Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, atupaye kushinda.

Kila jambo unalolifanya unapaswa kuwa na tathimini, imani yako uliyonayo juu ya Yesu Kristo unapaswa kufanyia uchunguzi kama kweli ipo sawa. Tathimini hii unaweza kuifanya kirahisi pale unapokutana na changamoto ngumu, je uwezo wako wa kukabiliana na changamoto hizo unao au huna kabisa.

Unajijua mwenyewe hapo ulipo una stamina kiasi gani za kuweza kukabiliana na magumu au huwa unajikuta unapandisha tu presha au huwa unaanza kutafuta kilevi ili kupoteza mawazo. Unajijua mwenyewe ukipatwa na vikwazo huwa unatafuta kukaa chini kupata suluhisho au huwa ndio mavurugano mwanzo mpaka mwisho.

Kama huna uwezo wa kukabiliana na changamoto ngumu, na hizo changamoto ukajikuta zinakuondoa kwenye uwepo wa Mungu.Yaani ukajikuta hutamani tena kuendelea na wokovu kwa sababu ya kwazo fulani ulilokutana nalo. Au ukajikuta unawakasirikia tu wale waliokukosea na huna mpango wa kuwasemehe kwa waliyokutendea, fahamu kwamba bado hujakua kiroho badala yake utakuwa mchanga kiroho hata kama una miaka 20 kwenye ukristo.

Mtu aliyekua kiroho utamjua kwa matendo yake, ni mwepesi wa kuachilia wale waliomkosea. Na yule asiyekua kiroho utamwona ni mgumu kuachilia waliomkosea, hujiona kosa alilokosewa haliwezi kusameheka kirahisi mpaka atakapolipiza kisasi.

Mtu aliyekomaa kiroho anaweza kusikia jambo la kumuumiza moyo wake, atapambana kuhakikisha mambo yanakuwa sawa. Wakati mwingine unaweza usijue kama kuna changamoto ngumu anapitia, kwa jinsi alivyo kwenye mwenekano wake na utendaji wake wa kazi zake.

Wakati yule asiyekomaa kiroho hawezi kujishughulisha kutafuta kumaliza tatizo bali kuendeleza tatizo. Bora uwe mwepesi kuzuia tabia fulani mbaya inayojitokeza mbele yako kama mazingira yatakuwa salama kufanya hivyo.

Mtu aliyekomaa kiroho anaweza kuvurugwa sasa hivi na jambo fulani, ukamwangalia kwa jinsi ya kawaida ukaona mpaka kuja kutulia labda itachukua wiki nzima. Ila kwa aliyekomaa kiroho jua haliwezi kuzama kabla hajatafuta amani ya moyo wake, na mwingine aliyepanda kiwango cha ukomavu wa kiroho haipiti masaa mengi sana utamkuta amerudia kwenye hali yake ya kawaida.

Hili zoezi la kujijua kama umekomaa kiroho au bado hujakomaa kiroho, unaweza kulifanya mwenyewe kwa kujitazama matendo yako mwenyewe. Sio zoezi gumu sana, jiangalie kiwango chako cha kuachilia mambo, jiangalie kiwango chako cha kuomba msamaha waliokukosea wewe kipo vipi, jiangalie kiwango chako cha kubeba mambo na kutoonyesha kila mtu kuwa umevurugwa.

Ukishajiona una tabia moja wapo ambayo imekung’ang’ania, cha kufanya ni kuongeza bidii ya kusoma Neno la Mungu. Jaza maarifa ya Neno la Mungu kwa kadri uwezavyo, ipo nguvu katika maandiko matakatifu.

Kuna jambo lilimtokea rafiki yangu siku ya jpili ya tar 23/7/17, nikalisikia hilo jambo lililomkuta. Sikuwa na haraka ya kumweleza nikajiahidi nitatafuta muda mzuri wa kumweleza nilichosikia kuhusu yeye. Kumbe wakati nafikiri hajasikia hilo nililoelezwa, kumbe alikumbana nalo uso kwa uso, nimekuja kulijua hili jana usiku wakati ananieleza kilichomkuta siku ya jpili nami nikamwambia nilikuwa najipanga kuja kukuambia.

Nilichomwambia rafiki yangu huyu ni kwamba amekomaa kiroho, maana mazingira aliyokuwepo alipaswa kuonyesha hayupo sawa. Ila yeye aliifunika hiyo hali mpaka mimi mwenyewe kushindwa kujua kilichompata muda mchache uliopita wakati sipo naye karibu.

Neno la Mungu halikufanyi tu uwe na uwezo wa kubishana na mataifa wanaomkataa Mungu wa kweli, hili nalisemea mara nyingi sana. Neno la Mungu linakujenga na kukuimarisha katika maeneo yote mawili, kimwili na kiroho. Kama upo vizuri kiroho alafu kuna baadhi ya mambo unashindwa kukabiliana nayo, unapaswa kuongeza bidii ya kujaza maarifa ya Neno la Mungu moyoni mwako.

Tamani kusogea hatua moja kiroho kila siku, kataa kabisa kubaki vile vile kila siku. Uchanga wa kiroho usiwe juu yako ndugu yangu katika Kristo, yaani aliyekuona mwezi uliopita akisema upo vizuri mfanye akikutana na wewe tena mwezi huu akuone unazidi kuwa wa tofauti zaidi.

Bila shaka umepata kitu cha kukusaidia katika kuweka umakini katika usomaji wako wa Neno la Mungu, umejua faida ya Neno la Mungu ipo vipi. Vizuri sana ukayafanyia kazi yale uliyojifunza katika ujumbe huu,haitakuwa na maana kusoma na kuyaacha hapa.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutafakari zaidi yale uliyoona ni muhimu kwako. Pia Usiache kutembelea mtandao wetu wa Chapeo Ya Wokovu, kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.