Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, anayeendelea kutupa kibali cha kuweza kumzalia matunda na kurekebisha pale tulipopoteza uhusiano wetu na yeye.
Rahisi sana kusema leo ngoja nijipe mapumziko mafupi ya kutokusoma Neno la Mungu, kweli ukaamua Kujipa hayo mapumziko. Ulikuwa upumzike wiki moja, unashangaa unaenda mpaka ya pili, ukiwa bado unashangaa unamaliza mwezi mzima ukiwa hufanyi zoezi ulilojipangia kulifanya.
Wote tunajua hakuna njia ya kuelekea kwenye mafanikio isiyo kuwa na changamoto, hata hili la kusoma biblia lina changamoto zake ngumu tu. Ukishalijua hilo unapaswa kupambana kwa kila namna kuhakikisha huondoki kwenye safari uliyoanza nayo.
Shida ya wengi tunajipa mapumziko hata kwenye maeneo yasiyopaswa Kujipa likizo. Mtu anakwambia nimesafiri nipo mbali na network sitoweza kusoma Neno la Mungu, kwa sababu tu huwa tunasoma kwa pamoja kwenye group la whatsApp. Anaona akiwa hayupo pamoja na wenzake hatoweza kusoma mpaka arudi kwenye network, anaporudi kwenye mazingira ya mtandao. Tayari ile hamu ya kuendelea kusoma Neno la Mungu haipo tena, shida nini, alijipa mapumziko.
Ukifikiri kwa kawaida network haiwezi kumzuia yeye kubeba biblia yake, network haiwezi kumzuia kushindwa kusoma biblia yake. Haijalishi alipo hakuna umeme, upo mwanga wa jua anaweza kutenga nusu saa ya kusoma na kutafakari maandiko Matakatifu.
Mwingine anakuambia kwa sasa nipo kwenye kipindi cha mitihani sitoweza kusoma Neno la Mungu, hivi ukisoma Neno la Mungu unaharibu kumbukumbu zote za kile umesoma au ukisoma biblia kwa nusu saa hutofaulu mitihani yako. Kwanini nasema hivi, wengi sana waliokuwa na bidii ya kusoma Neno la Mungu walipoteza mwelekeo pale walipojipa mapumziko ya kusubiri wafanye mitihani kwanza ya chuo.
Unapaswa ujiwekee kanuni zako kutokana na mazingira uliyopo, mazingira yangu yanaweza yasifanane na ya kwako. Shughuli zangu na zako zinaweza zisifanane na za kwako, sasa unapaswa kujua muda wako upi unakuwa na nafasi ya kufanya mambo yako. Huo muda unaokuwa na nafasi utumie kusoma biblia yako, usijipe mapumziko kwa sababu jioni hutokuwa na muda, hiyo asubuhi unayokuwa na muda itumie.
Narudia tena usijipe mapumziko yasiyo na lazima, bado ni mchanga mno kwenye eneo la kusoma Neno la Mungu. Bado unahitaji kujipa mazoezi zaidi ya kukusaidia kukua katika usomaji wako wa Neno la Mungu, unapojipa mapumziko unapoa na ukishapoa ni mwanzo wa kupoteana kabisa.
Uwe umechoka sana tenga dakika 10 au 20 tu za kusoma Neno la Mungu, uwe umebanwa sana na shughuli zako, tenga dakika chache za kupitia Neno la Mungu. Ukishasoma unaweza kuendelea na shughuli zako huku ukiendelea kutafakari yale uliyojifunza.
Hakuna muda mwingine sahihi sana kama unavyofikiria, muda ni huu huu na kila siku kinazaliwa kitu kingine. Ndio maana wengi wamejipa na msemo, kila kukicha afadhali ya jana. Wewe usiwe hivyo, unao muda wa kutosha na unayo kila sababu ya kutojipa mapumziko.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, usiache kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu kupata masomo mengine mazuri zaidi.
Nakutakia siku njema.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
www.chapeotz.com
+255759808081