Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona tena. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, maana wapo walitamani kuiona leo ila hawakuweza.
Kabla ya yote, nina kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa uweza wake. Tangu tumeanza kitabu cha Zaburi na timu nzima ya Chapeo Ya Wokovu whatsApp group, kuanzia sura ya kwanza mpaka siku ya jana tumehitimisha sura 150.
Unaweza kuona ni sura nyingi sana, ila tumekuwa tukisoma sura moja au sura mbili au sura tatu, kutokana na jinsi sura zilivyokaa. Maana zipo sura zimebeba mistari mifupi sana, tulikuwa tunatumia fursa hiyo kusoma sura zaidi ya moja.
Lengo letu kubwa sio kutaka kuonekana tunasoma tu, lengo letu tunapenda kusoma na kupata muda wa kutafakari zaidi yale tuliyoyasoma. Na tumeona mafanikio makubwa sana katika hili, ndio maana hatukuona shida kusoma Zaburi 1 hadi 150, tena hatua kwa hatua.
Wewe ambaye ulikuwa unaona kusoma Neno la Mungu ni mtihani mgumu sana, utakuwa umeanza kupata picha fulani kichwani mwako. Kweli kabisa kwa hali ya kawaida unaweza kuona kuanza kitabu cha Mwanzo hadi kufikia kitabu cha Ufunuo, ukaona inaweza isiwezekane, ila mimi nakuhakishia inawezekana.
Kwanza kubali kujiondoa kwenye makundi yasiyohusisha kabisa na usomaji wa Neno la Mungu, pili usiwaeleze mpango wako wa kusoma Neno la Mungu subirib waje wajionee wenyewe kwa vitendo. Tatu usisumbuliwe na ujazo/ukubwa wa biblia, anza na hatua hiyo hiyo uliyonayo. Nne usitake kuelewa kila kitu kwa wakati mmoja, mshukuru Mungu kwa kile kidogo unachokielewa na kadri unavyozidi kujifunza ndivyo na ufahamu wako unazidi kufunguka zaidi.
Mwanzo nilianza na kumshukuru Mungu kutuwedhesha kumaliza kitabu cha Zaburi kuanzia sura 1 hadi 150, tukiwa tumejifunza mengi sana. Unaweza kufikiri tumeanzia Zaburi tu, tumeanzia kitabu cha Mwanzo tukaenda kidogo kidogo hadi leo tumemaliza Zaburi. Hiyo ni agano la kale, agano jipya napo ni vivyo hivyo tumemaliza Mathayo hadi Ufunuo wa Yohana.
Usije ukafikiri tulianza kwa kusoma sura nyingi sana, tena kabla ya kufika kitabu cha Zaburi. Tulikuwa tunasoma sura moja tu ya kitabu kila siku, usishangae! Ndio ni sura moja tu tumeanza tangu mwaka 2015 hadi leo 2017. Kwa jinsi tulivyozungukwa na watu wasiojishughulisha na kusoma Neno la Mungu unaweza kuona ni jinsi gani tumepita katika mapito mengi na magumu sana.
Wengi walianza lakini wakarudi nyuma, na wale walioamua kujitoa kweli, leo wanafurahia matunda ya juhudi zao maana hawakukubali kukatishwa tamaa na jambo lolote. Ambapo na kwako inawezekana kabisa ukaanza kuwa msomaji mzuri wa biblia pasipo kulazimishwa na mtu yeyote.
Zoezi hili linahitaji usisikilize kelele zozote za watu wasiopenda kusoma Neno la Mungu, na hata kama wanapenda kama hawachukui hatua zozote za kusoma. Hao huwezi kusema wanapenda, maana kupenda kitu ambacho una uwezo nacho ila huchukui hatua zozote, huo upendo pasipo matendo sio kitu.
Unajisikia moyoni mwako kuanza kusoma Neno la Mungu, asikutishe mtu yeyote wala usijitishe wewe mwenyewe. Anzia hapo hapo, hata kama hutaanza kwa mtiririko tuliotoka nao sisi, unaweza kuanzia popote mpaka mwisho wa siku unakuja kujikuta umezunguka na kufikia mahali ulianzia.
Leo tunaanza kusoma kitabu cha Mithali 1, tutaenda na hii safari hadi tukapomaliza kitabu cha Mithali. Kwa wewe ambaye hujaanza unaweza kuona ni ngumu sana, lakini ukianza leo hutoona ugumu wowote. Ugumu unausababisha mwenyewe kutokana na jinsi unavyofikiri wewe, nakuambia hivyo kwa sababu wenzako wameweza na wewe ushindwe una nini? Amini unaweza.
Unatamani kuanza kusoma Neno la Mungu ila bado hujaweza kuwa na nidhamu binafsi, nakukaribisha kwenye group la whatsApp. Utakutana na kanuni zinazokubana kiasi kwamba utajikuta unakuwa msomaji mzuri wa biblia, kwanza lazima uwe na kiu, na uwe umedhamiria kweli kutoka moyoni.
Sifa ya group hili ni kuhakikisha kila mmoja anakuwa msomaji wa Neno la Mungu, humo hatukai na wavivu, watu walio na visingizio vingi vya kutokusoma Neno la Mungu, ukiwa na sifa hizo unatolewa. Kutokana na kusimamia kanuni zetu, tumejikuta tupambana kuhakikisha mtu hakosi kusoma Neno la Mungu kuepuka kutolewa.
Kama umepata bahati kwa mara ya kwanza kusoma ujumbe huu, kwanza nikupongeza kwa uvumilivu wako kusoma kuanzia mwanzo hadi sasa. Unajiona unahitaji msaada wa kusimamiwa ili uwe msomaji wa Neno la Mungu, nakukaribisha kwenye group letu ukiwa na nia kweli ya kusoma.
Unaweza kufikiri nakutania au unaweza kufikiri nitawezaje kusimamia mtu mmoja mmoja hadi kujua fulani anasoma na fulani hasomi, tena kwa njia ya mtandao wa whatsApp. Waliopo wanajua ninachosema, na kama umewahi kuwepo group utakuwa unaelewa ninachosema hapa.
Usikubali kushindwa, nimeshakuhakikishia unaweza, usitafute mwingine wa kukuambia unaweza au huwezi. Nimekueleza mimi ninayejishughulisha na jambo hili kila siku, ukianza kutafuta msaada wa wengine, wengi wao utakutana nao wasio soma Neno la Mungu. Hao ndio watakuvunja moyo kabisa kwa kukuambia maneno mengi ya kukatisha tamaa.
Tuwasiliane kwa njia ya whatsApp kwa namba hizo chini, ukiwa umedhamiria kweli kutoka moyoni mwako. Bila kuangalia mazingira ya kazi zako, biashara zako, shule/chuo chako, na familia yako. Nakuomba sana nitumie ujumbe kwa njia ya whatsApp kupitia namba ninazo kwenda kuzitoa hapo mwisho.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea Tovuti yetu www.chapeotz.com kupata masomo mengine mazuri zaidi. Pia unaweza kumjulisha ndugu/rafiki yako kuhusu tovuti yetu ili awe anapata mafundisho ya kumjenga katika eneo la usomaji wa Neno la Mungu.
Nakutakia siku njema.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Tovuti: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081