Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Tumrudishie sifa na utukufu kwa kwenda kumzalia matunda yaliyo mema kwa zawadi hii aliyotupa ya uzima.

Katika maisha yetu ya kila siku, eneo lolote unapokuwepo, iwe kazini, iwe kwenye biashara zako, iwe kwenye huduma ya kiroho, iwe katika familia yako, iwe katika masomo yako darasani. Kuna vitu lazima viwe kipaumbele chako, kama ni shuleni/chuoni kuna masomo yako baadhi utakuwa umeyaweka kipaumbele sana kuliko mengine.

Iwe katika familia, kuna vitu lazima vitakuwa vipaumbele vyako. Hata itokee nini lazima utajikuta unajilazimisha kukifanya hicho kitu, maana ndani yako unakipenda na una amani kujitoa kwa hali yeyote ile kukifanya hicho ulicho dhamiria kukitenda.

Vipaumbele vya kitu chochote vinatokana na umhimu/uzito wa jambo lenyewe analolipa mtu, jambo linapokuwa lina uzito zaidi kuliko lingine. Lazima mambo mengine yasimamishwa ili kitu/jambo lile liweze kufanikiwa.

Yanaweza kujitokeza mambo mengine mengi zaidi ila kama sio kipaumbele chako, yanaweza yasiuguse sana moyo wako. Ila ikitokea jambo ambalo ni kipaumbele chako hata kama halikuwepo kwenye ratiba zako muda huo, utaona linapata nguvu la kusitisha mengine na kwenda kulifanya.

Kulipa jambo kipaumbele au kwa maana nyingine tunaweza sema kuliweka jambo mstari wa kwanza, inaweza kutokana na usipolifanya hilo jambo kuna madhara yatatokea. Sasa unajikuta unajisukuma kulifanya hilo jambo ili kuokoa hasara itakayotokea kutokana na kutowajibika kwako.

Pia unaweza kulipa jambo kipaumbele kutokana na jinsi unavyoelewa umhimu wa lile jambo, unapojua umhimu wa jambo lolote lile. Hata namna ya kufikiri kwako juu ya hilo jambo kunabadilika, utakuwa na mtazamo chanya kila wakati hata pale itakapotokea umevunjwa moyo.

Kama huna vipaumbele katika maisha yako, unapaswa kuanzia sasa uweke vipaumbele eneo lolote lile ulipo sasa. Usipokuwa na vipaumbele vyako, utakuwa mtu wa kutangatanga/kuyumbishwayumbishwa kila wakati.

Sijui kama unanielewa hapa jambo ninalokueleza, ninazungumza kuhusu vipaumbele vyako ni nini. Kile unaweza sitisha mambo mengine ili chenyewe kifanikiwe hicho tunaweza sema ni kipaumbele, kile usipokifanya unasikia kelele ndani mwako mpaka umekifanya ndio unaona moyo wako umetulia. Hicho tunaweza sema ni kipaumbele chako.

Kile kinakufanya uamke asubuhi na mapema ndio kipaumbele chako cha siku, kile kinakufanya uwahi ofisini na uchelewe kanisani hicho ndicho kipaumbele chako, kile kinakufanya utafute kila mbinu kifanyike lakini mengine huwa huumizi hata kichwa ujue hicho ni kipaombele chako.

Tunapokuja kwenye maisha yetu ya wokovu, tunapaswa kuelewa vipaumbele vyetu ni nini. Vipo vitu vinatulazimu kuviweka mstari wa mbele hata kama hatuvipendi, na vipo vitu sio lazima viwekwe vipaumbele kutokana na jinsi vilivyo.

Ikiwa hutoweka kipaumbele cha kusoma Neno la Mungu katika maisha yako ya wokovu, kitu gani unafikiri kitakuwa cha maana sana kwako kukifanya pasipo kuwa na Neno la Mungu. Kama ni kuimba utahitaji uwe na neno la Mungu vinginevyo utawaambia watu vitu visivyofaa, kama ni kuhubiri/kufundisha utahitaji kuwa na Neno la Mungu vinginevyo utaanza kusema kwa hekima za kibinadamu tu.

Kama umeamua kumpendeza Mungu na kuishi maisha safi katika Kristo, ni lazima kipaumbele chako kiwe Neno la Mungu. Na Neno la Mungu sio kununua biblia na kuifanya ya kwendea nayo kanisani, na sio kuifanya ya kutafutia mistari michache ya kusimamia wakati unahubiri/unafundisha, ni kwa ajili ya kusoma kilichoandikwa ndani.

Ukishaliweka Neno la Mungu ni kipaumbele chako, uwe na uhakika maeneo yako yote katika maisha ya kimwili na kiroho yatakuwa salama kabisa. Maana ndani ya Neno la Mungu lipo neno la kuonya, lipo neno la kufundisha, lipo neno kukemea, na lipo neno la kukusukuma uwabijike katika nafasi yako.

Kama hili la kusoma NENO LA MUNGU sio kipaumbele chako na umeokoka na una safari ya kwenda mbinguni, itabidi ujihoji upya kuhusu uamzi wako. Usipofanya hivyo kuna hatari kubwa sana kutomzalia Mungu matunda yaliyo mema, tena unaweza kumkosea Mungu pasipo hofu yeyote.

Hadi hapo utakuwa umepata kitu cha kukusaidia katika kuweka vizuri mipango yako ya siku ili uweze kusoma Neno la Mungu. Hili ni muhimu sana kulizingatia na kulifanyia kazi, ili ufike wakati uone umhimu wa jambo hili la kusoma Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.