Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, nafasi nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuifikia. Kazi yetu ni kwenda kumzalia matunda yaliyo mema na kumletea sifa na utukufu.

Wakati mwingine tunawaza tukimjua Mungu sana Labda tutapunguza vitu fulani kwake, hali kama hii inawafanya wengi wakishakuwa kwenye daraja fulani la kufahamika sana. Ile bidii yao ya mwanzo ya kuutafuta uso wa Mungu inapotea kabisa, shida haswa ni ile kufikiri kiwango alichofikia hakihitaji kuwa na bidii zaidi ya kumtafuta Mungu.

Wengi waliofanikiwa kuwa maarufu kwa utumishi wao, wameacha ile bidii yao ya kusoma Neno la Mungu, wameacha ile bidii yao ya kuomba. Lakini wakati anapambana kutoka alikuwa na bidii kubwa na nidhamu ya hali ya juu sana kuhusu mambo ya Mungu.

Chunguza vizuri waimbaji wanapotaka kwenda kurecord CD/DVD zao, wana bidii sana ya kuomba, wanabidii sana kusoma Neno la Mungu. Kweli wanapopanda madhabahuni kuhudumia wengine unaona uwepo wa Mungu ukiwa juu yao na ukihudumia watu wengine. Baada ya kumaliza hilo shughuli ya ku record, ile bidii yao na usiriaz wa huduma unatoweka kabisa.

Shida yao ipo wapi, wanafikiri kuwa na viwango fulani vya kiMungu vinapaswa kuwa vya muda tu baada ya hapo havihitajiki tena. Ndio kosa la wengi sana wanalolifanya, kulipuka na kupotea baada ya kumaliza na kukipata kile ulikuwa unakihitaji, inakuwa sio salama sana kwa mwamini mwenye safari ya kwenda mbinguni.

Unapoweka bidii yako ya kumsogelea Mungu kwa njia ya kujisomea Neno lake, utajikuta unapata hamu zaidi ya kusoma Neno la Mungu. Sio kwamba ukisoma Neno la Mungu mara moja unakuwa umeshiba moja kwa moja, badala yake utajikuta unakuwa na hamasa zaidi ya kumjua Mungu wako kupitia Neno lake.

Unapojikuta huna hamu ya kuendelea kujifunza Neno la Mungu, unapaswa kujirudi na ujitafakari kwa upya. Lazima kutakuwepo shida inayokufanya ukose hiyo hamu, hatusomi Neno la Mungu kwa matukio maalum.

Usisubiri upangwe kuhubiri ndio uanze kutafuta mistari ya kufundishia, utakuwa unajidanganya mwenyewe. Usikubali ile sauti inayosema ndani yako kwamba biblia nimeisoma yote, haina haja kuendelea kuisoma zaidi, moja ya kosa kubwa ni pamoja na hilo la kufikiri umemaliza kila kitu.

Haijalishi wewe ni kiongozi wa kanisa, kusoma Neno la Mungu ni muhimu sana kwako, sio unawaambia washirika/waumini wako someni Neno la Mungu alafu wewe husomi. Unapaswa kusoma Neno la Mungu kila siku, unapoandaa somo la kwenda kuwalisha wengine uwe tayari wewe umeshiba hilo Neno.

Hatari kuwapelekea wengine chakula ambacho wewe mwenyewe hujui ladha yake, wala hujawahi kukila na kama umekila hujawahi kupata ladha yake. Ila kwa sababu umeona wengi wanakitumia na wewe unataka ukitumie kuwalisha wengine.

Mwanzo nilikuambia kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu ndivyo unavyozidi kufunguka zaidi na unapata hamu ya kwenda mbele zaidi. Hakuna siku utakinai Neno la Mungu, inaweza kutokea hivyo kwenye vitabu vingine ila sio biblia iliyobeba Neno la Mungu.

Chochea hamu yako kwa kuendelea kusoma Neno la Mungu, utakapoacha na hamu yako inaweza ikatoweka kabisa ikabakia ya mdomoni tu. Ila ile ya matendo inakuwa haipo tena mpaka pale utakapoamua kuchukua hatua tena.

Kusema napenda kusoma Neno la Mungu kwa maneno matupu pasipo matendo yeyote, hakuwezi kubadilisha lolote, cha msingi ni kuchochea hamu yako zaidi kwa kuanza leo kusoma Neno la Mungu.

Kusoma Neno la Mungu kuna kupa kufunguka zaidi kuliko unavyozidi kukaa ukitamani upate muda mzuri wa kuanza. Kama unasoma Neno la Mungu angalia hili ninalokuambia hapa, utaona ni kweli kabisa jinsi unavyozidi kujifunza ndivyo unavyozidi kufunguka zaidi.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, hata hapa umekuwa na hamu ya kupata jumbe kama hizi kwa sababu umeona kuna vitu vizuri unapata ndivyo ilivyo na Neno la Mungu.

Nakutakia siku njema.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081