Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuifikia. Tumshukuru Mungu na kumrudishia sifa na utukufu kwa neema hii anayoendelea kutupa.
Kuna watu wanajiweka bize kiasi kwamba unashindwa kuelewa huu ubize una leta faida au ni mtu tu ameamua kujiweka hivyo. Kwanini nasema hivi, unamkuta mtu yupo online whatsApp au facebook au intagram, yupo muda mwingi sana. Ila ukimuuliza vipi ndugu yangu mbona husomi Neno la Mungu, atakuambia unajua nabanwa sana na shughuli, atakuambia unajua nashindwa kupata kabisa muda wa kushika Biblia kwa ubize wa shughuli zangu.
Ukija kwenye mitandao ya kijamii unamkuta anapatikana kirahisi sana, kwenye magroup ya kuchati yupo mstari wa mbele sana kuchangia mada mbalimbali. Hata kama hachangii chochote ila anasoma kila ujumbe unaoingia, ila kwenye Neno la Mungu shughuli zinambana.
Shughuli zetu ndio zimekuwa furushi letu la kubebea lawama zote za uzembe wetu, mwingine yupo tu mtaani anazunguka tu. Anatoka mtaa huu anatokea mtaa mwingine, ila ukimgusa uwe na muda wa kusoma Neno la Mungu, atakupa hadithi zile zile za nipo bize sana ndio maana sipati muda wa kusoma Neno la Mungu.
Mwingine anashindia movies akitoka kazini, yaani anakuambia nipo sehemu ya 90 nikifuatilia huu mfululizo wa movie. Lakini ukimgusa kwenye kusoma Neno la Mungu atakuambia nimebanwa sana na shughuli zangu, nabanwa sana chuoni ndio maana siwezi kusoma Neno la Mungu.
Huyo anayekuambia anabanwa sana na chuo, anamaliza sms 1,000 kwa siku moja, kwa kuchati tu na wenzake. Hizi sms sio za whatsApp, ni sms za kawaida kabisa, ila mguse sasa kuhusu mpango wa kusoma Neno la Mungu. Hapo ataongea kila neno ambalo litakufanya uone huyu mtu kweli amebanwa, ila mfuatilia uone anachosema ndicho kinafanyika kweli au vipi. Nakwambia ukijua anachofanya utachoka mwenyewe.
Tukubali tuna shida ndani yetu, kama hatuna hamu ya kusoma Neno la Mungu ila tunashindia kufanya vitu ambavyo havina hata faida kwetu. Tusifichane tuabiane tu ukweli, tuna shida ndani yetu, sawa umeokoka muda mrefu ila wokovu wako upo chumba cha wagonjwa mahututi. Maana tangu uokoke bado umejaa uchanga wa kiroho, umejaa hofu na mashaka, huna imani kuhusu Yesu wako, ukiguswa kidogo na tatizo unapata hamu ya kwenda kutafuta msaada kwa miungu mingine.
Huna uwezo wa kusimama kwa mtu hata mmoja kumshuhudia habari za Yesu Kristo, umejaa uoga na mashaka kuhusu kumwamini kwako Yesu Kristo. Ukibanwa kidogo unasema Mungu wetu ni mmoja, hata kama mtu unamjua kabisa anaabudu miungu mingine. Kwa sababu huwezi kumtofautisha Yesu wako, na yeye akikutazama matendo yako na ya kwake, anaona mbona wote mpo sawa… unakuwa huna ujasiri wa kuendelea kusema naye.
Tuache kusingizia majukumu/shughuli, ukiamua kutenga muda wa nusu saa kila siku, hakuna hasara utaingia zaidi utapata faida nyingi sana kupitia kusoma Neno la Mungu. Usikae unajipa moyo kuwa Mungu anajua umebanwa sana na shughuli, umebanwa sana vipi mbona vitu vingine unafanya kwa muda mrefu sana na havipo kwenye mpango wa shughuli zako.
Acha kujifichia kwenye koti la shughuli/kazi zako, unataka kusema Mungu amekosea kukupa kibali cha kuwa na hiyo kazi? Unataka kusema Mungu amekosea kukuinulia wazazi/ndugu waliokuwa tayari kukusomesha hicho chuo? Kama hapana, mbona humpi Mungu nafasi ya kwanza katika mambo yako?
Hebu kuanzia leo, ona hili jambo la kusoma Neno la Mungu ni muhimu sana kwako. Ninamaanisha ninapokuambia ni muhimu sana kwako, zipo faida nyingi sana utazipata kupitia Neno la Mungu, siwezi kukutajia zote nikazimaliza.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kufanyia kazi yale umejifunza. Pia hakikisha hukosi kutembelea mtandao wetu wa chapeotz.com kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Kazi yangu ni kuhakikisha unaelewa umhimu wa kusoma Neno la Mungu, ni matumaini yangu ipo siku utanielewa, kama sio leo itakuwa kesho, na kama sio kesho basi itakuwa wakati mwingine wowote ule.
Unaweza kutupata kwa;
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081