Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, tunao ujasiri wa kujivunia jina la Yesu Kristo. Maana tangu mwanzo alitupenda sisi na kujitoa kwa ajili ya dhambi zetu wanadamu, ili tuweze kurejesha uhusiano/ushirika wetu na Mungu wetu uliopotezwa na dhambi. Tena tunaongea habari za aliye hai sasa hadi milele, ndio maana hatupaswi kuwa wanyonge tukiwa kama watu waliokoka.
Karibu sana tujifunze mambo ya kukusaidia kujua yale muhimu unayopaswa kuyafanya ili uwe na msingi usioweza kutetereshwa na jambo lolote linapokujia. Msingi utakaoweza kukusaidia mambo mengine yakamalizwa yenyewe bila kukuathiri wewe moja kwa moja.
Ili upate nyumba imara, unapaswa kutengeneza msingi imara, kama ni kushindilia mawe, unapaswa kuyashindilia ya kutosha haswa. Kama ni kumwaga zege, unapaswa kuimwaga haswa. Ili utakaposema msingi wa nyumba yangu umemalizika uwe na uhakika utaweza kukabiliana na mzigo mzito.
Wakati wa kujenga msingi kunahitaji umakini, pia kunahitaji uvumilivu wa kiwango cha juu sana. Maana ni wakati ambao una changamoto ngumu sana, muda mwingine unaweza usieleweke kabisa kitu/jambo unalolifanya.
Wakati unaanza kujenga msingi wa nyumba, unaweza usiwashtue sana watu wengi wanaokuzunguka na wale wanaopita eneo ulofanya hiyo shughuli. Lakini wakianza kuona ukuta umesimama, hapo ndipo wataanza kuona kumbe huyu ndugu alikuwa anamaanisha kujenga kweli.
Wakati unaanza wokovu ulijitengenezea msingi gani, ulijitengenezea msingi imara au ulijitengezea msingi ambao mvua ikinyesha kidogo unaanza kuona nyumba ikititia chini. Uliepukana na marafiki wabaya au uliogopa kukosa vitu fulani kwao, hao marafiki zako wanatambua wewe umeokoka na wakitaka kuzungumza mambo mabaya wanasimamisha kuongea kutokana wanakujua hupendi mambo yasiyofaa?
Msingi wako umeutengenezaje, au unaishi kama upepo, hueleweki umesimamia wapi, watu wanashindwa kukuweka kwenye mtu aliyeokoka au asiyeokoka. Maana unachanganya mambo, huna msingi uliosimamia.
Nikushauri jambo moja, kama hujatenengeza msingi katika maisha yako kwenye eneo lolote lile ulipo. Uwe na uhakika hutoweza kusimama vizuri na Mungu wako, utakuwa mtu wa kutangatanga, ndio wale tunawaita bendera fuata upepo au vuguvugu, wa moto sio moto na wa baridi sio baridi yaani haileweki yupo kundi gani.
Tengeneza msingi unaotoka kwenye Neno la Mungu, jua Mungu anakutaka ufanye nini na usifanye nini. Hakikisha unasimamia hili kwa hali zote kadri utakavyoweza kusimama, utachukiwa na wengi wasiopenda mambo ya Mungu ila uwe na uhakika itafika wakati watakuelewa.
Tengeneza msingi imara wa kusoma Neno la Mungu, msingi ambao hutoweza kubomoka ovyo, mwanzo utapata mateso na tabu nyingi. Hii ni kutokana hujazoea utaratibu wa kusoma Neno la Mungu, pia inatokana na mambo mapya na magumu ndani ya biblia yako. Hilo lisikupe shida, wewe endelea kumwaga zege kwenye msingi wako, ukishasimama vizuri usiache kumwagilia maji kabla ya kuanza kusimamisha ukuta.
Ukishatengeneza misingi imara, itakuwa rahisi sana hata kwa kizazi chako kuja kufuata humo humo. Usifikiri unachokifanya leo hakina mchango wowote kwenye kizazi chako, upo mchango mkubwa sana kwenye huo msingi unaoujenga leo.
Ukijenga msingi wa uzembe, ndivyo itakavyokuwa hata kwa kizazi chako, na ukijenga msingi imara, ndivyo na kizazi chako watetembea humohumo kwenye uimara. Hata kama wataenda kinyume, mioyoni mwao watasema baba/mama hakuenda hivi, alikataza kabisa kuishi maisha ya namna hii.
Jenge msimamo mzuri ulio ndani ya msingi wa Neno la Mungu, itakusaidia wewe na kizazi chako. Mara nyingi tunayumbishwa na maisha kwa sababu hatuna msingi imara tuliojiwekea katika maisha yetu.
Vizuri pia kuangalia msingi wako, usije ukawa ulijenga au ulijengewa msingi mbovu ukaendelea kuusimamia. Utakuwa unaona mambo yako hayaendi vizuri kutokana na msingi mbovu ulionao ndani yako. Tena itakuwa vizuri sana baada ya ukagundua msingi ulionao sio sahihi ukabomoa pote na kuanza kujenga upya.
Ipo gharama ya kufanya hivyo, yapo matamko ya wewe kushindwa, yapo maneno ya kukusema vibaya, yapo maneno ya kukushambulia usiweze kuendelea na kile umekidhamiria ndani yako, chenye kumletea Mungu sifa na utukufu. Hayo yasikumbue, kama umeijua kweli ni ipi, kubali kujenga msingi upya haijalishi umri ulionao.
Narudia tena, kama uliishi maisha ambayo hayakumpendeza Mungu, bomoa misingi yote ya vile vitu ulivyoamini miaka yako yote mpaka umefika hapo. Nasema hivi; kuna eneo umeona kabisa hukulea watoto katika msingi mzuri wa kumpenda Mungu, hakikisha unaanza upya kadri Mungu atakavyokuwedhesha. Kwenye ndoa yako vivyo hivyo, kwenye maisha ya ujana kuelekea ndoa vivyo hivyo, kwenye kazi yako vivyo hivyo, kwenye biashara yako vivyo hivyo, kwenye huduma yako vivyo hivyo.
Weka msingi mzuri wa usomaji wako wa Neno la Mungu, hakikisha hili jambo linaingia moyoni mwako kiasi kwamba mtu hawezi kukuambia kitu kuhusu kusoma Neno la Mungu. Ifike wakati umwone adui yako yeyote anayekukataza kusoma Neno la Mungu, utaona maisha yako yakibadilika kwa kiroho na kimwili.
Mungu akubariki sana kwa kutenga muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutafakari zaidi kuhusu haya nimekueleza. Utaona mabadiliko makubwa sana kwenye usomaji wako wa Neno la Mungu, na chochote kile unachofanya.
Kazi yangu ni kuhakikisha unaelewa umhimu wa kusoma Neno la Mungu, sitakuangusha katika hili maana naweka msingi imara kwako ili uwe msaada kwa wengine pia. Huenda nisiwafikie mimi ila wewe ukaweza kuwafikia.
Nikutakie siku njema iliyojaa ulinzi wa Mungu.
Tunapatikana kwa njia hizi;
Facebook: Chapeo Ya Wokovu,
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.