Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai. Siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona, sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.
Tunaweza kujikuta tupo njia panda kwenye maeneo mengi sana katika maisha yetu, na tukishaingia kwenye mambo mengine na kuachana na yale yaliyotuweka njia panda. Sio kwamba tunakuwa tumepata mwafaka wa hayo mambo, wakati mwingine tunaachia hapo.
Utatuzi mwingine unaweza kufikiri unahitaji msaada kutoka kwa wengine, ila na wao wanakuwa hawajui hilo unalotaka utatuliwe ili utoke kwenye utata. Ambapo matokeo yake yanaweza kuwa mazuri, na wakati yasiwe mazuri.
Unapokuwa unahitaji msaada fulani alafu ukakosa jibu la uhakika la ufanye nini na usifanye nini, unakuwa unashindwa kupata mwelekeo mzuri. Badala yake unaweza kufanya lisilotakiwa kufanywa kwa kufikiri linatakiwa ulifanywe au ukaacha kufanya linatakiwa kufanywa kwa kuogopa kukosea kumbe ulikuwa sahihi.
Najua hili huwezi kunikatalia, najua kila mmoja wetu ana maswali mengi ambayo mengine yanamweka njia panda. Akijaribu kuuliza sehemu anazoona anaweza kupata majibu, majibu anapata ila sio kwa kiwango ambacho alitamani kupata majibu yale. Bado shida yake inarudi pale pale ametolewa nusu kwenye utata wake na nusu nyingine imeachwa ndani yake.
Pamoja na changamoto zote hizo, kipo kitabu chenye majibu ya kila kitu, hichi kitabu kimebeba kila kitu cha maisha yako. Yawe maisha ya kimwili kimeweka vizuri na yawe maisha ya kiroho nayo yamewekwa vizuri.
Unaweza kuwa na utata na jambo ambalo hakuna mtu aliyewahi kufikiri hilo, na inaweza kutokea unayemuuliza naye hajawahi kupitia hilo, na anaweza kuwa hana maarifa ya kutosha kuhusu hilo unalomuuliza linalokupa utata wewe.
Nikupe tahadhari hapa, huyo unayemwona yupo vizuri kiroho na ana viwango fulani vya juu. Usije ukashangaa akashindwa kukujibu vizuri kile kinakuweka njia panda, kutokujibu vizuri kama ulivyotarajia. Haimfanyi kuwa hayupo vizuri kiroho, kinachoangaliwa hapo ni kiwango chake cha maarifa anayojaza moyoni mwake.
Wote tunajua tuna uvivu mkubwa wa kutosoma Neno la Mungu, Neno la Mungu ndilo lina maarifa sahihi kwa jambo lolote lile linalokupa utata sasa hivi na lililokupa utata siku za nyuma. Haijalishi ulipo hujui ufanye nini na usifanye nini, hayo yote dawa yake ipo ndani ya Neno la Mungu.
Tahadhari nyingine unayopaswa kuwa nayo ili uwe na bidii zaidi, unaweza kujifunza kitu kikubwa sana usijue kama umejifunza kitu kikubwa. Kinachokufanya uwe hivyo ni vile ulikuwa huna kazi nacho hicho ulichojifunza, inafika wakati unapaswa uyatumie yale maarifa unakuwa hukumbuki tena.
Tunarudi kwenye msingi wetu, kujifunza ni kila siku, unaweza usiwe na uhitaji wa jambo fulani leo. Ila kesho litakusaidia vizuri kabisa na ukawa na jibu sahihi la ufanye nini na usifanye nini.
Yapo mambo huwezi kusubiri ukamuulize fulani baadaye, badala yake utahitaji kutoa maamzi pale pale. Ndio pale tunapojikuta hatujui tufanye lipi na tusifanye lipi.
Ufanye nini kujitoa kwenye utata huu? Cha kufanya ni kujitoa kwa namna yeyote ile kuwa na ratiba ya kusoma Neno la Mungu. Ni jambo linaloonekana la kipuuzi kwa wengi ila nielewe ninachokuambia hapa, biblia imebeba kila kitu cha maisha yako.
Ukiifanya biblia kuwa rafiki yako, hata ile hali ya kusinzia ukianza kusoma inatoweka kabisa, unabaki uchovu wa kawaida ambao ukijiona umechoka sana ukapata muda wa kupumzika, unakuwa vizuri kabisa. Hayo yote yanakuja baada ya kupitia changamoto mbalimbali katika kujizoeza tabia mpya ya kusoma Neno la Mungu.
Wewe ambaye hujawahi kabisa kusoma Neno la Mungu au umewahi kusoma ukafika mahali ukaacha, unaweza kuona ninachozungumza hapa hakina ukweli wowote. Ila kwa yule aliyeweka nidhamu katika hili la kusoma biblia atakuwa shahidi wa haya ninayosema hapa. Yapo mambo mengi yalikuwa yanamweka njia panda(utata) ila baada ya kuanza kusoma Neno la Mungu ameanza kupunguza mzigo ndani yake.
Itapendeza sana kama utalishika hili leo, kuondoka kwenye utata wa ufanye nini na usifanye nini kwa jambo linalohitaji maarifa ya Mungu. Vizuri sana ukalitazama Neno la Mungu kwa sura ya tofauti, kama ulikuwa unalichukulia kawaida, kuanzia sasa lichukulie ni kitu cha thamani kubwa sana.
Ufanye nini na usifanye nini, yote yanapatikana kwenye Neno la Mungu. Hili limebeba maisha yako kwa pande zote mbili yaani maisha ya kimwili na kiroho. Ambapo hakuna kitabu kinaweza kueleza kwa usahihi kwa yote mawili isipokuwa biblia pekee iliyobeba Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Tovuti: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.