Haleluya,
Moja ya swali linalowatesa wengi bila majibu yeyote, ni hili la kupata kibali mbele za watu na mbele ya Mungu. Wengi tunafikiri tukiokoka tunakuwa na kibali upande mmoja tu wa Mungu, na wengine tunafikiri tunapaswa kukubalika upande wa wanadamu tu.
Kwa upande mmoja tunaweza kusema ni kweli, kutokana na unapotangaza kuokoka, utapoteza marafiki wengi mliokuwa nao pamoja kwenye maeneo mabaya ya kumkosea Mungu.
Unaweza kupoteza uhusiano wako na wazazi wako, ndugu zako, rafiki zako, jamii yote inayokuzunguka. Ikiwa tu ulikuwa upande wao wa kuabudu miungu mingine, pale ulipofika wakati ukasema imetosha kuabudu miungu ya mababu na mabibi, ukaanza kumwabudu Mungu wa kweli.
Unapofikia hatua hiyo, ujue utakosa kibali kwa hao mliokuwa pamoja kwenye imani hiyo ya kuabudu miungu mingine. Lakini pamoja na kukosa ushirikiano na watu wanaomkataa Mungu wa kweli na kuabudu miungu mingine, uwe na uhakika Bwana atakuinulia marafiki sahihi na wengi zaidi ya hao.
Kukubalika mbele za watu huku matendo yako yanamkataa Mungu wa kweli, uwe na uhakika unakubalika na watu walioharibiwa mioyo yao na fahamu zao na shetani. Huwezi kukubalika na watu wa dunia alafu ukaacha kukubalika na watu wa Mungu. Mtu wa Mungu anayelijua Neno la Mungu vizuri atakubalika na upande ulio sahihi na kutumika kubadilisha upande usio sahihi, hata kama itachukua Muda.
Kukubalika pande zote mbili yaani mbele za wanadamu na mbele ya Mungu, inahitaji uwe na Mungu wa kweli ndani yako na unahitaji upate elimu/maarifavideo ya Mungu. Elimu itakayokusaidia kufanyika baraka mbele za Mungu na mbele za watu wake.
Tunaona watu wanaenda kwa waganga wa kienyeji kutafuta dawa ya kukubalika na watu, wanaweza kupata msaada kweli ila wanakuwa wanakubalika na wanadamu tu, ila mbele za Mungu wanakuwa hawana kibali kabisa.
Kutokubalika mbele za watu sio jambo la kufurahisha sana hasa ukiwa umempokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako. Najua umewahi kuona watumishi wengine wanakuwa na kibali sana mbele za watu, wakiitisha jambo wanakusanya watu wengi sana. Watu wale wale wakiitwa sehemu na mtumishi mwingine wanakuwa hawafiki kabisa.
Najua umewahi kuona kanisani baadhi ya washirika wana kibali sana mbele za watu, sio kwa sababu wana mali nyingi, ni vile tu wanampenda Yesu Kristo na kulishika Neno lake katika roho na kweli. Unaweza kusema mbona kuna wapo wanampenda sana Mungu ila hawana kibali mbele za Mungu, swali lako ni la msingi sana na majibu yake utayapata hapa hapa.
Hatuokoki ili tupate kukubalika na wanadamu, unaweza kuokoka kwa sura ile ya kutafuta kukubalika na wanadamu ukaja kukutana na chuki za ajabu. Mwisho ukaona wokovu ni mgumu sana na ukaanza kutamani kurudi kwenye maisha yako ya uchafu.
Tunapookoka tunapata Neema ya kukubalika mbele za wanadamu na mbele ya Mungu, hii ni zawadi kwa mwana wa Mungu aliyemwamini Yesu Kristo, ikiwa tu ataokoka kweli. Maana wapo watu ni mguu ndani na mguu mwingine nje, dunia wanaipenda na mambo yake mabaya na wokovu wanaupenda na mambo yake mazuri. Huo mchanganyo hukubaliki mbele za Mungu.
Ili uweze kukubalika mbele za Mungu na mbele ya wanadamu, unapaswa kulishika Neno la Mungu na kuliweka moyoni mwako. Utalishikaje? Ni kwa kulisoma na kulitafakari, na kulitii, na kulifuata, na kuliweka katika matendo yako. Hapo ndipo utaona maisha yako ya kiroho na kimwili yakiwa salama.
Maisha yako yakiwa safi mbele za Mungu, yeye ndiye atakufanya uwe barua njema inayotazamwa na kila anayeamini na asiyeamini. Kibali chako kwa wanadamu, kitatolewa na yeye, sio kwa lazima wanadamu watakupenda, ni kwa hiari yao wenyewe. Matendo yako yatawafanya watu waanza kutamka maneno ya baraka mbele za Mungu.
Utasikia ana heri aliyemzaa kaka huyu, dada huyu, mama huyu, na baba huyu. Utakasikia tumbo lililomzaa baba, mama, kaka, dada huyu limebarikiwa sana. Kila mmoja atatamani kuitwa mtoto wa fulani, kila mmoja atatamani kutumia jina lako akifikiri atakuwa kama wewe, kila mmoja atatamani kuita mtoto wake jina lako akijua naye atakuwa vile ulivyo wewe.
Siri ni moja tu, kulishika Neno la Mungu na kuliishi siku zote za maisha yako, ukilishika Neno la Mungu hutokuwa mlevi, mwasherati, mzinzi, mwizi, mla rushwa, muongo, tapeli na mengine mengi mabaya.
Rejea: Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu. MITHALI 3:3-4 SUV.
Haleluya, kumbe huwi na kibali tu mbele za Mungu na mbele ya wanadamu, unakuwa na akili nzuri zinazoweza kuwa msaada kwa wengine na ukazidi kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.
Kuanzia leo chagua kuijaza kweli ya Mungu ambayo ni Neno la Mungu, utaona kukubalika mbele za Mungu na mbele ya wanadamu. Mungu sio muongo, Neno lake ni kweli kabisa, we jaribu utaona unavyopata vibali mbele ya wanadamu na mbele za Mungu.
Achana kabisa na habari ya kutafuta kukubalika na wanadamu tu, alafu ukawa huna kibali mbele za Mungu, hiyo ni hatari kubwa sana kwako. Kukubalika iliyo sahihi ni ile kuishika kweli ya Mungu, uhusiano wako mzuri mbele za Mungu kutakupa kukubalika mbele ya wanadamu.
Kila utakaposimama mbele za watu kuzungumza, watu watatamani uongee mpaka asubuhi maana kuna vitu vizuri Mungu amewekeza ndani yako. Hii inakuja tu unapoikubali kweli ya Mungu iwe ndani yako, na uishi vile Neno la Mungu linakuelekeza.
Utaijuaje sasa kweli? Ni kwa kusoma Neno la Mungu, unaweza kuwa umeokoka miaka mingi sana. Ila ukijitazama unajiona kabisa huna kibali mbele za watu, unaweza kusimama wakati mwingine watu wanakuzomea, unaweza kusimama kuongea mbele ya watu wanainamisha vichwa badala ya kukutazama. Hapo ujue uhusiano wako na Mungu sio mzuri kabisa japo kuwa umeokoka.
Nakusihi sana ulishike sana Neno la Mungu, utalishika kwa kulisoma, zaidi ya hapo ni kujidanganya ndugu yangu. Moyo wako wote uwe kwenye Neno la Mungu, utaanza kuona mabadiliko makubwa sana katika maisha yako ya wokovu.
Mungu akusaidie kufahamu haya.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Tovuti: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081