Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, hongera kwa kupata kibali mbele za Mungu cha kuweza kuiona siku ya leo. Mshukuru Mungu kwa kibali hichi maana si wote wameweza kukipata, wapo walitamani kuwepo leo ila haikuwezekana.

Kuna dada mmoja ndani ya Chapeo Ya Wokovu whatsApp group, nilikuwa namfuatilia kwa karibu sana kutokana na jinsi alivyonifanya nimfuatilie. Alikuwa vizuri kweli ila alikuwa mchanga sana kiroho, kadri siku zilivyokuwa zinazidi kwenda mbele nilimwona anazidi kubadilika taratibu.

Unajua mtu mchanga kiroho usipomwelewa haraka ni rahisi sana kukukera muda wowote. Maana yeye huwa hawezi kujua kutumia ile hekima kutokana na mazingira anayoyaona wakati huo, hata kama amejaza maarifa ya dunia. Kama wokovu ameuza muda sio mrefu na bado Neno la Mungu halimo ndani yake, ujue lazima atakuwa na mapungufu mengi sana.

Sasa huyu dada alikuwa anafanya vitu vingi ambavyo vilinivuta kuendelea kumfuatilia ili nijue mwisho wake utakuwaje. Nilichokuwa nachunga ni asiache kusoma Neno la Mungu kila siku, na asije akatoka group la Chapeo Ya Wokovu ambalo tunasoma Neno la Mungu kwa pamoja.

Mungu ni mwema sana, kadri siku zinavyozidi kwenda mbele, nilimwona anazidi kubadilika taratibu. Ile miondoko yake ya uchanga wa kiroho ilizidi kubadilika taratibu na kuanza kuwa mtu makini na anayeonyesha ameanza kukomaa kiroho.

Leo ninapokuandikia haya nimejiridhisha kwa asilimia kubwa sana kuwa huyu dada amekuwa vizuri kabisa tofauti na siku zile za mwanzo. Kama unakumbuka nilisema sio kwamba alikuwa hajaokoka, nilichosema kuokoka alikuwa ameokoka ila kuna vitu alikuwa anavifanya vya kitoto sana.

Hali hii anayo kila mtu ambaye anaanza wokovu na yule ambaye yupo ndani ya wokovu ila hajishughulishi kujaza maarifa mbalimbali ya Neno la Mungu. Hata kama yupo ndani ya wokovu miaka 20 au 30 kama hana muda wa kusoma Neno la Mungu na kutafakari yale anajifunza, na kama hana muda wa kuhudhuria mafundisho ya Neno la Mungu. Hali yake ya kiroho itakuwa ipo vizuri ila sio kwa kiwango ambacho anapaswa kuwa nayo mkristo aliyemwamini Yesu Kristo miaka mingi.

Huyu dada kilichomsaidia ni kuwa na bidii ya kusoma Neno la Mungu, kama ataendelea na bidii yake hii nina uhakika atakuwa na viwango vya tofauti. Maana najua yupo vizuri sana ila alikuwa na mapungufu ya kutokuwa na Neno la Mungu la kutosha.

Elewa kwamba sio mara zote unaweza kujitambua kuwa wewe ni mchanga wa kiroho, muda mwingine unaweza kujiona upo vizuri sana. Na mara chache sana unaweza kujiona upo chini sana unahitaji bidii zaidi ya kuutafuta uso wa Mungu, na ili ujijue haraka kuwa kiwango chako cha kiroho bado hakijakua vizuri, ni pale unapokuwa katika kundi. Mnapokuwa katika kundi la watu wengi alafu mkawa mnafanya jambo moja, ni rahisi sana kujitambua kwa kujipima kiwango chako cha kiroho.

Ukiwa mwenyewe mwenyewe na ukawa na uhakika umejazwa Roho Mtakatifu, nakwambia utajiona umemaliza kila kitu. Kumbe huyo Roho Mtakatifu aliye ndani yako unapaswa kumtumia akusaidie kulielewa haraka Neno la Mungu. Maarifa ya Neno la Mungu ndio yanakufanya ukue siku hadi siku, uondoke hatua moja kwenda hatua nyingine.

Ukikaa bila kusoma Neno la Mungu, ukawa unasubiria siku za jumapili ndio ukamate biblia yako, utaendelea kubaki na hali yako ya uchanga wa kiroho. Kwanini uendelee kujichelewesha wakati uwezo unao wa kutenga muda wako kusoma Neno la Mungu, nini kinakufanya uendelee kubaki kwenye uchanga wa kiroho wakati uwezo wa kusoma unao, na wakati Roho Mtakatifu yupo ndani yako.

Achana na uvivu wako, anza leo kuweka bidii katika kulisoma Neno la Mungu, na kama ulishaanza weka mkazo zaidi. Ipo faida kubwa mno kusoma Neno la Mungu, Neno la Mungu linaondoa utoto mwingi sana wa kiroho na kukufanya kuwa mkristo imara mbele za Mungu.

Bila shaka umepata kitu cha kukusaidia katika kuweka umakini na mipango imara katika usomaji wako wa Neno la Mungu. Nakusisitiza tena hakikisha Neno la Mungu linakuwa sehemu ya maisha yako yote.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutafakari zaidi kuhusu yale umesoma hapa.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.