Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai sasa na hata milele, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Tunapaswa kumshukuru Mungu kutuamsha salama na kuendelea kutupa uhai wake.

Uchanga wa kiroho ni ugonjwa mbaya sana unaotafuna wakristo walio wengi sana, bila wao kujijua kama wana shida ambayo inahitaji msaada wa haraka iwezekanavyo. Wameona kuishi hivyo inawafaa kwao, kutokana na wanavyoona wao.

Kubali ukatae, haijalishi umeokoka mwaka gani, kama husomi Neno la Mungu. Ukubaliane na mimi hapa, utakuwa mchanga wa kiroho aliyedumaa miaka mingi ndani ya wokovu. Kwanini nasema hivyo, nasema hivyo kwa sababu mambo mengi hayajui yaliyo ndani ya Neno la Mungu.

Kama husomi Neno la Mungu unaweza kulishwa mafundisho mbalimbali yakakuaminisha maisha fulani ndio sahihi kwako. Ukaendelea kushikilia hivyo, ukaishi maisha ya kujibana kiasi kwamba unaona hata kuokoka kwako hakuna furaha kabisa. Kutokana na jinsi ulivyojiwekea kuta kila kona, ukiona ni sahihi kufanya hivyo.

Mwingine ameokoka miaka mingi sana ila anavyogopa uchawi sasa, utafikiri hana Mungu wa kweli ndani yake. Anaona uwezo wa miungu mingine ni mkubwa zaidi kuliko Mungu wake, kinachompelekea ajione hivyo ni kwa sababu hana Neno la Mungu la kutosha ndani yake.

Mkristo yeyote aliyejaa Neno la Mungu moyoni mwake, anayelitafakari usiku na mchana, imani ya mkristo yule ipo juu sana. Tena anatamani kusoma zaidi Neno la Mungu, haijalishi amesoma mwanzo mpaka ufunuo. Bado utamwona ana kiu ya kutulia na biblia yake, akitaka kujua Mungu anasema nini juu ya maisha yake ya wokovu.

Hivi kweli utamwogopaje mchawi, sipendi sana ujumbe wangu ujae mazungumzo ya wachawi, ila inanibidi nifanye hivyo kumwondoa mtu mmoja aliyefungwa kwenye eneo hili. Najisikia moyoni kulisemea hili, maana limekuwa tatizo kwa wengi wetu. Unapozungumzia uchawi, unazungumzia ulimwengu wa roho, na wote tunajua vita vya roho vinapiganwa kiroho.

Rejea: Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Waefeso 6:12 SUV.

Unapoogopa maana yake unataka kuikimbia, utakimbiaje ulimwengu wa roho? Ni kitu kisichowezekana. Lakini kwa sababu hatupendi kutulia mbele za Mungu tukisoma na kutafakari Neno lake, tunajikuta kwenye vifungo ambavyo vimegeuka mateso kwetu.

Hebu nikuonyeshe ukuu wa Mungu kupitia mstari huu, ni tangazo zuri sana masikioni mwetu kama utaelewa kilichosemwa hapa;

Rejea: Moto hutangulia mbele zake, Nao huwateketeza watesi wake pande zote. Umeme wake uliuangaza ulimwengu, Nchi ikaona ikatetemeka. Milima iliyeyuka kama nta mbele za BWANA, Mbele za Bwana wa dunia yote. Mbingu zimetangaza haki yake, Na watu wote wameuona utukufu wake. Na waaibishwe wote waabuduo sanamu, Wajivunao kwa vitu visivyofaa; Enyi miungu yote, msujuduni Yeye. ZABURI 97:3‭-‬7 SUV.

Umeona hayo maandiko? Hapo mwishoni kabisa miungu yote imepewa amri ya kumsujudu Mungu, na sio miungu isujudiwe na Mungu. Sijui kama unaelewa ninachosema hapa, nasema hivi; boss wa vyote viliopo duniani na mbinguni viwe vizuri au viwe vibaya, haviwezi kushinda uwezo wa Mungu.

Huyo ambaye anapaswa kusujudiwa na miungu, na huyo anayeshusha moto, na huyo anayetetemesha nchi, na huyo anayeweza kuwaibisha waabudu sanamu. Ndiye aliye ndani yako, maana yake una silaha yenye uwezo mkubwa ila hujui hilo, una mwenye mamlaka anayeweza kunyamazisha dunia yote kwa sekunde moja na dunia yote ikanyamaza kimya. Huyo ndiye aliye ndani yako, alafu unakuwaje na mashaka/wasiwasi wa maisha yako?

Unatashiwa na bibi fulani mchawi unahainga siku nzima huli na hulali vizuri, kisa umeambiwa utaona. Unashindwa kumwambia Baba kuna mtu ananiambia nitaona, shughulika naye aone uweza na nguvu zako. Maana adui zako ni adui za Bwana, labda huamini hili;

Rejea: Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao. Kutoka 23:22 SUV.

Bwana atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba. Kumbukumbu 28:7 SUV.

Huenda nikisema sana utaona natunga kichwani tu hakuna kitu kama hicho, nimekupitisha kwenye maandiko machache ili uone uweza wa Mungu kwa yule aliyeokoka. Unaishi maisha ya wasiwasi kwa sababu huna Neno la Mungu moyoni mwako, unajihisi mtu wa kulogwa kila wakati kwa kutojua uwezo wa Mungu ulio ndani yako.

Kuepukana na hayo yote, amua sasa kusoma Neno la Mungu, sina maneno mazuri zaidi ya kukusaidia katika hili. Kama hujui kusoma tafuta audio bible, nenda play store tafuta biblia za sauti utapata za lugha ya kiswahili kabisa. Soma kwa njia ya kusikiliza maandiko matakatifu, utapata kitu kilekile kama anayesoma kawaida na kuweza kuona ahadi mbalimbali juu yako.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea mtandao wetu wa chapeotz.com kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Ahadi yangu kwako ni kuhakikisha unaelewa umhimu wa kusoma Neno la Mungu, ili utoke kwenye uchanga wa kiroho na ukuzwe kiroho na Neno la Mungu. Zaidi ya hapo utaendelea kuwa mchanga miaka yako yote alafu umeokoka, ni hasara kubwa mno.

Nakutakia siku njema.

Unaweza kutupata kwa;

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.