yetu tunayopaswa kuishi nayo.

Yapo mambo tumeshindwa kufanikiwa kutokana na dhana/picha fulani tuliyonayo kuhusu hilo jambo, yaani unamezeshwa/unalishwa hofu na wewe unaishikilia kama vile ndio sehemu yako ya maisha.

Wakati huo yule anayekuambia jambo fulani ni gumu na haliwezekani, yeye analifanya au kama sio yeye wapo watu wanalifanya na wanafanikiwa/wamefanikiwa. Bila shaka tunajua hakuna jambo zuri linalotokea pasipo kutoa gharama, kwa hiyo kila jambo zuri unapaswa kulitolea jasho ndipo uweze kulipata.

Ikiwa suala ni kujenga nidhamu, kuweka bidii, na kuweka ufanisi kwa unachofanya, kwanini tusiwe na hiyo dhana/picha. Ila tunakuwa na picha jambo fulani gumu na haliwezekani kirahisi, hilo la haliwezekani kirahisi linajulikana tena maandiko matakatifu yakazungumza mwanaume atakula kwa jasho lake na mwanamke atazaa kwa uchungu.

Mfano anakujia mtu anaweka dhana/picha mbaya kwako, kuwa huwezi kuishi maisha yako ya ujana bila kufanya uasherati. Kwa kuwa hatuna Neno la Mungu na hatujakomaa kiroho, tunaondoka na hiyo picha tukiwa watoto mpaka kufikia umri wa ujana. Tunakuwa tunaona hatuwezi kuvuka ujana bila kuwa na mtu wa kufanya naye ngono, moja kwa moja kijana analazimika kuingia kwenye uasherati kwa dhana/picha aliyojegewa.

Dhana/picha nyingine iliyojengwa kwa watu na ndio inaharibu ndoa nyingi, ni kuwa na dhana kwamba mwanamke unapaswa kuwa na mafiga matatu yaani hupaswi kuwa na mwanaume mmoja unayemtegemea. Na mwanaume unaambiwa hupaswi kuwa na mke mmoja, lazima uwe na wengine wa nje, tena wanaenda mbali zaidi wanasema kizuri kula na wenzio.

Dhana nyingine tunayotengenezewa ni hii, haiwezekani kufanikiwa kifedha. Yaani haiwezekani kuwa na mali nyingi pasipo kuwa na roho mbaya, pasipo kuimbia wengine, pasipo kwenda kwa waganga wa kienyeji, pasipo kudhulumu wengine. Hebu fikiri hii dhana/picha aliyonayo kijana wa kikristo, unafikiri ukimwambia fanya kazi kwa bidii utafanikiwa ataweza kukuelewa? Bila shaka utagonga mwamba kama hujajipanga.

Zipo dhana nyingi sana kwenye maisha yetu ya kila siku ambazo zilianza kama utani, ila wengi wamezifanya kama ni kanuni zao za maisha. Si unaelewa uongo ukizungumzwa/ukitajwa sana unakuwa kama ukweli, fikiri mtoto anakuta baba yake au mtu yeyote anayemwamini anamwambia jambo hili ni sahihi wakati ni la uongo. Uwe na uhakika mtoto huyu asipopata fundisho zuri la kumwondoa hapo mpaka anakuwa mtu mzima, ataamini hilo ndilo sahihi na kumwondoa inahitaji neema ya Mungu iingilie kati.

Wengine tumetengenezewa dhana ya lugha ya kiingereza ni ngumu sana na wanaoijua wana akili sana, wengine tumetengenezewa dhana ya kwamba somo la hesabu ni gumu sana na wanaoliweza wana akili sana. Lakini wakati mtu amejitengenezea lugha ya kiingereza wanaijua watu fulani wenye upeo mkubwa wa akili, huyohuyo mtu anafahamu lugha za makabila karibia mawili mpaka matatu. Ambapo hizo lugha hawezi kuzungumza na kuzielewa mzungu wala huyo anayesemekana ana akili sana, shida ni nini, ni ile dhana iliyojengwa tangu zamani zile.

Nisikupeleke mbali zaidi huenda nikaendelea kukuvuruga, nirudi kwenye dhana mbaya kuhusu biblia ambayo ni Neno la Mungu. Wengi tumejenga dhana potofu inayoendelea kututavuna taratibu na kutufanya tusiwe na uzito wa kusoma Neno la Mungu. Wakati mwingine tunaanza vizuri kuweka bidii ya kusoma Neno la Mungu lakini tunapokumbuka kuhusu dhana iliyopo ndani mwetu, tunaacha Kusoma Biblia.

Dhana yenyewe ni hii, biblia ni kichaka/msitu mnene; naomba utulie na uvute picha hili NENO biblia ni kichaka/msitu mnene,wewe kama wewe umelitamka mara ngapi? Kama hukulitamka wewe utakuwa umelisikia mara ngapi?

Bila shaka utakuwa umelitamka mara nyingi na bila shaka utakuwa umelisikia mara nyingi, nami sikatai kuwa biblia sio kama gazeti linaloweza kusomwa na mtu yeyote. Hilo linaeleweka na maandiko matakatifu yapo wazi kuwa kuna watu wanasoma lakini hawaelewi wanachosoma. Hasa kundi hilo lisiloelewa wanachokisoma ni lile ambalo halijaamua kuokoka.

Rejea:Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao; ambao; akili zao zimetiwa giza, nao wamefarikishwa na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao; ambao wakiisha kufa ganzi wanajitia katika mambo ya ufisadi wapate kufanyiza kila namna ya uchafu kwa kutamani. WAEFESO 4:17‭-‬19 SUV.

Umeona hayo maandiko matakatifu, kumbe wasioweza kuelewa maandiko matakatifu ni wale ambao akili zao zimetiwa giza na wamefakarakanishwa na Mungu. Ili wasiweze kuipata ile nuru ya kweli, hawa ndio wale wakisoma maandiko matakatifu hawawezi kuelewa kitu. Mpaka pale neema ya Mungu iweze kuingilia kati, tena Neno la Mungu likaongezea zaidi haya;

Rejea:Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia. MATHAYO 13:14‭-‬16 SUV.

Itashangaza unaposema biblia ni kichaka kwa wewe uliyeokoka, tena ukisoma mstari wa mwisho kabisa unasema hivi;Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia. MATHAYO 13:‬16 SUV.Neno la Mungu linasema heri wewe uliyeokoka macho yako ya ndani yanaona, heri wewe uliyeokoka na kumwamini Yesu Kristo masikio yako ya ndani yanasikia.

Hebu nikuombe kuanzia leo ondoa dhana mbovu kuhusu Neno la Mungu, ruhusu Roho Mtakatifu afanye kazi ndani yako. Acha kufikiri kama mtu asiyeokoka, wengine tumepata fursa ya kuokoka ila akili zetu ni kama watu wasiokoka kabisa. Umesoma maandiko Matakatifu mwenyewe, tena nimekupa na vifungu uweze kuona Mungu alivyokupa nafasi kwake.

Acha kuishi na dhana inayoendelea kuua mahusiano yako na Mungu, dhana ambayo inazidi kuleta madhara kizazi hadi kizazi. Maana kama wewe mama/baba una dhana hiyo, unafikiri mtoto/watoto wako utawajenga katika msingi gani.

Tukubaliane hapa kwa pamoja, biblia haipaswi kusomwa kienyeji, unapaswa kutulia na kumruhusu Roho Mtakatifu akusaidie kuelewa zaidi maeneo ambayo huelewi. Pia uwe na uhakika kuna vitu hutokaa uelewe kamwe kutokana na kiwango chako, na kutokana na mambo mengine yatabaki kuwa ya Mungu tu.

Rejea: Mambo ya siri ni ya BWANA, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele, ili tuyafanye maneno yote ya sheria hii. Kumbukumbu 29:29 SUV.

Kuanzia sasa ile dhana tuliyoijenga kuhusu biblia na kuona kusoma Neno la Mungu tuwaachie wachungaji, naomba tuifute kuanzia sasa.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.