Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona. Fursa kwetu kwenda kumzalia Bwana matunda yaliyo mema, na fursa kwetu kurekebisha na kutubu makosa tuliyofanya jana na siku za nyuma.

Kuna vitabia fulani fulani unaweza kuwa navyo ukafikiri ni sahihi kuwa navyo, hivyo vitabia vikaendelea kukutafuna siku hadi siku ukijipa matumaini kuwa ulivyo haina shida. Tabia hiyo unayoona ni nzuri kwako inaweza kuwa kikwazo kwako na kwa Mungu kushindwa kukufikisha kwenye majibu ya maombi yako. Maana kila mara unatengeneza ukuta wa hasira ndani yako kwa vitu visivyo na maana kuvishikilia kifuani mwako.

Kitu kidogo unakasirika siku nzima, jambo dogo unalibeba kiasi kwamba linakufanya unashindwa hata kuomba Mungu. Wengine walikosewa jambo siku nyingi mpaka leo wameshikilia kosa walilotendewa na hawapo tayari kuachilia hilo.

Mwingine ana kitabia ambacho kimekuwa kama amezaliwa nacho, kumbe amekitengeneza tu mwenyewe baada ya kujifunza hiyo tabia. Bahati mbaya sana mzazi alimchelewa kumkanya kuhusu hiyo tabia, ama aliichukua moja kwa moja kutoka kwa wazazi wake.

Baba akimkosea mama, mama atanuna siku nzima na wakati anaweza kumaliza hata wiki bado amenuna. Mpaka pale baba atakapotekeleza kile mama anataka ndipo furaha ya nyumba irudi.Sasa mtoto kile mama anafanya anakichukua na kukibeba akijua ni mbinu nzuri ya kuombea vitu, shida nyingine kubwa yule mtoto anaboresha zaidi ile tabia kwa kuzirazira kila jambo.

Tabia ya kuzirazira imesababisha watu wengi wameacha huduma zao nzuri, tabia ya kuzirazira imesababisha wengi wameacha kwenda kanisani, tabia ya kuzirazira imesababisha wengi wameacha wokovu, tabia ya kuzirazira imeshababisha wachumba kuwakimbia wenzao kutokana na kushindwa kuendana na tabia zao mbaya za kuzirazira ovyo.

Zipo tabia nyingi sana zinazoletwa na kuzirazira, wengine wamezitenga familia zao kwa kusitisha kuwapa hata msaada wa kifedha. Kwa sababu kuna jambo fulani baya waliwahi kutendewa huko nyuma, wanaona njia nzuri ni kutowasaidia kwa chochote.

Huenda nimekuacha njia panda kwa hili, ngoja nikutolee mfano huu utanielewa zaidi. Umewahi kuona au imewahi kukutokea wewe mwenyewe ukiwa mikononi mwa wazazi/walezi wako, ukifanya kosa wanakuchapa baada ya kuchapwa unazira na kula kabisa. Inabidi watu waanze kufanya zoezi lingine la kukubembeleza ule au unanyimwa Ada ya shule/chuo unazira na kula kabisa mpaka wakupatie hizo pesa.

Hizo njia zinaweza kuwa njia sahihi kama unaona unaonewa na kuacha kula ni kuwajulisha wazazi mnachonifanyia sikustahili kufanyiwa. Lakini kama kila ukifanyiwa jambo wewe ni kukasirika ovyo na kuzira kushirikiana na wenzako au unajizira wewe mwenyewe kwa kutamani ufe kabisa. Ukiangalia sababu haswa ya kuomba kifo unakuta ni kitu kidogo sana ambacho hata mtoto mdogo aliyefunzwa tabia njema akikusikia anakuona huyu ana shida.

Yote najaribu kukueleza ili uweze kujua zaidi, lakini yote hii inaletwa na uchanga wa kiroho. Asilimia kubwa ya watu wanaozirazira sana, ni watu ambao hajakomaa kiroho, kubali ukatae huo ndio ukweli wenyewe. We jaribu kujichunguza mwenyewe utaelewa zaidi ninachokueleza hapa, pia unaweza kuangalia wale wote wenye tabia hii utaona tatizo lao ni hili hili la uchanga wa kiroho.

Mtu aliyekomaa kiroho hawezi kuzira siku nzima amenuna, wala hawezi kufanya vitu kwa hasirahasira. Hata kama utamkwaza sana, hasira zake hazitachukua saa moja au siku nzima, utaona ameachilia moyoni mwake na kuendelea na mambo yake mengine.

Unakutana na mwimbaji wa kwaya amekwazwa kidogo, anachana na kwaya kabisa, bila shaka huyo hakuwa na huduma hiyo ndani yake. Na kama anayo basi anasumbuliwa na uchanga wa kiroho, si umewahi kuona makanisani wapiga vyombo wanavyosumbua wa kuzirazira ovyo mpaka mkawabembeleze weee….ndio warudi kufanya kazi yao.

Ondokana na hii anza ya kuwa mtu uliyejaa hasira bila hata sababu ya msingi, hili linaondolewa na kujaza maarifa ya Neno la Mungu. Soma biblia yako kila siku, sura moja tu inakutosha kabisa kwa siku ukapata muda wa kutafakari uliyojifunza.

Kama unaipenda tabia hiyo mbaya uliyonayo basi endelea kutokusoma Neno la Mungu, ila kama huipendi hiyo tabia pamoja na kuomba sana Mungu umejikuta upo vilevile. Suluhisho ni kulijaza Neno la Mungu kwa wingi moyoni mwako, utaona ujinga mwingi unafutika ndani yako.

Jipe nafasi kutafakari zaidi haya uliyojifunza, ujue wapi pa kurekebisha na wapi pa kuongeza bidii. Usifanye haraka, tulia kabisa ili utakapofanya maamzi uwe kwenye akili zako timamu.

Rafiki yako awe biblia, kila uendako usikubali kumwacha.

Mungu akubariki sana kwa muda wako uliotoa kusoma ujumbe huu.

Fb: Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.