Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kutuamsha salama. Haijalishi jana ulilaje na leo umeamka ukiwa mchovu, bado unapaswa kumshukuru Mungu. Maana wapo walilala na mipango mikubwa lakini hawakuweza kuamka tena.
Leo nimeona nianze na kichwa cha somo chenye kukufanya ujihoji mwenyewe ndani mwako, huenda hukuwahi kufikiri hili na kama uliwahi kufikiri huenda hukuzama kwa undani zaidi. Kupitia ujumbe huu unaenda kuondoka na vitu vya kukujenga na kukusaidia kujua umhimu wa kusoma Neno la Mungu.
Miaka miwili iliyopita, nilipatwa na jaribu ambalo lilinifanya muda mwingine nikose usingizi mzuri kutokana na maumivu niliyokuwa napitia. Ulikuwa ukinitazama ilikuwa sio rahisi kujua kwa haraka, hata kama ungekuwa mtu wangu wa karibu.
Ila ungeweza kunijua kama utakuwa makini sana na mimi, maana nilikuwa najikaza sana ila nafika muda najisikia vibaya mno. Ninapokutwa na hiyo hali unaweza kuniona kama nimezubaa/nimekanda fulani, si umewahi kuona mtu mpo naye sehemu moja mnaongea mambo fulani ila yeye hayupo pamoja nanyi kimawazo.
Mara nyingi unaweza kukutana na hali kama hizi hata darasani, kanisani, mikutano/semina, pale utakapotaka kujua kama watu wanakusikiliza. Unaweza kumuuliza mtu nimesamaje, hapo unaweza kumshtua na akakuambia sikusikia! sio kwamba hakusikia akili zake hazikuwa eneo la tukio.
Ndio maana kama mchungaji/mwalimu wa Neno la Mungu, unapaswa kujua kusoma watu ulionao wanakusikiliza au wameweka miili yao pamoja na wewe, ila mawazo yao hayapo pamoja na wewe.
Sasa wakati napita kwenye moto huo wa mateso ya moyo wangu, nilijifunza mambo mengi sana na niliimarika sana kiroho wakati huo. Maana nilikuwa nachukua muda mwingi kumtafakari Mungu, nilijifunza pia kujenga umakini ili kulinda mtu asije akajua hali ninayopitia. Nilichagua watu wachache wakuwashirikisha mzigo niliokuwa nao, ambao walipata kibali ndani ya moyo wangu.
Wakati naendelea kuugua moyoni, kuna siku nipo pafuni naoga, sijui ilikuwaje ila kuna wazo lilipita kwa nguvu na kuniuliza swali hili kwa upole kabisa. Hivi wewe si uliomba Mungu akufanyie jambo hili? Nilijibu ndio. Nikaulizwa tena mbona unahangaika sana na wakati uliomba?
Huwezi amini baada ya majibizano hayo ya ndani kwa ndani ambayo yalikuja kwa namna ya wazo fulani nilipata nguvu za ajabu. Nilitoka kuoga nikiwa na furaha ya kipekee sana, ambapo mtu angenitazama wakati naingia bafuni na wakati natoka bafuni, angejiuliza maswali mengi sana.
Kumbuka hili jambo lilinitesa kama miezi nane hivi, nilikuwa kila nikiingia kwenye maombi naliombea lenyewe kwa muda mrefu. Maana nilikuwa niliona ni kitanzi kwangu, muda mwingine nilikuwa naliona kama limeisha ila kila nikiingia kwenye maombi nasikia mzigo wa kuliombea.
Siku nakuja kukumbushwa kile niliomba unajua sikuumia tena, na hapo hapo nikajifunza kumbe mambo mengi tunamwomba Mungu alafu tunakuwa hatuna stamina/uwezo wa kupokea majibu yake. Hili nimeliona kwa wakristo wengi sana, na kila siku naendelea kuwaona watu wanateseka sana, ukifuatilia unakuta yeye mwenyewe ndio aliomba Mungu amsaidie.
Labda unajiuliza utawezaje kuondoka kwenye shida hii ya kuhuzunika pale Mungu anapokujibu badala ya kufurahia Mungu kukujibu hitaji lako wewe unaumia. Jibu ni kwamba, lazima ujaze Neno la Mungu kwa wingi moyoni mwako, unapokuwa na Neno la Mungu inakuwa rahisi kwako kupata picha kamili ya majibu yako.
Wakati mwingine mpaka kuja kuona majibu halisi ya jambo ulilokuwa unamwomba Mungu akutendee, Mungu huanza kutengeneza mazingira ya mbali. Ambayo wakati mwingine yanaweza kugharimu baadhi ya vitu vyako ulivyokuwa unavipenda, kumbe hivyo vitu ulivyokuwa unavipenda ndio vilikuwa kikwazo kwako. Sasa Mungu akitaka kukujibu lazima aviondoe kwanza ndipo jibu lako liwe wazi.
Wengi tunakwama eneo hili, badala ya kufurahia Mungu ametujibu, tunaanza kulia na kulaumu tena. Tunafanya hivi kwa sababu bado wachanga kiroho, kama tungekuwa wakomavu kiroho tusingerudi kumnung’unikia Mungu aliyetujibu haja ya mioyo yetu.
Usifikiri kila jibu linakuja kwa picha ya moja kwa moja, majibu mengine yanaanzia mbali sana mpaka kuja kuwa jibu kamili. Nakwambia kama hukujipanga utajikuta umeteseka sana. Jambo lingine la muhimu sana ni kumwomba Mungu akupe stamina za kupokea majibu ya mahitaji yako, hili linaambatana sana na ukomavu wako wa kiroho ila ni muhimu kujenga nguzo imara.
Hakikisha Neno la Mungu linabadili fikira zako changa na kuwa na fikira safi zilizokomaa, ili usiwe mhitaji alafu ukipewa unaanza kulalamika kwanini umepewa. Ili kujiondoa kwenye kundi la walalamishi wa majibu ya mahitaji yao wenyewe, hakikisha Neno la Mungu linakuwa chakula chako cha kila siku.
Neno la Mungu lina namna ya kukumbusha haraka na kukurudisha pale unapotaka kufikiri vibaya, na kujua hilo linalokupata ni maandalizi ya kupokea jibu lako halisi ulilomwomba Mungu miaka mingi.
Bila shaka kuna kitu umekidaka na kimekuongezea hatua zingine mbele, mshukuru Mungu kwa sababu ana namna ya kujibu watu wake. Huenda hapo ulipo umetolewa kwenye usingizi mzito sana kupitia mafundisho haya.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa Chapeo Ya Wokovu. Utapata masomo mengine mazuri zaidi ya kukupa hamasa ya kusoma Neno la Mungu.
Chapeo Ya Wokovu.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.