Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, tusipomshukuru Mungu kwa nafasi aliyotupa siku ya leo. Tutakuwa wanafiki maana kuiona siku ya leo ni muujiza tosha kwa kila mmoja wetu, kufikia siku ya leo inakupa nafasi ya kufanya mambo mengi sana.
Shida ya uchanga wa kiroho unabeba maeneo mengi sana ya mkristo, ambapo unamkuta mpendwa alianza vizuri na moto wa kuokoka. Baada ya kukutana na changamoto fulani katika mazingira ya mwili, akaona ni heri kuuacha wokovu na kufanya kile kinachomchukiza Mungu wake.
Sababu haswa ya kumfanya mtu achukie wokovu, na kumwona Mungu amechelewa kumjibu yale aliyomwomba miaka mingi. Anachofanya ni kupita njia ya mkato ambayo haina utukufu kwa Mungu wake, na unajua jambo lolote likikosa utukufu kwa Mungu ujue linakutenganisha na Mungu wako.
Sababu ni uchanga wa kiroho, na uchanga wenyewe wa kiroho ni kukosa Neno la Mungu ndani mwa mtu. Neno la Mungu likikosekana kwa mkristo yeyote yule, imani ya mkristo yule lazima itakuwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi. Atakuwa mwombaji mzuri sawa, tena mwenye kufanya maombi ya kufunga sana, ila itafika wakati ataona mbona sijibiwi.
Atakapoona hajibiwi kwa kile anaomba, akaja shetani akapitisha wazo lake potofu na akapiga hesabu kweli alivyokaa katika maombi haoni jibu lolote. Ni rahisi sana kwa mkristo yule kukatisha njia sahihi, na kufuata njia isiyo sahihi kwa imani yake kama mkristo.
Unaweza kusema sio kweli ninayosema hapa, hebu nikukumbushe tu hujawahi kusikia au kuona mkristo ameenda kwa waganga wa kienyeji baada ya kuuguliwa sana na mtoto/ndugu yake yeyote yule au yeye mwenyewe kuugua. Kama hujawahi kuona utakuwa umewahi kusikia, hapo ujue walijaribu kwenda kwa watumishi kuombewa walivyoona hawaponi akatokea mtu akawambia nenda kwa bibi/babu/mama fulani atakupa dawa utapona.
Neno la Mungu lina kazi kubwa sana kwa mkristo yeyote yule, unaweza usijue sana kazi yake wakati una amani. Ila kadri siku zinavyozidi kwenda na ukawa na ratiba ya kuendelea kulijaza zaidi Neno la Mungu moyoni mwako, utafika kipindi huwezi hata kusoma Neno la Mungu wala huwezi kuomba. Ile akiba/hazina yako uliyojiwekea ya Neno la Mungu ndio itakubeba wakati huo, ndio maana unakutana na mtu anapitia kwenye moto mkali wa majaribu mazito ila bado anampenda Yesu Kristo.
UsifikirI ni jambo la kawaida, wapo wanampenda Yesu mdomoni ila moyoni tayari wameshamwasi siku nyingi sana. Ingekuwa hawajamwasi Mungu matendo yao yasingemkataa Mungu, matendo yao yasingewafanya wanyoshewe vidole na watu wa mataifa.
Utasema haiwezekani, wanaume wangapi wamebeba wake kienyeji bila kufunga nao ndoa na walikuwa wameokoka na walikuwa waombaji wazuri tu. Wanawake wangapi wamebebeshwa mimba wakaachwa hapo na wengine wamechukuliwa kienyeji bila ndoa, sio kwamba walikuwa hawajamkiri Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wao, walishamkiri na wengine walikuwa wanafanya huduma kabisa.
Sikuelezi haya kukuumiza au kukujeruhi moyo wako, sikuelezi haya uanze kukumbuka ya kale na kujiona hufai mbele za Mungu. Nakueleza haya kujua makosa mengi tunayafanya kwa sababu ya uchanga wa kiroho, ujinga mwingi unaofanyika makanisani ni kwa sababu idadi kubwa ya wakristo wengi hawataki kujishughulisha na mambo ya kuwakuza kiroho.
Wengi walivyookoka waliona imetosha, kumbe kuokoka ilikuwa ni hatua ya kujitofautisha mwana wa giza na nuru, baada ya hapo alipaswa kutafuta vitu vya kukuza kiroho chake. Ili asije karudi tena nyuma baada ya kukutana na changamoto ndani ya wokovu.
Mungu amekupa fursa kubwa sana ya kujua haya,hakikisha unakuwa mstari wa mbele kusoma Neno la Mungu. Moja ya maombi ya kujinyima chakula Mungu akusaidie jambo unalomwomba akufanyie, ni pamoja na hili la kuelewa Neno la Mungu unapolisoma. Hakuna Sababu unaweza kutoa kujitetea usisome Neno la Mungu ikiwa tu umeweza kusoma ujumbe huu.
Uwe kiziwi unaweza kusoma Neno la Mungu ukaelewa, uwe kipofu wa macho unaweza kusoma biblia maalum zilizotengenezwa kwa ajili ya vipofu. Ukiona hiyo inakupa shida unaweza kutumia App yenye biblia ya sauti(audio).
Bila shaka umejua sababu haswa inayoturudisha nyuma tulio wengi, tafuta kukua kiroho, unapotembea waza namna ya kuondoka kwenye utumwa wa uchanga wa kiroho. Hutojuta maisha yako yote, kama ulikosea nyuma sema imetosha Baba, naja mbele zako kwa upya ili nikutumikie na kukutumaini wewe maisha yangu yote.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.