Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai sasa na hata milele. Siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona, sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, kuendelea kutupa kibali cha kuwa hai.

Kuna vitu vidogo sana Lakini unapaswa kuvizingatia pale unapotaka kusogea hatua fulani katika maisha yako ya kiroho na kimwili. Bila kukaa chini kulijua kusudi la wewe kufanya hilo unalofanya, itafika kipindi utaacha kulifanya na hutokuwa na uchungu wowote.

Chochote kizuri kinacholisha moyo wako, unapaswa kujua kwa undani kinachokupelekea au kinachokusukuma ukitumie chenyewe na kuacha vingine. Unapofikia hatua hiyo, unajipa nafasi zaidi kukithamini hicho kitu au kukipuuza kutokana na mafikiano yako ya kufikiri kwako.

Unapaswa kujua sababu inayokupelekea uendelee kwenda kanisani, usipoijua sababu ya msingi ya kwenda utajisikia kawaida sana, na usipoenda napo hutojisikia uzito wowote ndani yako. Hii ni kwa sababu umeacha jambo la msingi sana, ambalo ni kujua/kufahamu kipi kinakufanya ufanye hicho kitu/jambo.

Unapaswa kujua sababu ya wewe mzazi kuwalea watoto wako katika maandili mema ya kumjua Mungu, unapaswa kujua kwa nini ni muhimu kumchapa fimbo mwanao anapokosea. Usipoelewa utawalea wanao kama mayai, wakikosea jambo hata kuwachapa utaona ni vibaya kwa kuona utawaumiza. Badala ya kuvuna matokeo mazuri ya kuwanyim a wanao fimbo, unavuna uharibifu mkubwa.

Muhimu sana kufahamu haya mambo tunayoyafanya, hata kama tutaanza kwa kiwango cha chini sana kuyafahamu/kuyajua. Ni vizuri sana kuanza na hatua ndogo, ikiwa na mwelekeo mzuri wa kwenda hatua nyingine kubwa zaidi mbele.

Unapaswa kujua kwanini unapaswa kumpenda mke wako, unapaswa kujua kwanini unapaswa kumweshimu na kumtii mume wako. Vyema ukatafakari kwa kina haya, vizuri ukajihoji sana na kujiweka kikao wewe mwenyewe. Ili unapofanya maamzi ya kutompenda mke wako uwe unajua matokeo yake ni nini, na unapofanya maamzi ya kutomweshimu na kumtii mume wako uwe unajua matokeo yake ni nini usipotekeleza huo wajibu.

Siku yamekutokea kwenye ndoa yako, uwe unajua kabisa hayo ni matunda ya uzembe wako. Nasema hivi, chochote unachokifanya unapaswa kujua kwanini unakifanya, unategemea nini katika kufanya kwako hicho kitu.

Nimekupitisha kwenye maeneo mbalimbali ili uweze kunielewa hili ninaloenda kukueleza hapa, nimeona usingeweza kunielewa haraka ama usingeona uzito wowote wa hili nililokuwa nataka kukuambia siku ya leo.

Najua unasoma Neno la Mungu hata kama kwa kusuasua, ama uliwahi kusoma Neno la Mungu siku za nyuma ila sasa hivi husomi tena kutokana na sababu zako. Napenda kukuuliza wewe unayesoma au uliyeanza kusoma biblia siku za karibuni, umewahi kuijua sababu haswa ya wewe kuanza kusoma Neno la Mungu?

Usiogope kama hukuwahi kufikiri hilo, cha msingi hapa mimi nakupa changamoto kuhusu hili ili unapokuwa umekaa na unapokuwa kwenye shughuli zako. Ujue kwamba una jambo unapaswa kulitengea muda ili uweze kupata mwafaka wake.

Sababu moja wapo kubwa ya kusoma Neno la Mungu, Neno la Mungu lipokuwa kwa wingi ndani yako, ni vigumu sana shetani kukuingiza kwenye mitego yake ukamtenda Mungu dhambi na kupotelea huko huko. Utakuwa mwepesi wa kujirudi haraka sana pale unapogundua unapoelekea unaenda kupotea zaidi.

Neno la Mungu linaimarisha uhusiano wako na Mungu, unakuwa karibu zaidi na Mungu wako. Unajua ahadi alizokuahidia Baba kwenye maisha yako, unajua haki zako za msingi kama mtu aliyeokoka.

Utakapojua hayo na mengine mazuri zaidi ambayo sijakutajia hapa, utakuwa unajisukuma mwenyewe kusoma Neno la Mungu bila kukumbushwa na mtu yeyote. Bidii utakayokuwa nayo haitakuwa ya muda fulani, itakuwa ni bidii ya kudumu katika maisha yako ya wokovu.

Kumbuka kufanyia kazi hili, jua sababu inayokufanya uwe unasoma Neno la Mungu. Nitaomba mrejesho wako kwa kuniandikia ujumbe wako kwa mawasiliano nitakayotoa hapo mwisho au unaweza kutoa comment yako hapo chini. Wazo lolote lile usiogope kunishirikisha litakuwa la maana sana kwangu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, kazi yangu ni kuhakikisha unapata uelewa juu ya umhimu wa kusoma Neno la Mungu. Usiache kutembelea mtandao wetu wa chapeotz.com kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Unaweza kuwasiliana nasi na ukatupata kupitia;
Fb: Chapeo Ya Wokovu,
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081