Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona. Tukaitumie vyema siku ya leo ili kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.

Yapo mahangaiko tunayapata kutokana na mambo mbalimbali tunayokutana nayo katika maisha yetu ya kila siku. Wengi tunapopatwa na changamoto ngumu huwa tunashindwa kuhimili yale mahangaiko ya moyo. Badala yake tunaanza kufanya vitu vingine visivyompendeza Mungu au wakati mwingine tunaacha kutoa huduma au tunaacha ile bidii yetu ya ibada.

Tunaweza kusema tumesamehe, ila ndani mwetu tunaona kabisa hakuna utulivu mzuri kutokana na jambo lililotupata. Wengine wanakuwa kama wamerukwa na akili zao, ambapo linakuwa kama tatizo lake la kila siku.

Ukweli ni kwamba lazima upate mfadhaiko wa moyo wako unapopatwa na jambo usilolitegemea. Ila mfadhaiko huo hupaswi kuwa hivyo ndani yako kwa muda mrefu, unapokaa kwa muda mrefu unakupotezea mwelekeo wako wa kufanya mambo ya msingi kwa ufanisi.

Unapojiona una hali ya mahangaiko ndani yako kwa muda mrefu, ikafika mahali ukaona Mungu hayupo au ukaona Mungu hakusikii maombi yako au ukakosa kabisa imani kwa Mungu wako. Fahamu kwamba unasumbuliwa na uchanga wa kiroho, uchanga ambao hutolewi na maombi tu bali kwa Neno la Mungu.

Mambo mengi sana yanatawala mioyo yetu kwa kiasi kikubwa, sababu haswa ni kukosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu. Unaweza kusema ni hali tu ya kawaida, nakwambia haiwezi kuwa ya kawaida ndio maana imedumu ndani yako kwa muda mrefu sana. Tena umefika mahali umeona Mungu hasikii maombi yako.

Kwanini Neno la Mungu? Unapopatwa na msukosuko wowote, uwe wa kibinafsi, uwe wa kifamilia, uwe wa kijamii, uwe wa kitaifa. Neno la Mungu litakukumbusha au litakupeleka moja kwa moja kwenye mstari/mlango unaoleza vizuri hali inayokupata/inayokutokea/unayopitia wakati huo.

Hutohitaji kuwaomba watu mistari ya kujua hali yako unayopitia imeandikwa wapi, utajionea mwenyewe ndani ya moyo wako. Tena inakupa nafasi zaidi ya kumtafakari Mungu na kukupa ufahamu wa kuelewa majira na nyakati unazopitia, nazo ipo siku zitapita.

Neno la Mungu linaondoa kabisa vishawishi vibaya wakati huna utulivu mzuri wa kuumizwa na jambo fulani. Maana shetani anaweza kumtumia mtu wake, akakusahauri jambo la ajabu ambalo linamkosea kabisa Mungu wako.

Hebu amua kuchukua hatua madhubuti ya kukuwezesha kuwa na ratiba ya kusoma Neno la Mungu, acha kusikia Neno la Mungu linasaidia watu. Jaribu na wewe mwenyewe kwa kusoma, acha visigizio visivyoweza kukuvusha hapo ulipo.

Kujijengea msingi wa Neno la Mungu ni bora zaidi katika maisha yako, msingi huu utakusaidia kutokuwa na maswali mengi sana yasiyo na majibu. Msingi huu utakusaidia kusimama na Yesu wako katikati ya shida yako, msingi huu utakusaidia kusimama wewe kama wewe bila kuhitaji watu walioupande wako ni wangapi.

Bila kukubali kusoma Neno la Mungu kwa kumaanisha, utaendelea kubaki kwenye uchanga wa kiroho. Ambapo huo uchanga ndio utakaokuletea mahangaiko mengi ya moyo wako, kwa sababu umeacha jambo la msingi linaloweza kunyonya habari mbaya na kukupa ujasiri wa kusonga mbele.

Zoezi hili sio gumu sana kama unavyofikiri, ni kuamua kuchukua hatua sasa, na kama ulishachukua hatua ni kuongeza bidii zaidi. Bidii yako itakufikisha mahali utaamini maneno haya niliyokueleza leo hapa, ila kwa sasa nakusihi ufuate haya niliyokueleza.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Tovuti: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.