Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, atupaye kushinda kila siku.

Tunaposema soma Neno la Mungu ukue kiroho, tunamaanisha kweli tunachokisema. Usije ukafikiri tumekosa kazi za kufanya ndio maana tunahangaika na hili jambo, naweza kukuambia hii ni moja ya kazi kubwa sana yenye mshahara mkubwa ambayo Mungu ndiye atakayeulipa huo mshahara.

Tuna changamoto kubwa kwa wakristo wengi wasiopenda kujifunza Neno la Mungu, wanapoacha kujifunza wanakuwa vile vile mwaka hadi mwaka. Huwezi kuona mabadiliko yeyote juu yao, kwa sababu wameona kuokoka imetosha hawahitaji kitu kingine tena.

Kuokoka ni vizuri sana, ila hatuwezi kuacha kulisha mioyo yetu Neno la Mungu, hata kama tunajiona hatumtendi Mungu dhambi. Dhambi sio uzinzi tu, dhambi sio uasherati tu, dhambi sio ulevi tu, dhambi sio wizi na kupokea rushwa. Hata kuwa sehemu ya makwazo kwa wenzako nayo ni dhambi.

Haiwezekani kila mtu anasema wewe huna kauli nzuri, kweli wapo watu hawajui kutofautisha kauli ipi ina maonyo, kauli ipi ina mafundisho, kauli ipi inakemea. Mimi sisemei hao wanaopenda kuambiwa maneno malaini lani kila saa hata kama wanakosea wanataka kuambiwa maneno yale yale matamu.

Tunaweza kuwafananisha na wale wazazi wanaopenda watoto wao mpaka kufikia hatua ya kushindwa kuwachapa fimbo. Wakifikiri kutomchapa mtoto kunamjenga na kumtengenezea tabia njema, badala yake wametengeneza kizazi kibovu cha watoto wasio na maadili.

Wamesahau biblia inasisitiza kuhusu kutomnyima mtoto fimbo, inaonyesha ni kiasi gani hawasomi biblia zao. Maana wangesoma biblia wangekutana na mstari huu wa biblia;

Rejea: Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa.Mithali 23:13 SUV.

Ninachokisema mimi hapa sio kile unaweza tumia ukali kumrejesha mtu kwenye mstari mzuri, ambapo huenda mwanzo ulitumia lugha ya upole hakukuelewa. Ninachozungumza mimi hapa ni ile kila mtu kukusema vibaya wewe, ni ile watu kulalamika kuhusu kauli zako mbaya.

Nimeona wengi hawataki kuonywa eneo hili, anaelezwa/unamweleza unavyoenenda ndugu sivyo mkristo anapaswa kuwa. Unamwambia hivyo badala ya kushuka chini ajitafakari, anainua mabega na kusema achana na mimi.

Unapaswa kujichunguza upya una nini, ingekuwa tabia uliyonayo ni njema watu wote wasingepiga kelele kuhusu wewe. Lazima kuna hitilafu sehemu, lazima kuna ufa sehemu, watu sio vichaa waanze kulalamika kupitiliza. Maana kwenye kwaya wanakulalamikia wewe, kwenye makundi mbalimbali wanakulalamikia wewe.

Labda uwe unalenga jambo fulani kufanya hivyo, unajua kabisa wataumia kwa muda ila baada ya muda fulani watafurahia matunda ya maumivu yao. Lakini kama ndio tabia yako ambayo haina matunda yeyote, na wala huna mpango wa kuibadilisha, nikueleze ukweli unasumbuliwa na uchanga wa kiroho.

Uchanga wa kiroho una viwango tofauti tofauti, unaweza kujiona upo vizuri sana kumbe kuna eneo haupo vizuri. Moja ya eneo hilo ni kukwazana na kila mtu yaani wewe kila anayekuja mbele yako lazima mkorofishane naye, kila mtu unamwona anakuwa kikwazo kwako, kila mara wewe ni mtu wa kuzirazira.

Kwanini nakwambia usome Neno la Mungu, Neno la Mungu linaleta hekima ndani yako, kadri unavyozidi kulijua Neno la Mungu. Ndivyo unavyozidi kutoka kwenye uchanga wa kiroho, uchanga wa kiroho huondolewi na maombi, uchanga wa kiroho unaondolewa na maarifa ya Neno la Mungu.

Kama una maombi ya kuondoa uchanga wa kiroho, nikuombe urudi kwenye kusoma Neno la Mungu, majibu ya maombi yako utakuwa umepata. Hunilipi pesa unaposoma Neno la Mungu, naomba uelewa hili usije ukasema napalilia sana suala la kusoma Neno la Mungu kwa sababu kuna pesa unatoa.

Kusoma Neno la Mungu ni kwa faida yako mwenyewe, ni aibu kuwa na vitabia vibaya ambavyo hata walioamini wanashindwa kukuelewa. Achana na wale wasioamini huenda wakashindwa kukuelewa sana, hata wenzako mlio na safari moja washindwe kukuelewa wewe tu? Hapana lazima kuna hitalafu kwako.

Hupaswi kuwa sehemu ya makwazo kwa wengine, angalia kauli zako zinajenga watu au zinawapoteza watu. Nimeshasema sio kila maneno yako yataeleweka kwa wachanga wa kiroho, ila dhamira yako ya ndani ikushuhudie unachofanya kina mwelekeo wa kuzalisha matunda mema.

Usije ukatumia mwavuli wa cheo cha mwinjilisti, kuwa sehemu ya mavurugano. Nimeona wengi wanatumia sana cheo cha mwinjilisti kuleta makwazo kwa wengine, mwinjilisti anapasua iliyo kweli ya Mungu pasipo uoga. Nia yake ikiwa watu waje kwa Yesu Kristo na sio watoke kwa Yesu Kristo, na wakishakuja ana uwezo wa kuwafanya kumpenda Mungu.

Ndugu yangu unapaswa kubadilika, kama umeokoka huna maelewano na kila mtu na wala hutaki kusikiliza ushauri wowote. Fahamu ya kwamba una shida, ndani yako unapaswa kuwa na unyenyekevu hata kama kutatokea mvurugano wa namna yeyote ile. Penda amani, penda kukaa na wenzako kwa utulivu, penda kuona furaha yenu mkiwa pamoja.

Mahusiano mazuri na watu hayaondoi kitu ameweka Mungu ndani yako, tena ukiwa na mahusiano mazuri na watu wanajua huyu sio mtu wa masihara, wanajua huyu sio mtu wa kuambiwa maneno ya ovyo. Lakini kama wewe mwenyewe ndio unakuwa sehemu ya maneno ya ovyo, ujue mwenye tatizo ni wewe mwenyewe.

Jua kuishi na rika lote, ukiwa na vijana wenzako endana nao kwa hekima na akili, ukiwa na wazee endana nao kwa hekima. Vivyo hivyo na mzee ukiwa na kijana jua namna ya kuendana naye, na ukiwa na mzee mwenzako jua namna ya kumwendea. Pasiwepo mang’uniko ya kupitiliza mpaka ikaonekana hata wenye makosa wakaonekana hawana.

Bila shaka umepata kitu cha kukusaidia kuboresha mwenendo wako, Neno la Mungu liwe chakula chako cha kiroho. Hakikisha unamwomba Mungu akusaidie katika hili.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

www.chapeotz.com

+255759808081.