Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Karibu tujifunze kwa pamoja yale yanayoweza kutusaidia katika usomaji wetu wa biblia.
Marafiki ni watu wazuri sana, pia wanaweza kuwa tatizo kwako usipokuwa makini, hasa kwa mtu anayeanza wokovu yaani akiwa bado mchanga kiroho. Asilimia kubwa wakiambatana na marafiki wasio na bidii kwa mambo ya Mungu, na wao wanakuwa wazembe kwa mambo ya Mungu.
Bila wao kujua wanajikuta wanabebeshwa uzembe wote wa rafiki zao, wanakuwa wanasikia jambo fulani ni muhimu sana kwa mkristo kulifanya. Lakini rafiki yake anakuwa kikwazo kwa kumkatisha tamaa za maneno ama kwa kumwona rafiki yake hajishughulishi na hilo jambo aliloambiwa ni muhimu.
Wapo marafiki waliotushawishi tuachane na mambo ya dunia, badala yake tufuatane na mambo ya Mungu. Wale waliotushawishi tuokoke, mara nyingi huwa marafiki zetu, huwa kama makocha wetu au kwa kiswahili kingine tunaweza kusema ni walezi wetu wa kiroho au wengine huwaita mama/baba zao wa kiroho.
Hawa watu wana mchango mkubwa sana kuturudisha nyuma au kutupeleka mbele zaidi. Kama watakuwa wavivu/wazembe kwa mambo ya Mungu, bila kusukumwa na mtu yeyote tunajikuta tumekopi tabia zao kama zilivyo. Kama ni wazembe kwa mambo ya Mungu na sisi tunakuwa vivyo hivyo, kama ni wenye bidii kwa mambo ya Mungu na sisi tunakuwa vivyo hivyo.
Kusoma Neno la Mungu sio kana kwamba wengi wanashindwa, wale waliowaambia habari hii ya kusoma Neno la Mungu wao wenyewe hawana mpango kabisa kuhusu hili jambo. Unakuta aliyemhamasisha kusoma Neno la Mungu, yeye mwenyewe yupo bize tu na mambo yake wala hana mpango wa kujifunza Neno la Mungu.
Kwa kuwa huyu aliyehamasishwa alikuwa mzembe siku za nyuma, akiona aliyemhamasisha yeye mwenyewe hana muda wa kusoma Neno la Mungu. Anaona kumbe sio jambo la muhimu sana, kama anayeniambia la muhimu yeye mwenyewe halifanyi bora na mimi niachane nalo.
Chunguza vizuri, mara nyingi sana walioanza wokovu huwa wana watu wao wa kuwafuatilia kujifunza kwao. Ikitokea bahati mbaya wakajifunza kwa mtu ambaye baadaye anakuja kumwasi Mungu, mara chache sana utawakuta wale waliokuwa wakijifunza kwake wakiendelea na wokovu. Wengi hurudi nyuma na kuachana na wokovu.
Nataka kusema nini, ukiwa mchanga kiroho alafu ukazungukwa na kundi kubwa la marafiki wasio na hofu ya Mungu. Uwe na uhakika utakuwa kama wao, usipokuwa kama wao unaweza kuwa zaidi yao, hata ile nidhamu ndogo mbele za Mungu uliyokuwa nayo unajikuta imetoweka kabisa ndani yako.
Hapo ulipo kama ni kwa uzembe au kwa bidii, uwe na uhakika marafiki wamechangia kiasi kikubwa sana sana kwako. Uwezekano upo umebaki mkristo jina ila moyoni mwako unajua kabisa unamtenda Mungu dhambi kwa siri. Hiyo dhambi unayoitenda kwa siri, na huna mpango wa kuitubia, ndio inayokutafuna na kukukosesha hamu ya mambo ya Mungu maana imeondoa ujasiri wako uliokuwa nao.
Pamoja na hatupaswi kuwatenga ndugu zetu na marafiki zetu wanaotuzunguka, ni muhimu sana kuwa na watu wazuri tunaojifunza mambo mazuri kwao. Pia uwe na uwezo wa kuchambua mambo ya kujifunza, ukiona wameanza kutoka kwenye kile ulichokuwa unakiona ndani yao, ni heri kusitisha mpango wako wa kujifunza kwao na kuwafanya kuwa marafiki wa kawaida.
Roho Mtakatifu ndio awe mwalimu wako, usiendelee kuchota uzembe kwa ndugu/rafiki yako. Yeye alifanya kazi yake, mshukuru kwa kutumika kuwa daraja la kuujua wokovu, mshukuru kwa kutumika daraja la kujua umhimu wa kusoma Neno la Mungu. Baada ya hapo achana na mengine, elewa yeye hana mbingu, mwenye mbingu ni Mungu.
Unajijua mwenyewe upo vipi kwenye kusoma Neno la Mungu, unaweza kuwa ulianza vizuri sana ukiwa na bidii ya kusoma Neno la Mungu ila umemezeshwa ghafla vitu vibaya na marafiki/ndugu zako. Rudi upesi kwenye kusoma Neno la Mungu, Neno la Mungu halijawahi kumwacha mtu katika uchanga wa kiroho.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutafakari zaidi kuhusu haya nimekueleza. Pia usiache kutembelea mtandao wetu wa chapeotz.comkwa masomo mengine mazuri zaidi.
Fb: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.