Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, ametupa nafasi nyingine ya kwenda kumzalia matunda yaliyo mema.
Wapo watu wanafurahia sana mafundisho ya Neno la Mungu hasa pale wanapopitishwa kwenye vitabu mbalimbali vya biblia walivyowahi kuvisoma wenyewe. Mtu wa namna hii anapokutana na mafundisho ya habari aliyowahi kuisoma mwenyewe, inaleta hamu ya kusikiliza zaidi.
Tofauti kabisa na yule ambaye hajawahi kusoma biblia alafu akawa anasikia yale mafundisho kwa mara ya kwanza, inaweza ikamfunza jambo na akaondoka na kitu kikubwa sana. Ila haiwezi kumfikia huyu aliyewahi kusoma Neno la Mungu alafu akakutana na mafundisho yanampitisha humo humo alipopita yeye.
Kwanza kabisa kama umewahi kusoma kitabu fulani cha biblia, inakuongezea uelewa zaidi pale unapomsikiliza mwalimu anakupitisha humo humo. Inaleta usikivu ndani yako, na inaleta hamu kubwa ndani yako, na inaleta kutiwa moyo mahali ambapo ulitaka kuchoka na kuacha mpango wako wa kusoma Neno la Mungu.
Pamoja na mazuri hayo, inaweza kukusaidia pia kujua anayekufundisha anakufundisha sahihi au anakupotosha. Sasa hapa kuna faida na hasara zake, kama umewahi kusoma vizuri habari fulani ndani ya biblia alafu akatokea mwalimu akapindisha ile habari. Inaweza kukuondoa kwenye uamini mkubwa juu ya yule mwalimu anayekufundisha, pia inaweza kukusaidia kujua mwalimu anayekufundisha sio mwalimu mzuri.
Unapofikia kiwango hicho cha kujua unacholishwa kipo sahihi, sio sahihi tu kwa sababu unajua mahali unaposikiliza mafundisho hayo huwa wanaisema kweli ya Mungu. Utakuwa unajua kinachosemwa ni sahihi kwa sababu umesoma mwenyewe biblia na kinachosemwa ndivyo ulivyosoma.
Furaha yako huzidi zaidi unapofikia hatua ya kusoma Neno la Mungu alafu ukiwa kanisani mchungaji anapita humohumo uliposoma mwenyewe. Tena inakupa msukumo zaidi wa kuongeza umakini wa kusoma Neno la Mungu tofauti na yule asiyejishughulisha na jambo hili, atabaki kusema leo mchungaji alihubiri vizuri kweli au wakati mwingine anatoka mtupu.
Labda ukasikia habari za mwanamke tasa ambaye alipata neema kuzaa mtoto, alafu ukapitishwa kwa Elisabeth mke waka na Zakari ambaye alimzaa Yohana mbatizaji. Ambaye Yohana huyu waliachana kidogo katika kuzaliwa kwao, yaani Yohana alitangulia kuzaliwa akaja kufuata Yesu Kristo.
Nimetoa hiyo habari ya mwanamke tasa aliyekuja kuzaa mtumishi wa Mungu, tayari wapo watu wanaoijua hii habari wamefurahi sana ndani ya mioyo yao. Lakini huenda wewe ambaye hujawahi kusoma mkasa huu, unaweza kushangaa inawezekana vipi mwanamke tasa kupata mtoto, tena sio tasa tu alikuwa mzee.
Kusoma Neno la Mungu wakati mwingine inakuletea furaha ambazo hukupanga wewe kuzipata, lakini zinakuja tu zenyewe. Kwanini usiwe miongoni mwa watu wanaipata hii raha ya kweli, utaendelea mpaka lini kuona wenzako wakitikisa vichwa kumaanisha kinachosemwa mbele yao, kipo sahihi.
Unajisikiaje unapoona fundisho fulani lipo sahihi alafu akaja mtu anayesoma biblia akakuambia hichi kinachosemwa hapa sio cha kweli, ni upotoshwaji wa Neno la Mungu. Bila shaka moyoni mwako utajisikia vibaya mno maana ulikuwa na uwezo wa kujua kinachosemwa sio sahihi hata kabla ya huyo kuja kukuambia huu ni uongo.
Zipo faida nyingi sana unapokuwa msomaji wa Neno la Mungu, nimekumegea kipande hichi kidogo kwa namna hii. Ili uweze kuona ni jinsi gani kuna vitu unaweza kuvipata vikakupa furaha ya maisha yako ya wokovu.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa Chapeo Ya Wokovu.
Fb: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081