Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, mimi na wewe tumepata kibali cha kuiona siku ya leo. Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kutuamsha salama, haitoshi tu kumshukuru tunapaswa kwenda kumzalia matunda yaliyo mema.
Kuna vitu vinatokea kwa kuviruhusu wenyewe vitokee, lakini tungesimama katika nafasi zetu tungeweza kuvizuia kabisa visitokee. Vitu hivyo vimejikuta vinajiingiza kwenye maisha yetu na kuviona kama vyenyewe vinapaswa kushika nafasi kubwa kuliko vingine.
Kila kitu kisichomkosea Mungu wetu, kina maana kwa mwanadamu, kila shughuli iliyo halali mbele za Mungu inapaswa kupewa muda wa kutosha kuifanya kwa bidii ili uweze kuona mafanikio kwa unachofanya.
Unapoacha kuyapa kipaumbele mambo mengine ya kimwili kwa kufikiri yanayopaswa kupewa kipaumbele ni mambo ya kiroho. Utakuwa unakosea sana, unahitaji ule chakula cha tumbo, utapaswa kufanya kazi ili uweze kupata chakula. Unahitaji kuvaa nguo nzuri, utahitaji kufanya kazi ili upate pesa ya kununua hizo nguo, unahitaji kuishi kwenye nyumba nzuri yenye mazingira mazuri, utapaswa kufanya kazi kwa bidii ili uweze kuwa na hiyo nyumba.
Tunahitaji kumjengea Mungu nyumba nzuri ya kukusanyika pamoja kwa ibada, tutahitaji kufanya kazi za mikono kwa bidii ili tuweze kumjengea Mungu nyumba nzuri ya kupendeza. Mungu ameshatupa kumiliki vyote viliopo chini ya mbingu, kazi yetu ni kufanya kazi kwa bidii ili tuweze kuvipata vile alivyotuahidia kutupa.
Vipo vitu vinavyoonekana ni vidogo sana katika maisha yetu na wakati mwingine vinaweza kuonekana sio muhimu sana kwetu. Kumbe ndio vimebeba dira/mwongozo wa maisha yetu ya kiroho na kimwili, hili huwa hatulifikiri kabisa kutokana na jinsi tulivyokuzwa kwa kulelewa bila kuhimizwa kuhusu umhimu wa hivyo vitu.
Kusoma Neno la Mungu ni jambo la muhimu sana na linapaswa kuwekwa kipaumbele kikubwa sana kutokana na uzito wake. Nimesema kila jambo linapaswa kupewa nafasi yake, ila hichi ninachokuambia unapaswa kuliweka vizuri zaidi ili mambo yako mengine yawe salama.
Muhimu sana ukaweka ratiba rasmi ya kusoma Neno la Mungu, yaani inapofika huo muda, hakikisha kila kitu kinasimama na kutuliza akili zako kuziandaa kusoma Neno la Mungu. Baada ya hapo tulia tena kutafakari yake uliyojifunza, ikiwezekana rudia tena kusoma kutokana na utaratibu wako uliojiwekea kusoma biblia.
Mfano mimi sasa hivi nasoma sura 1 au 2 tu kwa siku, sizidishi zaidi ya hapo, nataka kuelewa kile nasoma. Ninaposoma sura chache napata uwanja mpana zaidi wa kukumbuka kile nilichosoma, maana napata muda wa kutafakari. Sio kwamba nitakumbuka kila kitu, ila yapo ambayo yanakaa moyoni moja kwa moja.
Nimeona faida ya kuweka muda wa kusoma Neno la Mungu, maana inapofika saa ya kusoma Neno la Mungu nasikia kelele kubwa ya kutaka niachane na jambo lingine ninalolifanya. Ili niingie kwenye zoezi langu la kila siku, mara moja sana inatokea naivunja ratiba yangu niliyojiwekea kutokana na mahali nilipo. Inaweza kutokea kwa mwezi mara 1 au 2 au isitokee kabisa mpaka baada ya miezi 2 au 3 mbele, ila nahakikisha napata muda wa kusoma pale nilipoishia na kufika pale nilipopaswa kupafikia siku hiyo.
Kutenga muda rasmi ni muhimu sana, na ukiona huo muda utakuwa una jambo lingine ambalo hutoweza kuliacha, ni vizuri kutafuta muda katikati ili kuziba pengo la ule muda uliojiwekea siku zote. Hii inakufanya unakuwa na nidhamu ya kudumu kwa kile ulichoamua kufanya, na nidhamu hiyo itawafanya wale wanaokuzunguka kuanza kuiga mazuri kutoka kwako.
Fanya shughuli zako vizuri zinazokuingizia kipato, tena weka nguvu kubwa wakati unafanya. Ila inapofika ile saa ya kusoma Neno la Mungu, hakikisha upo tayari kusitisha kila kitu ili upate chakula cha kiroho. Hata kama unaendesha gari, kama unavyofanya ukiwa safarini unapoumwa njaa huwa unasimama kutafuta chakula. Vivyo hivyo na kwenye Neno la Mungu fanya hivyo, kuna hasara gani kupaki gari pembeni kwa dakika 20 au 30 kwa ajili ya kusoma Neno la Mungu?
Utaona hakuna hasara zaidi ya faida, kama hakuna hasara zaidi kuna faida, kwanini kusoma Neno la Mungu kusipewe uzito wake. Hebu kataa hali ya kupuuza suala la kusoma Neno la Mungu, hakikisha ratiba zako zinakuwa na kipindi cha NENO LA MUNGU.
Kazi yangu ni kuhakikisha wewe unaelewa umhimu wa kusoma Neno la Mungu, hiyo ndio furaha yangu. Na wewe kazi yako ni kufuata kile nakuelekeza, unaweza kuboresha zaidi hata kwa yale ambayo sijakuambia hapa ilimradi maboresho yale yawe yanalega usomaji wa Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, nathamini sana muda wako. Sitakuangusha, kuendelea kukuletea masomo mengine mazuri zaidi, unachotakiwa kufanya ni kuendelea kutembelea mtandao wetu wa chapeotz.com. Na kama ulikuwa bado hujajiunga group letu la whatsApp, unaweza kuungana nasi kwenye group la whatsApp ili tuwe karibu zaidi kupitia +255759808081.
Unaweza kutupata au ukawasiliana nasi kwa;
Fb: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.