Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, Mungu anaendelea kutupa kibali cha kuziona siku zingine zaidi. Inaweza kuonekana ni kawaida kwetu, ila ki ukweli sio kawaida, ipo sababu ya kumshukuru Mungu na kumrudishia sifa na utukufu.
Kuna mwimbaji mmoja akaimba wimbo ukisema “Dunia Haina Huruma” ukifikiri haraka haraka na ukisoma au ukisikia kichwa cha ujumbe wake unaweza kusema huyu anamaanisha nini anavyosema Dunia haina huruma.
Ukitaka kujua Dunia haina huruma, mpende mtu kwa moyo wako wote, mpe kila hitaji lake analotaka. Atafika siku atasahau wema wako wote uliomtendea, badala ya kupokea shukrani utapokea majuto.
Unaweza kumlea mwanao vizuri leo, ukamfikisha hatua zile ulizopaswa kama mzazi kumtendea mwanao. Ikafika wakati amefanikiwa kimaisha, akainguwa tamaa ya kufanikiwa zaidi kwa njia zisizo halali, anaenda kwa waganga wa kienyeji anaambiwa ili upate unachohitaji mtoe mama yako kafara/sadaka.
Bila kukumbuka wema uliomtendea, atakubali kutoa damu yako ili apate mali nyingi zaidi. Kama hukuwa vizuri na Mungu wako, uwe na uhakika unaenda kufa kifo ambacho hukupaswa ufe ukiwa na umri ule.
Unaweza kumpenda mdada/mkaka(mchumba), ukajitoa kwa namna ya pekee sana kumthamini na kujitahidi kadri ya uwezo wako kuhakikisha anapata kile anahitaji kwako. Wengine mpaka wanajitoa kusomesha, wengine wanajitoa kuwajengea wachumba wao nyumba, wengine wanajitoa kuwanunulia magari, wengine wanajitoa kuwafungulia maduka makubwa.
Ikafika siku akaanza kukuambia kwa vitendo viovu sikuhitaji wewe, namhitaji huyu unayeniona nipo naye sasa. Unaweza kushikwa mshangao wa ajabu ila kumbuka nimekuambia dunia ikitaka kukuadhibu haitakuwa na huruma na wewe.
Ninaposema SOMA NENO UKUE KIROHO, nina maanisha kile nakueleza hapa. Kuna vitu vigumu utakutana navyo katika maisha yako, penda usipende jua ipo siku utakutana na vitu vya kuujeruhi moyo wako.
Mpaka kufika umri huo nina uhakika umekutana mambo mazito ya kuujeruhi moyo wako, na mpaka sasa mengine unasema umesamehe lakini bado unaona kabisa moyoni mwako kuna hali ya kuumia na kulia machozi.
Ukikaa ukiwaza unaona mbona dunia hii haina huruma kabisa, mtu umtendee wema wote alafu leo hii anaenda kukukana mbele za watu. Leo hii mume wako anatembea na wanawake wengine amekuacha wewe mke wake, wakati anaumwa ulikuwa unamfulia mpaka nguo zake za ndani alizochafu kwa haja kubwa. Maana ilifika kipindi ndugu zake wote wakamkimbia na kukuachia wewe hapo, umehangaika huku na kule kutafuta msaada.
Unaweza kufikiri na ukalia sana, ukajihisi kulia sana labda haitoshi, badala ya kumwombea Rehema kwa Mungu. Unaweza kuanza kumwomba Mungu amuue kabisa usimwone tena duniani, kweli kwa jinsi alivyokutendea utakuwa umewaza hivyo.
Pamoja na dunia hii haina huruma, bado dunia hii hii inahitaji watu jasiri, watu wanaoweza kuumizwa na kujeruhiwa mioyo yao. Lakini bado ukawakuta wanasema Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yao, watu wanaopambana kuhakikisha hawarundishwi nyuma kiimani kwa sababu ya kutendwa vibaya na ndugu zao.
Huenda hapo ulipo unapewa historia yako kuwa wakati bado mtoto mdogo, mama yako mzazi alikutupia kwenye shimo la choo baada ya baba yako kukataa ujauzito wako. Ukaokolewa na wasamaria wema wakakuelea na kukukosemesha shule nzuri mpaka ukamaliza. Leo hii unawaona wazazi wako wote wawili wanakuja kukuomba msaada wa kifedha huku wewe ukiwa na maisha mazuri.
Ukijilemaza na kuanza kutafuta huruma za wanadamu unaweza kufa siku sio zako, maana pamoja na dunia imebeba watu wasio na utu. Bado dunia hiyo hiyo inahitaji kuona washindi waliovumilia mapito mbalimbali magumu wakashinda. Dunia ile ile inakuja kuwapa majina ya washindi wale aliowajeruhi, lakini kabla ya hapo ilikucheka na kukudharau.
Leo baba anakupigia simu anahitaji umpe fedha, lakini tangu unazaliwa na mpaka unafikia utu uzima na familia yako ya watoto. Aliyehangaika kukulea ni mama yako, aliumiza kichwa huku na kule kuomba misaada kwa ndugu, jamaa na marafiki kuhakikisha mwanaye anafikia hatua nzuri kielimu. Mama alikuwa sio mwajiriwa wa serikali wala shirika/kampuni yeyote, lakini alifanya kila biashara kuhakikisha unakula na unaenda shule.
Anakuja mzee wako, kukuambia mimi ndio baba yako. Na ukiangalia kweli ni baba yako mzazi, na mnafanana kweli kweli. Anakueleza shida zake umsaidie, nakwambia unahitaji stamina za kweli kutoka Mungu mwenyewe. Unaweza ukalia sana na ukamwambia Mungu mbona anakuonea sana, mtu amwache/amkimbie mama yako kwa miaka yote 20 au 30, tena kwa kukataa ujauzito wako. Leo hii anakuja kuomba msaada kwako‼‼
Dunia inajua hayo yote ila haitaki kukuhurumia wewe, bado inakukandamiza zaidi. Na usipoachilia huo mzigo wa maumivu, jehanamu inakuhusu kabisa, maana huo ni mtego wako kabisa unapaswa kuachilia ndani mwako.
Baada ya kukueleza hayo, huenda kuna eneo nimekukumbusha na umejisikia machozi moyoni mwako. Huenda unasoma ujumbe huu, wakati huo unaendelea kushindana na machozi kwa kuyafuta na kitambaa chako. Kwanza mshukuru Mungu kukuletea ujumbe huu maana unaenda kuwa uponyaji kwako.
Suluhisho la haya yote ni kusoma Neno la Mungu, kama dunia inahitaji watu jasiri na wanaoshinda changamoto mbalimbali ngumu katika maisha yao. Na dunia haina huruma kabisa pale inapoamua kutuchapa/kutuadhibu, inatuchapa/inatuadhibu kweli kweli. Tunapaswa kulijaza Neno la Mungu kwa wingi ili tuweze kusimama na miguu yetu wenyewe.
Neno la Mungu linatusaidia kuondoa takataka mbalimbali ya mambo yanayotaka kututoa kwenye njia sahihi ya Yesu Kristo. Unaweza kuona nakutania lakini amini ninachokueleza hapa, unapoambiwa ufalme wa Mungu unatekwa na wenye nguvu, usije ukafikiri ni utani utani. Ni jambo la kweli kabisa, sasa wewe unaweza kunyanyaswa na hali yako unayopitia ukaacha na wokovu.
Wenzako wanakutana na mambo magumu tena sio magumu tu, ni mazito hata kusikia hutamani kuyasikia kabisa. Lakini bado wanaendelea mbele, bado wanafurahia wokovu wao, tena wana afya nzuri, hawana magonjwa ya presha presha, hawazimii zimii kwa taarifa mbaya.
Kinachowafanya wawe hivyo ni hazina ya Neno la Mungu wanalilowekeza na wanaloendelea kuwekeza mioyoni mwao. Siku zote wanajihisi washindi na kweli wanashinda mengi wanayokutana nayo.
Dunia inapoona hivyo bila kusukumwa na chochote, inasema huyu mtu ni mshindi. Itatamka maneno ambayo yataandikwa pande zote nne za dunia, utakuwa shuhuda wa wengi waliokata tamaa, walioona wameonewa sana.
Unaweza kuwa huelewi sana faida ya kusoma Neno la Mungu, nakuambia ipo siku yaja utakuja kuona faida ya maarifa uliyowekeza ndani yako. Endelea kusoma Neno la Mungu, kama dunia haiwezi kukuonea huruma, kwanini usiitafutie jambo la kuishinda pale inapotaka kukuangusha.
Ungana na wenzako waliopo group la whatsApp, kusoma Neno la Mungu kila siku. Usiwe nyuma kwa hili, hakikisha unapata mtu aliyeokoka na mwenye safari ya kwenda mbinguni. Mweleze umhimu wa kusoma Neno la Mungu, hakikisha unamwalika katika group la Chapeo Ya Wokovu. Au mwambie atumie hizi namba kunitafuta
0759808081, Kumbuka kutumia njia ya whatsApp kuwasilina nami.
Ahadi yangu kwako ni kuhakikisha unafikia malengo yako, ni kukikisha unaelewa umhimu wa kusoma Neno la Mungu. Na kuhakikisha unalipenda na kuliona ni chakula chako cha kiroho, usipokula kwa muda mrefu ujisikie kupoteza uhai wako.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa chapeotz.com kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Unaweza kutupata kwa mawasiliano yafuatayo;
Fb: Chapeo Ya Wokovu.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.