Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona. Fursa kwetu kwenda kumzalia Bwana matunda yaliyo mema na kutengeneza njia zetu mbaya pale tulipoenda kinyume na Mungu.

Kifaa kinachotupa mwanga wa kutosha kusafiri salama, tumefika mahali hatuoni umhimu wake vizuri wa kukitumia. Pamoja na kuhimizwa sana umhimu wa kifaa hicho, bado hatuna muda wa kukitafuta.

Tumeokoka sawa, umefanya vizuri sana kuokoka wala hujakosea kabisa, kitu kitakachokufanya uendelee kudumu katika wokovu na uendelee kufanya mapenzi ya Mungu. Na kitakachokufanya uzidi kumzalia Mungu matunda yasiyo na mapooza ni Neno la Mungu.

Neno la Mungu ndio dira nzima ya maisha yako, maisha yako ya kiroho na kimwili yanategemea sana Neno la Mungu. Jinsi ya kuenenda na kuishi maisha yampasayo mkristo aliyeokoka.

Lakini pamoja na hayo yote, bado hatuna muda kabisa wa kusoma Neno la Mungu, wala hili jambo hatulioni kama lina uzito wowote. Tusiposoma tunaona sawa, na tukisoma hatuoni tofauti yeyote kutokana na vile tunaliona Neno la Mungu.

Unaweza kujitazama mwenyewe ni jinsi gani hili suala la kusoma Neno la Mungu unavyolichukulia. Bila kuangalia wengine unaweza kuona mengi sana kwako, kama utajiona kwa sasa unalichukulia ni jambo la maana sana kwako na huwezi kumaliza siku bila kusoma Neno la Mungu. Utakuwa umefaulu na utakuwa na ruhusa ya kuwatazama wengine, pamoja na wana bidii kwa mambo mengine mazuri ya Mungu lakini wamefeli katika kusoma Neno la Mungu.

Hatuwezi kujua tuendako pasipo kuwa na njia inayotuelekeza mahali tunaenda, tunaweza kujua njia inayoweza kutupeleka ila katika njia hiyo tukawa hatujui tutashukia wapi. Lazima pawepo mahali pa kuhitimisha safari yako, bila kujua utafikia wapi utajikuta umepitiliza sehemu uliyopaswa kufikia.

Tufanye nini ili kila mmoja aelewe umhimu wa kusoma Neno la Mungu, kama Taa ya maisha yetu ya kiroho na kimwili ni Neno la Mungu. Na ukitazama asilimia kubwa ya wakristo hawana muda kabisa wa kusoma Neno la Mungu.

Wengi wetu tuna muda wa kufanya mambo mengine mazuri na makubwa, ila kwenye Neno la Mungu limeonekana ni jambo lisilo na faida kwetu. Kama jambo hili lingekuwa na faida kwetu kila aliyemkiri Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yake, angeona uzito wa kusoma Neno la Mungu.

Hatusomi huenda kutokana na kuona sio lazima sana, ni sawa na mtu anayejua afanye jambo fulani lakini hafanyi, akijua hakuna madhara yeyote atakayopata. Anavyofikiri hivyo hata ule moyo wa kujitoa kufanya jambo kwa ufanisi mkubwa unakuwa hakuna.

Hebu tuone maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu Neno la Mungu, huenda nakueleza haya unaona hayapo kabisa;

Rejea: Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu. Zaburi 119:105 SUV.

Neno la Mungu ni taa ya maisha yako ya kiroho na kimwili, na ndio linalomlika maisha yako yote. Ndio linaloweza kukufanya ukaishi maisha safi ya kumpendeza Mungu wako, na unakuwa na uhakika wa maisha unayoishi sasa yanampendeza Mungu au hayampendezi Mungu.

Zipo dhambi zingine sio maarufu kama kuzini, uasherati, ulevi. Kama huna Neno la Mungu unaweza usijue kama unamkosea Mungu, ila ukiwa na Neno la Mungu ndani yako na ukaendelea kujikumbusha kila siku. Inakuwa rahisi kwako kujua njia unayoifuata bado uko sahihi au umekosea mahali.

Labda mfano rahisi tunaweza kusema hivi, Taa ya mwili ni jicho, pasipo jicho mwili unapata shida, miguu haiwezi kuwa na uhakika mahali inapoelekea. Maana taa inayofanya uone njia na kutembea kwa kujiamini ni jicho/macho.

Rejea: Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote unao mwanga; lakini likiwa bovu, mwili wako nao una giza. Luka 11:34 SUV.

Haya ndugu, husomi Neno la Mungu maisha yako yatakuwaje safi? Sio mimi nasema haya maneno, Neno linasema jicho lako likiwa safi na mwili wako wote unao mwanga, na likiwa bovu, mwili nao unakuwa giza.

Na mwanzo tuliona taa ya miguu yetu ni Neno, husomi sasa Neno la Mungu, maisha yako yatakuwa na hali gani Ndugu yangu. Hebu we kaa ufikiri mwenyewe, nimejaribu kukupitisha kwenye maandiko matakatifu ili uweze kuona uzito wa hili jambo.

Huenda hapo ulipo unajiona sio kipofu, ila kwa mjibu wa maandiko matakatifu, kama husomi Neno la Mungu wewe ni kipofu. Naona unakataa Kabisa, naomba nikurudishe kwenye andiko hili;

Rejea:Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu. Zaburi 119:105 SUV.

Umeona hapo, tena maandiko mengine matakatifu yakaeleza kwa uwazi kabisa pasipo Neno la Mungu ni sawa na kipofu.

Rejea:Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote unao mwanga; lakini likiwa bovu, mwili wako nao una giza. Luka 11:34 SUV.

Mungu akusaidie kufahamu haya niliyokueleza hapa, Mungu afungue ufahamu wako uweze kuona uzito wa hili jambo.

Mungu akubariki kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Tovuti: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.