Haleluya, nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai. Namshukuru Mungu naendelea vyema kabisa sijui wewe ndugu yangu, nakusihiusiache bidii yako kwa mambo ya Mungu hata kama unapita mahali fulani pagumu.

Leo nichukue nafasi hii kukupongeza wewe uliyeamua kutoa muda wako kusoma Neno la Mungu, ni faida kwako ila nimeona ni vyema nikupogeza kwa juhudi hizo.

Najua ukijitazama ulivyoanza na ulivyo sasa unaona hatua kubwa sana, pia unapaswa kumshukuru Mungu kwa hatua uliyonayo. Maana kuna watu mlianza nao vizuri ila waliishia njiani.

Upo hapo kwa sababu ya juhudi zako za kutokubali madhaifu fulani yakurudishe nyuma. Na utaendelea kukua zaidi katika usomaji wako wa Neno la Mungu usiporuhusu udhaifu wowote ukurudishe nyuma.

Wewe ni mshindi sasa, kwa kuwa umeshinda ule udhaifu wa wengine ambao bado wanao, wanaojiahidi kila siku wataanza kesho. Usiache kuwaombea ili waone hawapaswi kukaa bila kusoma Neno la Mungu. Kitu kingine hupaswi kunyamaza kuwaambia marafiki zako umhimu wa kusoma Neno la Mungu.

Itakuwa rahisi kwako na kwao, kama wataona hilo Neno la Mungu limekubadilisha wewe mwenyewe. Usiache kuwashuhudia uzuri wa Neno la Mungu, kwa sababu tayari unao mwanga wa kutosha kuhusu umhimu wa kusoma Neno la Mungu.

Usisubiri upate kikubwa sana ndio uje uanze kushuhudia wenzako, kile kidogo ulichokipata uwe mwaminifu kuwagawia wenzako. Unapowapa faida ya kusoma Neno la Mungu, unapanda vitu ndani yao, hata wasipofanya utekelezaji leo ipo siku watasema fulani alinisaidia sana.

Pongezi zangu zimfikie kila mmoja anayesoma ujumbe, haijalishi mazingira unayopambana nayo sasa naamini hata kama ulianza kupunguza ile kasi ya usomaji wako wa Neno la Mungu. Unaenda kuinuka tena na kasi nyingine mpya, maana juhudi yako inatambulika mbele za Mungu.

Na wewe ambaye unaendelea kujiambia utaanza kusoma Neno la Mungu, lakini huanzi chochote unapaswa kukaa chini ujue cha kufanya. Mwisho uwe na hitimisho la kuanza sasa na sio kesho, wenzako hawasubiri wapate kazi, mume, mke ndio waanze kusoma, wenzako hawasubiri wawe mazingira mazuri ndio waanze kusoma. Humohumo kwenye ugumu wanaendelea kupambana na wanapenya.

Mkulima wa kweli hachugui jembe kama wasemavyo walimwengu, na wewe usichague mazingira. Ulipo panatosha kabisa kuendelea na ratiba zako za usomaji wako wa Neno la Mungu. Hutokaa upungikiwe na kitu chochote zaidi sana utakuwa umeongeza kitu kikubwa sana ndani ya moyo wako.

Tamani kuwa sababu za wengine kujenga mahusiano mazuri na Mungu kupitia wewe, pale utakapokuwa na ratiba za usomaji wako wa Neno la Mungu. Kuna mtu mmoja unamsaidia kati ya hao wanaokuzunguka, iwe ofisini kwako, iwe eneo la biashara yako, iwe jirani yako, iwe kanisani au kwenye kikundi chochote kile. Amini kuna mbegu unapanda ndani ya mioyo yao.

Si umewahi kupita sehemu huna habari kabisa na bidhaa fulani au kuna mtu amewahi kukupitishia bidhaa fulani anauza. Unakuwa huna shida nacho kabisa wakati huo, ila ipo siku inafika unahitaji hicho kitu unakumbuka na kuanza kumtafuta muuzaji kwa bidii. Ndivyo ilivyo kwenye neno la Mungu, kwa sasa wanaweza wakawa kama hawaoni umhimu wa kusoma biblia, ila watakukumbuka siku moja uwape mbinu za kusoma.

Nisikuchoshe sana na maneno mengi, ila nikushauri kwamba usije ukakata tamaa kwa namna yeyote ile. Jambo lingine la msingi sana usije ukalewa sifa, ukajaa kiburi na kuona umeweza sana. Ukijiona hivyo ni bora kukemea hiyo hali mapema kabla haijakuangusha chini.

Mungu akubariki sana kwa muda wako, endelea kutembelea tovuti yetu www.chapeotz.com kwa masomo mengine mazuri zaidi ya kukujenga katika usomaji wako wa biblia.

Nakutakia wakati mwema.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Tovuti: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.