Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, ashukuriwe Mungu atupaye uhai wake na atupaye kushinda. Kila mmoja aliyeifikia siku ya leo, anayo nafasi ya kumzalia Bwana matunda yaliyo mema ikiwa kila mmoja wetu atatambua umhimu wa yeye kuwepo hapa duniani.

Ipo misimamo ya kidini, ambayo inawafanya washirika wote kuwa na kauli moja. Na wakati mwingine inawatofautisha na watu wengine ambao na wao pia ni wakristo.

Misimamo ya dini inaweza isitokane kabisa na Neno la Mungu, ndio, sio kila msimamo unasimamiwa kwa Neno la Mungu. Misimamo mingine inatungwa tu na sisi wenyewe wanadamu, kutokana labda na tamaduni zetu, au kutokana na labda mazingira tuliyopo/tuliyokulia.

Na kadri jambo linavyozidi kusimamiwa kwa nguvu na likaleta yale matokeo mazuri aliyoyatarajia na mleta kanuni hiyo. Na ikawa huyo aliyeisimamia hiyo sheria/kanuni/pendekezo akawa na nguvu ya ushawishi kwa jamii, anaweza akawa kiongozi wa taifa au kikundi au kanisa au ukoo au jamii fulani. Ni rahisi sana watu kufuata kile amesema.

Sheria zile huzaa misimamo mikali ya watu, mtu anaweza kuhakikisha anakufa kwa ajili ya kusimamia misimamo ya dini yake. Ila akawa mtende dhambi mzuri tu, na wala akawa hapati shida au wasiwasi kwa uovu/uchafu anaofanya. Si unajua dini haiwezi kukusaidia kushinda dhambi isipokuwa Neno la Mungu likiwa ndani yako.

Wasiwasi wake anaoweza kuwa nao, ni kulinda asionwe na viongozi wake wa dini au asionwe na washirika/waumini wenzake wa dini yake. Hii inafanya watu kushika sana dini zao kuliko kumshika Yesu Kristo, sio vibaya kutii kanuni na taratibu za dini yako, ila hazipaswi kuchukua nafasi ya Neno la Mungu.

Misimamo ya dini yako haipaswi kuwa juu ya Neno la Mungu, bali misimamo ya dini yako inapaswa kuwa chini ya Neno la Mungu. Na sio misimamo ya moja kwa moja yaani nikiwa na maana sio ya kudumu milele. Muda wowote inaweza kubadilika kadri unavyozidi kupata elimu ya Neno la Mungu, maana elimu nyingi hazijatokana na Neno la Mungu.

Tunakabiliwa na kasumba moja, kutokutaka kuonekana ulikosea, hili ndio linawafanya walio wengi kuendelea kushikilia yale yale ambayo tayari wamegundua walikosea. Ili kulinda heshima zao kama wanavyofikiri wao, hawatakaa wakubaliane na kubadili misimamo ya dini zao.

Hili sio kwenye dini tu, hata kwenye familia, mzazi anaweza kumkosea mtoto wake na akamtenda jambo la kumuumiza moyo wake. Wakati mtoto yule hajahusika na lile analomshutumu nalo, mzazi kuomba msamaha kwa mwanaye inaweza kuwa tabu na wakati mwingine asiombe kabisa ili kuepuka kuonekana alikosea.

Jambo hili linaenda hadi kwa wanandoa, mwanaume ili kuonekana hawezi kuwa chini ya mwanamke. Hata kama atamkosea mke wake, na akatambua kabisa alitenda kosa na anachopaswa kufanya ni kumwomba msamaha mwenzi wake. Mwanaume yule atasimamia vile vile msimamo wake kwa kigezo cha kulinda heshima ya uanaume wake.

Kumbe msamaha huwezi kuondoa heshima ya mtu yeyote yule, zaidi kuomba msamaha inarejesha uhusiano mzuri na Mungu wako, na inamfanya yule aliyekosewa kujisikia kujaliwa kwake na aliyemkosea.

Nataka kusema nini hapa, ninachotaka kukueleza hapa yaani kiini cha maelezo haya yanalenga nini, kinacholengwa hapa ni hichi; kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu, kuna vitu vingi ulivyokuwa umevijaza kwenye moyo wako na kuvimiani, vitaondolewa na maarifa ya Neno la Mungu.

Vinapoondolewa vile ambavyo ulikuwa unaviamini mwanzo ni sahihi, vitazaliwa vipya na vizuri zaidi. Na utajua ulikuwa hasi sana kuhusu Mungu kwa baadhi ya mambo yake.

Utaona kusoma Neno la Mungu sio kukusaidia upande fulani tu, kumbe Neno la Mungu linaweza kukubadilisha kabisa mtazamo wako. Ukawa mtazamo mzuri zaidi, na baadhi ya misimamo yako isiyostahili ikaonekana haifai tena kwako kuisimamia au kuishikilia.

Elekeza nguvu zako katika Neno la Mungu, ipo hazina kubwa unaenda kuichota. Ile kweli isiyotiwa sukari/chumvi mahali popote, utaenda kuijua mwenyewe, utabaki kuamua mwenyewe kuendelea kusimamia misamamo yako inayopingana na Neno la Mungu au kufuata Neno la Mungu linavyokuelekeza.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

chapeo@chapeotz.com

www.chapeotz.com

+255759808081