Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, kutupa kibali cha kwenda kuendelea kutimiza malengo yetu pale tulipoishia jana.

Kuna vitu ambavyo vinaweza visiwe vizito sana kutokana na jinsi vilivyokaa, kutokujua kama vina uzito mkubwa sana. Huwa mara nyingi tunavipuzia na kuviona vya kawaida na havina maana sana kuvizingatia. Ndio maana wengi tukigusiwa kuhusu hivyo vitu tunaona ya nini kujihangaisha.

Siku hizi tukisikia miili yetu ina shida sehemu huwa tunakimbilia kuangalia nini kinatusumbua ndani yetu, tofauti na miaka ya nyuma ilikuwa ukisikia unaumwa. Unachofanya ni kumeza dawa za malaria, lakini siku hizi unaweza kumeza dawa za malaria kumbe unaumwa kitu kingine.

Kama ilivyo mambo ya mwili ukipata shida unaenda kuangalia unasumbuliwa na nini, na wakati mwingine husumbuliwi na kitu chochote. Ila unaona ngoja nikafanya vipimo vya mwili mzima, unaweza kujikuta upo vizuri kabisa na ukapewa ushauri kwa baadhi ya maeneo. Vilevile unaweza kukutwa ulikuwa unaumwa kitu fulani pasipo kujua wewe kwa hali ya kawaida, ambapo wewe ulikuwa unasumbiri usikie homa ndipo ukapime.

Leo nakutaka ufanye uchunguzi wa jambo hili, wakati unaendelea kusoma somo hili, jitahidi kujua upo salama au haupo salama. Uwe mkweli kabisa maana hakuna atakayekuona ni wewe tu na Mungu wako.

Unaposoma Neno la Mungu huwa unajisikiaje, unajisikia furaha ndani yako au huwa husijikii chochote zaidi ya kusoma na kufunika Biblia yako ukaendelea na mengine. Je unapomaliza kusoma biblia yako pale unapotafakari yale uliyosoma huwa unajisikia kitu gani ndani yako? Unajisikia raha ndani yako au huwa huhisi chochote?

Kama huhisi chochote pale unapotafakari maandiko matakatifu, bila shaka una shinda ndani yako. Na usikimbilie kusema huna shida, ipo shida ndani yako na unapaswa kupata tiba haraka sana ili usiendelee kuharibika zaidi.

Unapaswa kujisikia vizuri kabisa ndani yako unaposoma Neno la Mungu, pale unapoendelea kutafakari yale uliyojifunza. Hapo ndipo furaha yako inapaswa kuendelea kuwa kubwa zaidi, kwanini iwe kubwa? Kuna eneo ulikuwa umekwama ukafunguliwa ufahamu wako na Neno la Mungu, kuna mahali uliona hata iweje haitawezekana tena. Ila kupitia kusoma Neno la Mungu ukaona inawezekana, hapo lazima furaha iwe kubwa ndani yako.

Sio maigizo kwamba unaposikia kuna watu wanajisikia raha ndani ya mioyo yao pale wanapotafakari maneno ya Mungu, pale wanapotafakari ukuu wa Mungu juu ya maisha yao. Usifikiri ni utani na jambo lisilowezekana, shida yako upo kama mtu anayeumwa ndio maana unaona hakuna jambo kama hilo.

Hata tunaposoma maandiko matakatifu tunaliona hili lipo, kutafakari kwako lazima kuwe kutamu kama unavyopata ladha ya chakula unachokipenda. Hupaswi kusoma Neno la Mungu kama vile unakula chakula usichokipenda kukila, ila kutokana na mazingira uliyopo. Unaona ngoja ule tu ila ukweli kabisa mdomoni kinakataa kutafunika, unachofanya ni kufumba macho ili uridhishe tumbo.

Wakati mwingine unakuwa mgonjwa kiasi kwamba kila chakula unakiona kibaya kwako, ndivyo ilivyo hata kwenye mambo ya Mungu. Kuna watu ni wagonjwa kiasi kwamba, kuomba kwao ni kubaya, kwenda kanisani kwao ni kubaya, kufanya kwao huduma waliyokuwa wanaifanya wanaona haina maana tena. Kila kitu kwao ni kibaya, sasa hapo wasipokuwa makini na wasipokutana na ujumbe wa Neno la Mungu, ni rahisi sana kwao kumwacha Yesu Kristo.

Tafuta hamu ya Neno la Mungu, tafuta utamu pale unapotafakari Neno la Mungu, usikubali kuwa mdhaifu katika eneo hili. Usione kawaida wakati wenzako wanafurahia ukuu wa Mungu kwa kadri wanavyozidi kumjua kupitia Neno lake.

Rejea:Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake; Mimi nitamfurahia BWANA. ZABURI 104:34 SUV.

Unaona huna utamu wowote unaoupata kwenye kusoma kwako Neno la Mungu, mwambie Mungu rejesha hamu yangu ya kusoma Neno la Mungu. Eleza kwa uwazi kabisa ukiamini Mungu anaweza kukupa kile unaomba kwake, usikae kimya wakati umenyang’anywa furaha ya wokovu wako.

Rejea: Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi. ZABURI 51:10‭-‬12 SUV.

Omba Mungu maombi ya namna hiyo, hiyo ndio itakuwa tiba yako, acha kuendelea kunywa dawa ambazo hujapata vipimo vyake. Kipimo kinaonyesha unapaswa kurejeshewa furaha ya wokovu wako, na dawa za kumeza ukapona ni maombi yako kwa Mungu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, bila shaka kuna kitu umejifunza siku ya leo. Nakusihi usiache kutembelea mtandao wetu wa chapeotz.com kwa masomo mengine mazuri zaidi kadri Roho Mtakatifu akavyotuwedhesha.

Kazi yangu ni kuhakikisha unaelewa umhimu wa kusoma Neno la Mungu, hili tu ndilo linanifanya nikuandikie haya yote. Na sitochoka kamwe kukueleza hili.

Nakutakia siku njema.

Unaweza kutupata pia kwa;

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.