Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali kingine cha kuiona leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, kwa neema hii anayoendelea kutupa.

Kama ni kutenga muda wako ni vyema ukafanya sasa kujiuliza ni kwanini ulianza vizuri jambo la kiMungu alafu ghafla ukaona halina maana tena kuendelea nalo. Kweli yapo mambo unaweza kujaribisha katika maisha yako, ukafika hatua ukaona ulichoanza kufanya haikuwa sehemu yako.

Yapo mambo pia unaweza kuanza nayo kwa namna ya udhaifu ila kadri unavyozidi kufanya Mungu anaweka vizuri mazingira na hilo jambo linakuwa la baraka kwako na kwa wengine. Udhaifu ninaousemea hapa ni ule wa kuanza jambo huku watu hawakuelewi kabisa, ila wewe ukawa unaelewana na Mungu wako maana ameweka mzigo ndani yako kulifanya.

Pamoja na kuchagua vitu vya kufanya, unapaswa kuelewa ukishakuwa mkristo vipo vitu sio vya kusikia msukumo ndani yako ndio uanze kufanya. Vipo vitu ambavyo kuvijua ni muhimu kwako kufanya, unapaswa kufanya kwa lazima hata kama huna upendo navyo wakati huo.

Wote tunajua hatupaswi kufanya mambo ya kiMungu kama desturi ila desturi hii tunaweza kuitumia kama bado hatuelewi baadhi ya vitu. Mpaka pale tutakapokutana na nguvu ya Roho Mtakatifu, ataweza kuondoa ule ukawaida ambao tuliona ukristo ni jambo la kawaida kawaida au mazoea.

Wengi sana wanaposikia kwa watumishi mbalimbali kusoma Neno la Mungu ni muhimu kwao, na wakiangalia wanaowaambia hivyo ni wale watumishi wanaowaamini wao. Wanajikuta wanahamasika sana na kukimbilia kusoma Neno la Mungu kwa kasi sana, ila haichukui wiki wanarudia kwenye hali zao za udhaifu.

Elewa suala sio kumwamini mtumishi fulani, hiyo ni sauti ya Mungu imepitia kwa mtumishi wake kusema nawe kuhusu umhimu wa kusoma Neno la Mungu. Sauti inaposikika masikioni mwako unasikia mtetemo ndani yako kuanza hatua za kusoma Neno la Mungu.

Usifikiri ni sauti ya mchungaji wako, usifikiri ni msisitizo wa mwalimu wako, Mungu anamtumia kiongozi wako wa kiroho kusema nawe, Mungu anamtumia huyo mtumishi unayependa kumfuatilia kupitisha msisitizo wa kusoma Neno la Mungu.

Unapojiona msukumo ndani yako kuchukua hatua, usifikiri ni utani, usifikiri ni mawazo yako mwenyewe ndio yanakusuma ndani yako. Hiyo ni sauti ya Roho Mtakatifu inakusuma kufanya hivyo, ndio maana usipotii unamhuzunisha Roho Mtakatifu. Wakati mwingine umejiona umekosa amani ni kwa sababu umeacha kusoma Neno la Mungu, wakati mwingine umeona furaha imerejea ghafla pale ulipoanza tena kusoma Neno la Mungu.

Shida inakuja kusoma Neno la Mungu kuna vita vyake vikali sana, hapa ndipo shida inapoanzia kwa wengi wetu. Kwanza kabisa tumekua tukiwa hatuwajawahi kuona hili jambo likiwekwa msisitizo tangu watoto wadogo, kingine tangu umeokoka huenda hujawahi kuona mkristo mwenzako analiweka hili jambo kipaumbele.

Ninachokuomba ujikalishe mwenyewe kikao ujihoji nini kimekufanya uanze kusoma Neno la Mungu alafu baada ya muda fulani ukaachana kabisa hiyo shughuli. Kama hujaachana na kusoma Neno la Mungu mbona ile furaha yako imetoweka ghafla, unasoma ilimradi siku ipite. Mbaya zaidi umeridhika na hali hiyo ya udhaifu, hujapata kabisa hamu ya kukemea huo udhaifu.

Utaniambia mtumishi nina mambo mengi sana ndio maana nashindwa kusoma Neno la Mungu, sio kweli una mambo mengi shida yako ipo kwenye utayari wako wa kufanya mambo ya kiMungu. Shetani amejua ukijua Neno la Mungu kuna vitu vingi sana hataweza kukuchomekea ukakukubaliana naye.

Utanimbia mtumishi shida sio kusoma Neno la Mungu, shida ipo kwenye kuelewa Neno la Mungu, sio kweli Mungu anashindwa kukupa ufahamu wa kulielewa Neno lake. Shida yako unamkataa kumkaribisha Roho Mtakatifu ndani yako, unamwona Roho Mtakatifu kama adui yako na wala hutaki kumsikia.

Unasikia ndani yako kuna huzuni kwa sababu umeacha kusoma Neno la Mungu, hakikisha unaanza upya kusoma Neno la Mungu. Unasikia kuchoka na huna hamu tena ya kuendelea kujifunza Neno la Mungu, hakikisha unamwambia Mungu arejeshe furaha ya wokovu wako. Usife na kamba shingoni, hakikisha unatafuta msaada haraka sana.

Ingia hata maombi ya kufunga kumweleza Mungu akusaidie utoke katika eneo la kutokusoma Neno lake. Pasipo Neno la Mungu utamtenda Mungu dhambi, pasipo Neno la Mungu hutojua haki zako za msingi, pasipo Neno la Mungu yapo mambo utahalalisha kumbe hukupaswa hata kugusa wala kuyapa kibali.

Naona machozi ya mtu mmoja yakitiririka baada ya kusoma ujumbe huu, hakika Mungu anakusudi jema na wewe. Mungu anakutaka uchukue hatua ya kusoma Neno lake, Mungu anakutaka utoke katika uchanga wa kiroho, kubali sasa kuchukua hatua.

Kile umejifunza hakikisha unachukua hatua, furaha yangu wewe kusoma Neno la Mungu, furaha yangu ni kukuona unaondoka kwenye uchanga wa kiroho. Sio lazima nikujue kama unasoma Neno la Mungu kama umepata nafasi ya kunijua kwa kusoma ujumbe huu, inatosha kabisa.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, kwa leo niishie hapa, endelea kutembelea mtandao wetu wa Chapeo Ya wokovu kupata masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.