Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.

Kila mmoja ana maswali ambayo yanamtatiza kwenye ufahamu wake, maswali haya yanaweza yakakufanya ukahalalisha jambo fulani lisilo sahihi mbele za Mungu. Vilevile maswali haya yanaweza yakakufanya ukashindwa kufuata kile Mungu anakutaka ukifuate.

Maswali haya yametufanya tulio wengi kubaki njia panda kuhusu imani yetu ya kikristo, mwingine anaweza kuwa yupo yupo kanisani ila ukimuuliza kwanini umeokoka anaweza asiwe na sababu haswa ya kuokoka. Na wengi ambao tuna sababu za kuokoka bado tuna maswali ambayo muda mwingine yanatupa mashaka kuhusu imani yetu.

Wakati mwingine tumejaribu kuwauliza wenzetu waliokoka siku nyingi, majibu wanayotupa bado tunaona hajafikia kiwango fulani tunachotaka kufikishwa. Muda mwingine tumejaribu kuwahoji wachungaji wetu, ila tunaona majibu wanayotupa yapo nusunusu.

Kwa taswira hii tunajikuta tunahangaika ndani ya mioyo yetu, tunashindwa kujua ipi ni mbichi na ipi ni mbivu. Tunafika wakati tunaanza kusema, bora kuokoka ukiwa duniani ukaenda kumkosa Mungu siku ya mwisho, kuliko kutokuokoka ukaenda kumkuta Mungu anayesemwa.

Mtu anayesema hivyo maana yake hana uhakika na imani yake, na Mungu anayemwamini yupo kweli au hayupo. Maana mpaka kusema hivyo ujue amejiuliza maswali mengi sana juu ya Mungu anayemwamini akashindwa kupata majibu.

Ninazo habari njema kwako, Lipo suluhisho la haya yote, maswali yote uliyonayo wewe unaweza kujibiwa na Neno la Mungu. Sio utani nakueleza ukweli, mimi ninaweza nisikujibu kama ulivyotaka nikujibu ila kupitia usomaji wako wa Neno la Mungu, Mungu anaweza kukujibu maswali yako na kupitia mafundisho ya Neno la Mungu unaweza kupata ufafanuzi wa mstari fulani uliokutana nao ukashindwa kuelewa.

Kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu ndivyo unavyozidi kufunguka zaidi na kupunguza baadhi ya maswali uliyokuwa nayo. Utaona mabadiliko ndani yako, na utaondoka eneo la maswali hatua kwa hatua, na kuibua mambo mengine zaidi ya kukufanya uingie ndani zaidi.

Yapo maswali ukiuliza mtu anajua moja kwa moja huyu bado mchanga kiroho na yapo maswali ukiuliza mtu anajua kabisa huyu kakomaa kiroho. Tena ukiuliza swali ambalo muulizaji atakuelewa haraka nia yako ni nini, atakujibu vile ulitaka ujibiwe au anaweza kutaka kwanza uelewa wako juu ya hilo ulilouliza.

Najua hapo ulipo una maswali mengi ambayo mengine unashindwa umuulizeje mtu mwingine, kila ukijaribu kuweka sentensi zako vizuri ili yule unayemuuliza akauelewe unajikuta unapelea sehemu fulani. Njia sahihi ya kuondoka katika mahangaiko haya ni wewe kuamua kusoma Neno la Mungu kwa bidii.

Neno la Mungu linakupika hatua kwa hatua kadri unavyozidi kujifunza, utashangaa ulivyokuwa jana sivyo ulivyo leo. Hii inakufanya kuendelea kuondoka kwenye utata fulani uliokuwa nao ndani mwako. Na kitakacho kuondoa ulipo ni kujitoa kwako kusoma biblia.

Maswali uliyonayo yaweke moyoni mwako huku ukiendelea kujifunza Neno la Mungu, yatajibiwa moja baada ya jingine. Na mengine utaanza kujicheka mwenyewe kwa jinsi ulivyokuwa na ufahamu mdogo kushindwa kunyambua mambo madogo.

Biblia yako ni jibu kwa kila swali ulilonalo, ukiwa na tabia ya kuisoma kwa bidii na kupata muda wa kutafakari zaidi yale uliyojifunza. Utaondoka na vitu vingi sana ambavyo vilikuwa vinakutatiza hapo awali.

Bila shaka umepata mwanga na kujua njia ipi sahihi ya kukusaidia kuondoka kwenye utata uliokuwa nao. Endelea kusoma biblia kama ulikuwa unaisoma, na kama ulikuwa husomi, anza sasa kuisoma.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovukwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

www.chapeotz.com

+255759808081.