Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, fursa kwetu kwenda kufanya yale ambayo yanamzalizia Bwana matunda yaliyo mema.

Kabla hujaanza kusoma Neno la Mungu uliona ni jambo ngumu sana kwako kulifanya, hiyo ilikuwa kabla hujalianza. Lakini baada ya kuanza kwa hatua ndogo ndogo bila shaka umeanza kuona sio jambo nzito sana.

Hii ni kwa wale waliochukua hatua baada ya kusikia mafundisho ya kuwasukuma kusoma Neno la Mungu, nasema hivyo kwa sababu huenda unasoma ujumbe huu kwa mara ya kwanza na hujawahi kuwa na mpango wowote wa kusoma Neno la Mungu.

Leo nikurudishe nyuma kidogo kwa kujitafakari ulipo sasa na ulipokuwa kabla hujaanza kusoma Neno la Mungu. Nataka uone ni jinsi gani jambo ukilianza linakuwa jambo jepesi kadri unavyozidi kusogea hatua kwa hatua.

Muda mwingine huwa tunajikatisha tamaa wenyewe ila ukianza kusoma biblia, kwa kuweka bidii na nidhamu, unajikuta umefika mbali zaidi. Napenda wewe mwenyewe ujiangalie ulivyoanza na sasa upo vipi, hii itakupa hamasa ya kwenda mbele zaidi katika usomaji wako wa Neno la Mungu.

Muda mwingine unapaswa kujifakari, unapofanya hivyo unaweza kujua mengi sana uliyovuka. Na hayo utakayoyajua katika kutafakari ndio yatakuwa daraja lako la kukuvusha maeneo mengine zaidi uliyoanza kukata tamaa.

Mfano wakati unaanza kusoma biblia ulikuwa huelewi chochote zaidi sana ukibahatisha unapata mistari miwili au mitatu kati ya mistari 50. Mwanzo hili jambo lilikuumiza na kufika wakati kufikiri uache kabisa kusoma Neno la Mungu, lakini ulijipa moyo na umejikuta ufahamu an akili zako zimefunguka zaidi, tena nzuri zaidi unafunguka siku hadi siku.

Mfano mwingine labda wakati unaanza kusoma Neno la Mungu uliona biblia ni kubwa sana, ambapo ulikuwa ukiitazama kwa nje ilivyojaza makaratasi mengi. Ulikuwa unafika kipindi unaona ni jambo ambalo lipo nje ya uwezo wako, lakini ulivyoanza kuisoma biblia yako mpaka sasa huenda umeanza kusahau na ukubwa/ujazo wa biblia yako.

Mfano mwingine labda wakati unaanza kusoma kitabu cha Zaburi au kitabu chochote kile ulichoanza nacho, uliona kina sura nyingi sana. Ila tangu uanze na kufikiri kesho nitasoma sura fulani, mpaka sasa umefikia hatua nyingine kubwa. Ambapo huwazi tena Zaburi ina sura nyingi badala yake unawaza kujua mwendelezo wa kesho upoje.

Labda nikufikirishe kidogo kwa kutolea mfano mwingine, umewahi kufikiri kuangalia movie yenye season 100? Bila shaka ukitamkiwa movie fulani inavipengele mpaka 100 unaweza kupata uvivu wa kuanza kuifuatilia. Ila cha kushangaza mtu anakuwa mtumwa wa kujua nini kitaendelea kwenye sehemu ya pili, na wala hawazi tena kuhusu wingi wa season wala hawazi tena gharama ya fedha anayotoa kununua DVD.

Wengine ni wale wa kufuatilia thamilia, wanakuwa makini sana kufuatilia nini kitaendelea katika sehemu inayofuata kuliko hata kufuatilia Neno la Mungu. Nakukumbuka niliwahi kuwa mtumwa wa hili mwaka 2007/2008. Ila nilijitoa haraka sana maana nilijiona nakuwa mtumwa kwa kitu ambacho naweza kuacha.

Nazungumza kuhusu kuanza jambo, unapodhamiria kutoka ndani ya moyo wako, haijalishi utakutana na changamoto ngumu kiasi gani. Unapaswa kujua ukiamua kutoka ndani ya moyo wako, hakuna jambo litashindikana. Ule ulevi wa kufuatilia movie/tamthilia, unaweza kugeuza ukawa msomaji na mfuatiliaji mzuri sana wa Neno la Mungu.

Muhimu sana ni wewe kuanza, kwenye kuanza kuna faida kubwa sana kuliko kuongea maneno matupu bila vitendo vyovyote. Zingatia sana hili ili uwe miongoni mwa watu ambao walikuwa hawapendi kusoma Neno la Mungu na sasa wanasoma Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutafakari zaidi kuhusu kuanza kusoma Neno la Mungu.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

www.chapeotz.com

+255759808081.