Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.

Nimekuwa nikieleza hili sana na nitazidi kulirudia siku hadi siku pale tu nitakapopata nafasi ya kufanya hivyo. Hata katika ukurasa 227 wa SOMA NENO UKUE KIROHO nililisemea hili kwa upana mkubwa sana, unaweza kusoma tena kwa kubonyeza HAPAkama hukupata nafasi ya kusoma. Hata kama ulisoma hakikisha unasoma tena huo ujumbe kuna kitu kizuri utakipata, cha kufanya ni kubofya hili Neno HAPA.

Kutafuta kikundi cha kusoma Neno la Mungu kwa pamoja ni muhimu sana sana, na uzuri wake teknolojia imekurahishia hili. Yapo Makundi ya whatsApp ambayo unaweza kuungana na wenzako ukawa msomaji wa Neno la Mungu bila kuishia njiani, ikiwa tu utaheshimu taratibu zilizowekwa.

Nimekuwa mzoefu wa hili kwangu mwenyewe ndio maana nakusisitiza kutengeneza mpango mzuri wa kuungana na kikundi ambacho kitakufanya usome Neno la Mungu hata kama hujisikii kufanya hivyo. Zamani wakati nina hamu sana kusoma Neno la Mungu, nilikuwa nikianza kusoma ilikuwa haichukui hata mwezi ninajikuta nimeacha. Wakati huo nilikuwa sina kundi la whatsApp kunisukuma niweze kusoma Neno wala siku na rafiki ambaye ananisimamia katika hili la kusoma Neno la Mungu.

Nilijikuta naumia sana ila nilikuwa nikijipa siku, yaani nasema nitaanza tena kesho, ikifika hiyo kesho nasogeza tena kesho nyingine, nikianza kidogo najikuta uvivu unaniingia. Mpaka ikafika kipindi nikapoa kabisa na kubaki kuishika biblia yangu siku za ibada tu, mpaka pale nilipoanza kusoma Neno la Mungu na wenzangu. Ndio nikawa nalizimika kutenga muda wa kusoma na kufakari Neno la Mungu kila siku, kuna siku naamka sijisikii kabisa kusoma Neno la Mungu ila naona nitavunja makubaliano yetu tuliyojiwekea.

Uzuri wa kikundi chetu cha kusoma Neno la Mungu, unasoma alafu unatoa kile umejifunza kupitia sura husika mliopo pamoja. Huwezi kusema umesoma alafu usitoe tafakari yako, kwa hiyo kama ulitaka kuingiza uvivu wako unajikuta unajisukuma kusoma ili upate cha kuwaambia wenzako ulichojifunza.

Sasa wakati nipo peke yangu kipindi kile cha nyuma cha kuanza na kuishia njiani, nilijiona nipo peke yangu na wala hakuna anayeniona kama nilikuwa na hili zoezi. Kujipa moyo ule ilinifanya niendelee kutamani kusoma neno la Mungu pasipo kuweka matendo ya uhakika.

Inaumiza zaidi pale unapoona wakristo wengi wanaingia kwenye imani potofu kwa kutojua maandiko Matakatifu, wakifikiri sehemu walipo wanamwabudu Mungu wa kweli kumbe sivyo ilivyo. Hii pia kutosoma biblia imewafanya wakristo wengi kuendelea kuwa wachanga kiroho, kwa sababu ya kutokuwa na Neno la Mungu, hii pia imewafanya wakristo wengi kuendelea kurudi nyuma na kuacha wokovu.

Nilipoangalia sababu kama hizi nilijisikia vibaya sana moyoni, japo mpaka sasa inaniumiza ila namshukuru Mungu amenipa huu mzigo wa kuwaambia watu umhimu wa kusoma Neno la Mungu nikiwa na mimi nafanya hivyo. Najisikia furaha sana pale ninapoona mkristo mwenye safari ya kwenda mbinguni, anasoma Neno la Mungu akiwa anamaanisha anachofanya.

Hutokaa umkute mkristo yeyote aliyeamua kumjua Mungu wake kupitia Neno lake, akiwa ana mambo ya kipuuzipuuzi. Maana kadri anavyozidi kujifunza Neno la Mungu, kuna hekima ndani yake inazidi kujengeka, kuna utoto uliokuwepo ndani yake unazidi kutoweka siku hadi siku. Mpaka unamkuta amekomaa kiasi kwamba anaweza kula chakula kigumu na asipate madhara yeyote.

Mchanga wa kiroho ukimkosea leo, atanuna wiki nzima bila kutaka kuachilia, mchanga wa kiroho asipotembelewa na wapendwa kanisani atanung’unika na kuhama kanisa, mchanga wa kiroho akikemewa kidogo atajiona amedharauliwa na ataacha kwenda kanisani.

Mchanga wa kiroho huyohuyo akiona mhubiri amesimama kuhubiri, kama ujumbe unalenga matendo yake mabaya moja kwa moja ataona anasemwa yeye. Badala ya kujutia makosa yake na kutubu, yeye atajenga chuki na yule mhubiri aliyekuwa anatoa Neno.

Unaweza kuona jinsi madhara yalivyo mengi kwa wakristo wa leo wasiotaka kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Uzuri wa Neno la Mungu linakutengeneza vizuri na kukuweka katika mstari unaopaswa kuwa kama mkristo.

Ninapokuambia kuwa na kikundi cha kusoma Neno la Mungu naelewa nakwambia nini, wengi tunaanza na kuishia njiani kwa sababu hatukujengewa huu msingi mapema wa kusoma Neno la Mungu. Sasa ukianza ukubwani utajikuta unaanza kwa kasi ila baada ya wiki/mwezi unapoteana kabisa.

Nguvu ya kundi ni kubwa sana maana tangu nianze kusoma Neno la Mungu mwaka 2015, sijawahi kuacha mpango huu wa kusoma Neno la Mungu kila siku. Hatua niliyonayo leo haifanani kabisa na wakati sijaanza kusoma Neno la Mungu, naona matunda ambayo wakati naanza nilikuwa nafanya tu na wakati mwingine nilikuwa najiona sipati kitu kikubwa sana. Ila kwa kuwa nilishaungana na wenzangu na mimi ndio kiongozi wao, niliona sio vizuri kuwasisitiza watu kusoma Neno alafu mimi nakuwa mtoro.

Kundi la whatsApp ndio limenifanya nikasoma agano jipya kuanzia kitabu cha Mathayo hadi Ufunuo na nikahamia agano la kale. Ambapo nilianza kitabu cha Mwanzo na sasa nipo kitabu cha Ayubu, hili jambo lingekuwa gumu kama ningekuwa sina hichi kikundi cha Chapeo Ya Wokovu.

Kusoma Neno la Mungu ukiwa na wenzako katika kikundi, ule uvivu wako wote utamezwa kama utakuwa mtiifu kufuata kanuni zilizowekwa kukufanya uwe msomaji wa Neno la Mungu.

Bila shaka umeondoka na jambo la kukusaidia katika kuweka bidii yako ya kujifunza Neno la Mungu, hicho umekipata katika ujumbe huu hakikisha unakifanyia kazi. Haupo kwenye group la whatsApp na unatamani uwepo, tuwasiliane kwa namba nitakazotoa hapo chini.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.