Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, nafasi nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuonana tena. Tukaitumie nafasi hii kumzalia Mungu matunda yaliyo mema, na itakuwa hivyo kama tutambua nafasi zetu.

Kuna tatizo linatusumbua tulio wengi, huenda hatujui kama ni tatizo ila linavyozidi kwenda litaonekana ni kitu cha kawaida kabisa. Wakati sio jambo la kawaida kabisa, ni tabia inayotokana na mapokeo ya dini/madhehebu yetu.

Wakati mwingine tunataka kuyakataa maandiko matakatifu tukifikiri ni mafundisho ya kanisa fulani au tukifikiri ni mwongozo wa kanisa fulani. Sababu haswa inayotufanya tufikiri hivyo, ni vile tu kilichozungumzwa ndani ya biblia kinapingana na kile tunaamini sisi au tulichoaminishwa sisi.

Tunaweza kujipa moyo kuwa madhehebu yetu ni bora zaidi kuliko madhehebu mingine, tukabaki tunajivunia dhehebu/dini tukaacha kumhubiri Yesu Kristo. Tukawa tunahubiriana dini zetu au madhehebu yetu, na kila mmoja akawa anavutia upande wake kwa kadri akatavyoweza.

Nguvu inayotumika kutetea madhehebu yetu au dini zetu, inaweza isifikie ile ya kumtangaza Yesu Kristo. Ambalo ni agizo la kila mmoja wetu, tumesahau hili kabisa na kubaki kutupiana lawama, kanisa fulani lipo hivi na lingine lipo vile.

Tusipokuwa makini, tutakuwa na vituo vingi vya makanisa/madhehebu vinavyojadili wenzao. Na kusahau kabisa kusudi la wao kukusanyika pamoja.

Kweli hatuwezi kunyamaza kimya tunapoona hali fulani ya upotoshaji wa Neno la Mungu ipo katika dhehebu/dini fulani. Lazima tutakemea na kuelezana ukweli, ila sio agenda ya kuifanya ndio sehemu ya ibada zetu kila siku.

Nasikitika kukuambia hilo dhehebu/dini yako, halijaandikwa kwenye biblia yako. Tafuta Kuanzia mwanzo mpaka Ufunuo uone kama utakutana na kanisa la KKKT, FPCT, EAGT, TAG, KLPT, RC… na mengine mengi unayoyafahamu wewe. Hutopata kamwe, ni majina tu tunayoyatunga sisi wanadamu katika kuyatambulisha makusanyiko yetu.

Usije ukaona dhehebu lako lipo sahihi kuliko Neno la Mungu, kama kuna kitu ambacho kinaelezwa na biblia yako. Haijalishi dhehebu lako linapingana nalo, ukweli utabaki pale pale mnachoendana nacho sio sahihi au mnachoendana nacho ni sahihi.

Neno la Mungu linapaswa kuwa kiongozi wetu na sio sisi tunapaswa kuliongoza neno la Mungu. Maana wakati mwingine dini zetu zinatukolea moyoni kiasi kwamba tunaona Neno la Mungu limekosewa kuandikwa. Yaani unaona dini yako ni bora zaidi kuliko Neno la Mungu!!

Ili uweze kulielewa Neno la Mungu, na ili uwe salama kuepuka mahangaiko ya moyo wako, na ili uwe salama kuepuka kupingana na Neno la Mungu. Hakikisha unaweka mapokeo ya dini/dhehebu lako pembeni, haijalishi mazingira unayosali ni mazuri kiasi gani. Hilo lisikupe shida, hakikisha unajiachia mbele za Mungu na kumruhusu Roho Mtakatifu afanye kazi yake.

Sikuelezi haya ili uanze kudharau wachungaji wako, sikuambii haya uanze kudharau dhehebu/dini yako. Nakueleza haya ili usilione Neno la Mungu kama unavyoliona dhehebu/dini yako, Neno la Mungu ni mwongozo wa kila mwanadamu aliyelikiri jina la Yesu Kristo. Hata kama mchungaji wako au kanisa lako litatunga biblia yenu pake yenu, bado Biblia ya kweli itakuwepo na kuipoteza hamtaweza.

Jenga twasira mpya kabisa ndani yako kama ulikuwa na twasira ya kuiona biblia kama adui wa dhehebu lako. Ujue ulikuwa unasoma biblia kwa kupoteza muda wako, ujue ulikuwa unakosea sana kuwaza biblia imekosewa.

Ukifika mahali ukaiona biblia ni mwongozo wa kila mkristo yeyote yule, utaanza kuielewa unapoisoma. Wakati mwingine unashindwa kuisoma na kuielewa biblia kwa sababu umeweka misingi ya dini yako isiyoweza kubombolewa na Neno la Mungu.

Jiepushe na mtego huo, mimi sikuambii haya ili uje kwenye kanisa langu. Mi sina kanisa na wala sikuambii haya uje ninaposali, kwanza sitaki ujue nasali wapi na sina uhakika kama umewahi kuniona najivunia dini/dhehebu langu. Siku zote nimekuwa najivunia kumpata Yesu Kristo, aliyenikoa kwenye utumwa wa dhambi.

Ninachotaka hapa kukujengea wewe ni uwezo wa kuliona Neno la Mungu kama kitu cha thamani kubwa isiyoweza kulinganishwa na dhehebu/dini yako. Wengi wamekamatiwa kwenye dini, ndio maana ukimweleza habari za Yesu Kristo yupo tayari kukushikia silaha akumalize.

Hadi hapo naamini kuna kitu umejifunza, ninachokuomba ni kuhakikisha unaelewa umhimu wa Neno la Mungu katika maisha yako. Chunga sana hili, acha kupuuza Neno la Mungu kwa sababu linapingana na dhehebu/dini yako. Bora Neno la Mungu lipingane na dini yako, kuliko dini yako kupingana na Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako, endelea kutafakari zaidi haya niliyokueleza hapa. Kipo kitu kizuri kitaenda kujengeka kwako na kuondoa kile kisichostahili kukaa ndani yako.

Nakutakia siku njema.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Tovuti: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.