Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Fursa kwetu kwenda kuweka alama njema kwenye mioyo ya watu wengine, ambayo italeta kumbukumbu njema mbele za Mungu na wanadamu.

Jambo usipolijua unaweza kufikiri ni jipya, kumbe sio jipya lilikuwepo tangu zamani isipokuwa wewe hukuwahi kujua kama lipo. Mambo mengi sana yanayotutokea leo yapo ndani ya biblia, kwa kuwa hatuisomi hatuwezi kujua kama yapo.

Tunaweza kufikiri changamoto zinazotutokea leo, hazijawahi kuwepo kwa mkristo yeyote yule, utakuwa unajidanganya kwa kutojua kwako Neno la Mungu. Lakini ungejua neno la Mungu isingekupa shida sana pale utakapotokewa na jambo la kukuumiza moyo wako.

Wakati mwingine tumeyabeba mambo mbalimbali mioyoni mwetu, kwa sababu tu ya uchanga wa kiroho. Kwa sababu tu ya kutokuwa na Neno la Mungu, unaweza kutengeneza chuki kwa kutokuwa na maelekezo muhimu ndani ya biblia.

Kwa mfano unaweza kumwamini sana ndugu/rafiki yako, ukawa unampa baadhi ya siri zako ila baadaye mkapishana kidogo kauli akaenda kutoa siri zako zote nje au mnaweza msikosane lakini akakugeuka.

Unaweza kujitoa kwa ndugu yako ukampa msaada wa hali na mali kuhakikisha anafanikiwa Kwenye maisha yake. Labda alikuwa anahitaji kusomeshwa ukajitoa ukamsomesha, ikafika siku moja akakufanyia kitu ambacho unaweza ukapata mshangao ambao hukufikiri kama angekufanyia baya la namna hiyo.

Labda unaweza kumtegemea ndugu yako atakusaidia jambo fulani, ukaweka asilimia zote kuwa yeye anaweza kusimama na wewe ukafanikiwa. Huyo ndugu/mzazi/mlezi wako ukaenda naye vizuri ila ikatokea akakata mawasiliano na wewe, na kusimamisha msaada aliokuwa anatarajia kukupa.

Usipoelewa Neno la Mungu linasemaje, utajenga chuki naye mpaka utajishangaa umeokoka kweli ila kuna vitu una kinyongo navyo ndani yako. Kama mtu uliyemwamini na ukampa siri zako, leo hii anakugeuka na kufanya yale aliyoyajua kwako ndio fimbo yako ya kukuchapia nayo, huyo si hatari sana.

Unaweza kufikiri ninachosema hapa ni uongo, labda nimekitunga tu kichwani, hebu soma andiko hili utaelewa ninachosema zaidi.

Rejea: Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake. ZAB. 41:9 SUV.

Umeona hapo, msiri wako anaweza kuwa mke wako, anaweza kuwa mume wako, anaweza kuwa mchumba wako, anaweza kuwa mama yako, anaweza kuwa baba yako, anaweza kuwa mchungaji wako. Ikafika siku akakugeuka kwa kutumia yale mambo nyeti anayoyajua kuhusu wewe, akaanza kuyasambaza kwa watu wa nje.

Unaweza kuwa ulimfadhili rafiki yako ukampa chakula akala, unaweza ulimfadhili rafiki yako ukampa kila hitaji. Ikifika siku akakugeuka, nakwambia usipokuwa na Neno la Mungu la kutosha moyoni mwako, utateseka siku zako zote kuhusiana na huyo ndugu.

Ipo pia unaweza kusikia kuna ndugu zako wanakuombea ufe ili wao wamiliki mali zako, unaweza kupata taarifa kuwa watoto wako wanafanya kila njia kukuua wamiliki mali zako.

Unaweza kufikiri mke/mume wako yupo pamoja nawe katika shida, kumbe anakuombea ufe ili yeye amiliki mali zako ulizozitafuta kwa jasho lako.

Unaweza kufikiri unachofanya kazini kwako, kinampendeza kila mtu, kwa vile unavyofanya kazi na kupandishwa zaidi viwango. Ukaona nafasi uliyonayo wenzako watakuwa wanakupenda, kumbe wao wanakuombea ufe hata leo wakalie kiti ulichokalia wewe.

Usipoelewa Neno la Mungu kuhusu hili, utagombana nao sana pale utakaposikia walijaribu na kukuwekea sumu kwenye chakula/chai ufe. Usipongombana nao unaweza kupata hofu kubwa ikakuondoa kwenye ile bidii yako.

Rejea: Adui zangu wananitaja kwa maneno mabaya, Atakufa lini, jina lake likapotea? Na mmoja wao akija kunitazama asema uongo, Moyo wake hujikusanyia maovu, Naye atokapo nje huyanena. Wote wanaonichukia wananinongona, Wananiwazia mabaya. ZAB. 41:5‭-‬7 SUV.

Unaweza kufikiri washirika wako wanakupenda sana kwa jinsi wanavyokuletea habari za kuhusu watu fulani. Kumbe wanakupa taarifa za uongo ili kukuchota akili zako, badala yake unawamwagia vitu vya ndani zaidi wanapeleka kwa wapinzani wako.

Unaweza kuona unakubalika na mfanyakazi wako anayekuletea habari mbalimbali za wafanyakazi wenzake. Kumbe ana agenda yake binafsi, ambapo anachukua maneno kwako na kupeleka kwa wale wale aliokuletea taarifa kuwa ni wabaya wako.

Yote hayo biblia imeyaweka wazi, tunaweza kuona wambeya wameanzia kwako, unaweza kuona wachonganishi hawakuwepo kabisa. Biblia imewazungumza vizuri kabisa, kwa kifupi hakuna jipya unaliona wewe ambalo biblia halikulisema.

Kila tabia mbaya ilishasemwa, kila tabia nzuri nayo ilishazungumzwa. Ukiwa na maarifa ya namna hii, hutoyumbishwa imani yako kwa jambo lolote litakalokutokea.

Weka bidii na nidhamu katika kulisoma Neno la Mungu, lina maarifa mengi kuliko unavyofikiri wewe. Biblia ni kisima cha kisichokauka, ukihitaji kujua mengi zaidi utayapata ndani ya biblia yako. Hata hali ya nchi tuliyonayo sasa maelezo yake yapo ndani ya biblia.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutafakari zaidi kuhusu biblia.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

www.chapeotz.com

+255759808081.