Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Karibu sana tushirikishane mambo muhimu ya kukusaidia katika safari yako ya wokovu.
Uhamasishaji ni mzuri sana, tena una manufaa kwa jamii zetu na wale wanaotuzunguka. Kama kuna jambo walikuwa wanalichukulia kawaida, kupitia uhamasishaji wanaanza kukichukulia kwa uzito mkubwa.
Nina uhakika umeanza kulipenda Neno la Mungu kupitia mafundisho mbalimbali ya kukuhamasisha na kukueleza umhimu wa kusoma Neno la Mungu. Na kama unasoma ujumbe huu kwa mara ya kwanza na huwa huna tabia ya kusoma Neno la Mungu, naamini mpaka kufikia mwisho wa somo hili utakuwa umepata kitu.
Kumekuwa na tabia moja hivi ya ajabu sana, hasa kwa wakristo walio wengi wanahamasisha watu kuishi maisha matakatifu alafu wao wanaishi maisha ya ovyo. Kweli unaweza kufanikiwa kumsaidia mtu akatoka kwenye utumwa wa dhambi ila usiporekebisha na kutubu makosa yako, hakuna mbingu ya ofa.
Wazazi wengine wamekuwa wakiwahimiza watoto wao kuishi maisha ya kumcha Mungu lakini wao wanaishi maisha yasiyo mpendeza Mungu. Watoto wao wanapowatazama wazazi wao wanaona mbona mama ananikataza kuvaa nguo za aibu ila yeye anavaa, mbona baba ananikataza kuanza kutembea na mwanamke kabla ya ndoa ila yeye ana tembea ovyo na wanawake kwa uzinzi.
Anapokuja kujua mzazi wake anachomsisitiza yeye afanye au asifanye kutokana na ubaya wake alafu mzazi akawa anafanya. Na wakati anafanya sio kwamba kwake ni sahihi sana, mtoto naye anaona kumbe na mimi nikifanya haina ubaya.
Chunguza vizuri wazazi wenye nyumba ndogo, huwa anatokea mtoto mwenye tabia ile ile, hata kama mzazi alifanya kwa siri. Tabia yeyote njema unayotaka mwanao aishi, unapaswa wewe kuwa mfano namba moja.
Unapomwambia mtoto uwe na tabia ya kusoma Neno la Mungu, akuone wewe unafanya hilo jambo. Unapomwambia mtoto uwe msafi, akuone wewe unapenda usafi na ni msafi kweli.
Sio vyote unaweza kuvihamisha alafu ukawa na uwezo wa kuvifanya, hiyo inaeleweka. Mfano mzazi anahamasisha watoto wake wasome, wakati yeye hajamaliza hata darasa la pili, hilo haliwezi kuwa tatizo kwa mtoto.
Tunachosema hapa ni ile tabia ya kuhamasisha watu vitu alafu wewe mwenyewe huwa hushiriki kabisa. Na wakati nafasi ya kushiriki hayo unayohamasisha unayo, mfano unahamasisha watu waombe alafu wewe huombi kabisa.
Tusiende mbali sana nijitolee mfano mimi mwenyewe, mimi hapa niwe nawahamasisha kusoma Neno la Mungu kila siku. Ila mimi mwenyewe nikawa sisomi, hata wewe mwenyewe kama ulianza kusoma ukaja kugundua kuwa aliyekuhamisha yeye mwenyewe hasomi, ni ngumu sana kuendelea kusoma.
Labda uwe umefika hatua fulani za juu sana kiroho, vinginevyo utaacha kufanya kile uliambiwa ni muhimu kwako. Hata katika vita, yupo kiongozi anayeongoza mapigano, yeye huwa mstari wa mbele kuhakikisha mambo yanaenda sawa.
Tabia hii ya kuhamasisha watu wafanye vitu fulani alafu wewe hufanyi, lazima tukae tujiulize kwanini unatuhamasisha vitu ambavyo wewe haupo tayari kuvifanya. Kama unaona ni vizuri kufanya shida ni nini kwako inayokupelekea usifanye, tueleze kinachokuzuia kufanya huenda ukatusaidia wote tuliohamasika tusirudi nyuma.
Nimeshasema kuna vitu Mungu anaweza kumtumia mtumishi wake kuvisema ila huyo mtumishi asiwe navyo. Mfano mtumishi anaweza kuwa na nguvu za Mungu kuwekea wagonjwa mikono wakapona, alafu kwake kukawepo mgonjwa wa miaka mingi anaumwa.
Hilo linaweza kueleweka kwa sababu ambazo tunaweza kuziangalia pande zote mbili, huenda mhusika anayeumwa hana hana imani ya Yesu Kristo. Anakuwa na imani yake ambayo hataki kumruhusu Yesu aingie ndani yake au wakati wa Mungu ukawa hujafika huyo mgonjwa kupokea uponyaji wake.
Ila tabia ya kuwaambia watu wafanye jambo fulani ni zuri alafu wewe mwenyewe unalipita mbali, tunakuwa na mashaka na yale unatueleza. Labda mfano mzuri tunaweza kusema Musa angetokea mtu mmoja akamwambia Musa tunaomba wewe uanze kuvuka bahari ndipo na sisi tufuate. Huyo mtu angekuwa sahihi kama asingekuwa anajua Musa alivyokuwa kiongozi wao na Mungu alikuwa anamtumia yeye kusema na wao.
Tumesoma habari za wana wa Israel wakati wanatoka nchi ya Misri, walisita kidogo ila walipoona bahari imeachia walisonga mbele upesi. Maana waliona maadui zao nyuma, unaweza kufikiri pia huenda wasingekuwa wale maadui nyuma yao wasingevuka haraka hiyo bahari. Huenda wangeanza kujadili inawezekana vipi bahari kugawanyika na watu wakapita, kweli wanaweza hawakuwahi kushuhudia tukio la namna hiyo.
Bila kukuficha wala bila kukupita pembeni, ni tabia mbaya sana kuhamishisha watu kitu ambacho wewe mwenyewe ulipaswa kuhusika. Ukaacha kuhusika kwa makusudi tu na ulikuwa na uwezo wa kushiriki, maana tunaona Musa baada ya kuona wote wamepita naye alimalizia mwisho na bahari ilikuja kuwameza maadui zao.
Unapomwambia mtu soma Neno la Mungu, hakikisha na wewe unasoma Neno la Mungu. Tena kuwa zaidi yake kwa kuweka bidii zaidi, aone kweli kusoma Neno la Mungu ni muhimu sana kwake.
Mpaka hapo kuna kitu umejifunza kupitia ujumbe huu, hakikisha unautafakari na kuelewa zaidi. Sijakuandikia yote ila nimekupa njia ya kuongeza mengine zaidi ambayo unaona Roho Mtakatifu amekugusa moyoni mwako baada ya kusoma ujumbe huu.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
www.chapeotz.com
+255759808081.