Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, kwa neema ya Mungu ametupa kibali cha kuweza kuiona siku nyingine tena. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.

Tunapoanza jambo la kiMungu alafu ghafla tukaliacha kwa kufikiri labda kuna kitu tutakiepuka, badala yake huwa tunaambulia kuchoka kiroho zaidi tofauti na tulivyokuwa tunafanya hilo jambo.

Unaweza kufikiri unavyojitoa kwa mambo ya Mungu, kuna vitu vingi sana unavipoteza na ukafika wakati ukaona ili uanze kuvipata vile ulivyokuwa unavikosa. Unaona ni bora uachane na baadhi ya mambo ya kiMungu na uanze kutoa muda wako kuyafanya hayo unayoona ni muhimu sana kwako.

Unashangaa baada ya kuachana na mambo ya kiMungu kwa kuyaona yanakupotezea muda wako, unashangaa mambo yako yanazidi kuharibika zaidi ya mwanzo ulivyokuwa unatenga muda wako kwa ajili ya Mungu wako.

Unaweza kujifuatilia mwenyewe, jitazame pale unapoacha kukusanyika pamoja na wenzako kanisani kwa sababu ya kubanwa sana na shughuli. Angalia ile nafasi unayoanza kutengeneza baina yako na Mungu, unaanza kuona kabisa moyoni kuna mahali umeanza kupoa kiroho.

Ukiendelea kuwa hivyo na wewe ukaacha kufanya bidii yeyote, kuna hatari kubwa baada ya muda fulani utaanza kuona hata kwenda kanisani ni jambo la kupoteza muda wako. Badala yake utaanza kuona bora kukaa kwenye TV yako kuangalia mahubiri yanayoendelea sehemu zingine wakati huo wenzako wameenda ibada ya pamoja na wewe wakati huo huna sababu ya kukufanya usiende.

Unaendelea na tabia yako hiyo ya kutokwenda kanisani, unakuja kujiona hata ule muda uliokuwa unauona unaupoteza. Unakuwa unapotezewa muda wako na mambo mengine zaidi ambayo yanakuwa mwiba kwako, na wakati huo unakuwa unahitaji msaada kutoka kwa Mungu wako.

Bahati mbaya unaweza kuhitaji msaada ukiwa tayari umejiingiza kwenye eneo baya ambalo ungekuwa umetulia na Mungu wako na kumpa nafasi ndani ya moyo wako. Usingeweza kujiingiza katika majuto unayojutia sasa, badala ya kuvuna mazuri uliyokuwa unayafikiri mwanzo unavuna machungu/mateso.

Chukulia umeacha kusoma Neno la Mungu, ulichokipata haswa ni kipi kama sio hasara. Maana tangu ukae na kuendelea na ubize wako, kipi unajivunia kwenye ubize wako, kama ni uchanga wa kiroho bado unao wa kutosha, kama ni kudanganywa bado unadanganywa, kama ni kuamini kila mtu hata anayepotosha jina la Yesu Kristo bado unayo hiyo tabia.

Kipi umekipata zaidi ya hasara, ndio umeambulia hasara kwa sababu hakuna cha msaada ulichokipata zaidi umeendelea kubaki kwenye mahangaiko ya uchanga wa kiroho. Wakati huo wenzako wanaendelea kufurahia ukristo wao hata kama wanapitia changamoto ngumu, wanaona ni heri kukaa na Yesu wao kuliko kutangatanga na mambo ya Dunia.

Kuliko kuendelea kuvuna mapooza, rudi kwenye Neno la Mungu, rudisha utaratibu wako wa kusoma Neno la Mungu. Kama ulikuwa unasoma na huoni matokeo yeyote ya kusoma Neno la Mungu, kaa chini ujihoji kuna jambo gani linalokuzuia wewe usiweze kudaka vitu vilivyomo ndani ya Neno la Mungu.

Neno la Mungu sio la kupuuzwa, weka mpango mkakati wa kusoma bila kuachia njiani, iwe masika, iwe kiangazi, hakikisha Neno la Mungu linakuwa kipaumbele chako. Amini chakula pekee cha kiroho ni Neno la Mungu, ndilo linatufanya tuweze kuhimili mambo mbalimbali hasa yanayogusa imani yetu ya ukristo.

Narudia tena hutopoteza muda wako kama utaamua kweli kutenga muda maalum wa kusoma Neno la Mungu, hakuna siku utajiona ulifanya kazi ya bure. Badala yake utajipongeza kwa kuchukua maamzi sahihi ya kukuondoa kwenye ujinga wa kiroho na kukufanya kuwa mkristo anayejitambua.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi. Hujajiunga group la whatsApp la kusoma Neno la Mungu na unahitaji kujiunga nasi, karibu tuwasiliane kwa namba hizo chini.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.