Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie Bwana wetu Yesu Kristo, kwa wema wake mkuu kwetu.

Maarifa ni mazuri sana maana yanamtoa mtu kwenye ujinga na kumpeleka eneo la ufahamu, ndipo anapojua mahali alipokuwa hapakuwa sahihi kwake. Wakati hajaelimika, aliona yupo sawa tu.

Kadri mtu anavyozidi kuelimika kwenye jambo fulani, ndivyo uwezakano wa kudanganywa unapungua, ndivyo uwezakano wa kukosea sana inapungua kabisa kwake.

Maarifa ni mazuri sana, yanakupa mwanga wa kufanya kazi zako kwa ufanisi, yanakupa mwanga wa kuenenda katika njia sahihi, yanakupa uwezo wa kuwaongoza watu vizuri, yanakupa kujali familia yako, yanakupa moyo wa kuwalea watoto wako katika maadili mazuri.

Maarifa kadri yanavyoongezeka ndani mwa mtu, hata zile tabia za ajabu ajabu zilizomvaa mtu ndani yake zinatoweka kabisa. Ikiwa tu mtu yule atayashika yale anayojifunza na kuyafanyia kazi kwa vitendo.

Inafika mahali mtu huyu mwenye bidii ya kuyajaza maarifa ndani yake, anakuwa kwenye kiwango fulani cha juu sana. Kiwango hichi cha juu kimeletwa na jinsi anavyojituma kutafuta maarifa sahihi ya kumjenga katika kile anatamani awe imara.

Mlango ule ule aliotumia mpaka kufikia kufanikiwa kwake, Shetani anautumia kumjaza kiburi. Badala ya mafanikio aliyoyapata yawe chachu ya yeye kwenda mbele zaidi, anaona amefika kiwango cha juu sana hahitaji tena kujifunza kitu kingine.

Sifa ya kiburi ilimfanya Malaika Lusifa kushushwa mbinguni, alijiona na yeye anastahili kupewa heshima ya Mungu. Akasahau kiwango alichokuwa nacho kimetokana na huyo anayeitaka nafasi yake.

Wengi wanasahau haraka viwango walivyonavyo walipaswa kunyenyekea zaidi mbele za Mungu. Ili Mungu aendelee kuwafunza zaidi mambo mengine wasiyoyajua, badala yake wanaikosa hiyo fursa kutokana na kujaa kiburi cha kujiona wametosheka.

Ugonjwa huu unawakumba wengi wanaosoma Neno la Mungu, mtu akifanikiwa kusoma kitabu cha Mwanzo hadi Ufunuo wa Yohana. Anajiona amefika mwisho wa mambo yote, anajiona ametosheka na hahitaji kujifunza zaidi kadri siku zinavyozidi kwenda mbele.

Unakuta hata yake machache waliyoyapata, wanafika mahali wanayasahau kabisa kwenye kumbukumbu zao. Wanabaki kusimlia wamesoma biblia nzima ila ule uhalisia wa mtu aliyesoma Neno la Mungu alafu likamjenga na kumwimarisha. Unakuwa haupo kwenye matendo ya nje.

Kupata maarifa sahihi na mengi zaidi, hakuwezi kukufanya ukajiona umetosheka. Kadri unavyozidi kujifunza ndivyo uwezakano wa kutamani kujifunza zaidi unakuwa mkubwa zaidi.

Hakuna kutosheka Neno la Mungu, haijalishi umesoma biblia yote zaidi ya mara 5. Bado utasikia kiu ya kusoma Neno la Mungu, maana ndani yako unasikia kufunguka zaidi kadri unavyozidi kujaza maarifa ya Neno la Mungu.

Wale wachanga wa kiroho wakishasoma mara moja au mbili, wakamaliza biblia nzima wanajiona tayari wamemaliza kila kitu. Fanya hivyo kwenye vitabu vingine ila sio kwenye neno la Mungu.

Hakuna siku utakula chakula kizuri sana cha tumbo, ukashiba wiki nzima au ukajiona huhitaji kula tena. Haijawahi kutokea hata siku moja, ndivyo haitatokea kwenye chakula cha kiroho ambacho ni Neno la Mungu.

Ukishaona umeanza kujaa kiburi na hicho kiburi kikakufanya unakuwa mzembe wa kusoma Neno la Mungu, ujue kuna roho imekuvaa. Utajua pale utakapochoka zaidi, ila kwa sasa utajiona upo sahihi kufikiri umetosheka kujifunza Neno la Mungu.

Neno la Mungu lifanye chakula chako, najua hujawahi kufika mahali ukasema nimekula sana chakula miaka mingi ngoja nipumzike mwaka mmoja. Kama haiwezekani, jua na kwenye Neno la Mungu ni zaidi ya chakula cha mwili.

Kiburi kikae mbali nawe, nyenyekea mbele za Mungu ili aendelee kukupika zaidi uive. Bidii ile ile uliyokuwa nayo mpaka ikakufikisha mahali ukajiona una afadhali, isipungue kabisa bali ikaongezeke zaidi.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Tovuti: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.