Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.

Tunapokuwa kwenye safari, tutakutana na changamoto za kila aina, unaweza kukutana na changamoto ambayo hukuiweza kabisa. Lakini ikaja mbele yako, huna namna ya kuikwepa utapaswa kupambana nayo kuhakikisha imeisha salama.

Wengi tunapokutana na changamoto ngumu, huwa tunashindwa kuhimili maumivu makali. Badala yake tunaanza kutafuta kukimbia ile changamoto, tunapojaribu kukimbia kinachotukabili mbele yetu, wengi wetu huwa tunaanza kutafuta kupunguza bidii zetu kwa Mungu.

Ulikuwa mtu wa ibada, unaona ngoja nipumzike kwanza kwenda kanisani, ulikuwa mtu wa maombi unaona ngoja nipumzike kwanza kuomba, ulikuwa mtoaji mzuri kwa wahitaji unaona ngoja niache kabisa kutoa, na ulikuwa msomaji mzuri wa biblia unaona ngoja niache kwanza kusoma Neno la Mungu.

Unavyofikiri wewe unaona ukiacha hayo mambo utakuwa umepunguza mzigo, unaona labda kusoma Neno la Mungu ni mzigo kwako, unaona maombi ni mzigo kwako, unaona ibada za kanisani ni mzigo kwako. Ndio ni mzigo kwa sababu umeacha kufanya ya msingi, umeona upunguze hayo mpaka utakapopita kwenye changamoto yako ngumu uliyokuwa unapita.

Kinachoshangaza na kusikitisha ni kwamba, tangu useme unapumzika kwanza, hadi leo hujawahi kuvuka hiyo changamoto. Kama umeivuka, mbona huombi tena kama zamani, mbona husomi tena Neno la Mungu, mbona huendi tena kanisani, mbona hujali tena wahitaji kama zamani.

Utakataa na kusema bado upo vizuri sana kiroho, mbona matendo yako yanapingana kabisa na kauli zako. Ungekuwa hupingani na kauli zako, tungekuwa tunakuona ukiwa na bidii yako ile ile ya kusoma Neno la Mungu, na tungekuwa tunakuona na bidii yako ya ibada.

Umeruhusu ndoa yako ikuondoe kabisa kwenye eneo la uanafunzi wa Yesu Kristo, Umeruhusu biashara yako ikuondoe kabisa kwenye bidii ya ibada, Umeruhusu kuachwa na mchumba wako umekosa na hamu ya kuomba na kusoma Neno, Umeruhusu kupoteza kazi au fedha zako umeona kujishughulisha na mambo ya Mungu hakufai tena.

Ulichokosea ni kuruhusu kutawaliwa na changamoto ngumu zilizojitokeza mbele yako, ilikuwa inaumiza kweli. Ila hukupaswa kuchoka mapema, ulipaswa kusimama imara na kusonga mbele bila kuangalia mazingira magumu unayopitia.

Tena wakati unapita pagumu unapaswa kuwa karibu zaidi na Mungu, maana wakati huo ndio wakati uliojaa makelele mengi, ni wakati uliojaa washauri wengi wazuri na wabaya, ni wakati uliojaa vishawishi vya kila namna. Unaweza ukajikuta upo njia panda unashindwa ufuate lipi na uache lipi, ni wakati ambao unamhitaji Mungu sana.

Simaanishi usubiri uwe kwenye matatizo ndio uwe karibu sana na Mungu, wakati haupo kwenye matatizo unakuwa mbali na Mungu. Kama utakuwa unasubiri upate shida ndio uwe karibu na Mungu, huo utakuwa usanii wa hali ya juu. Ninachomaanisha hapa, utulivu wako unapaswa kuwa zaidi kwa Mungu kuepuka kuingizwa kwenye upotovu.

Tofauti kabisa siku za leo, mkristo akiguswa kidogo na changamoto humwoni tena akiendelea na juhudi zake mbele za Mungu. Wengi sana walikuwa watumishi wazuri sana wa Mungu, ila changamoto ziliposimama mbele yao na utumishi uliishi hapo hapo. Wengi sana walikuwa na bidii sana ya kusoma Neno la Mungu, ila baada ya kukutana na changamoto ngumu mbele ya safari yao ya usomaji wa Neno la Mungu, waliacha kabisa.

Dawa ya haya yote ni kutokubali changamoto ikuondoe kwenye utaratibu wako wa kusoma Neno la Mungu, haijalishi utakutana na nini. Ilimradi uhai wako upo, macho yako bado yanaona, hakikisha ratiba yako ya kusoma Neno la Mungu ipo palepale. Haijalishi jambo gani limekuvuruga sana akili yako, hakikisha unatafuta utulivu kisha unasoma Neno la Mungu.

Ukikubali kupumzika mpaka changamoto itakapoisha, nakwambia ukweli itaisha na itakuja nyingine mpya kabisa kwa namna yake. Utaona ya mwanzo ilikuwa afadhali na uliopo sasa ndio ngumu zaidi, kumbe ungendelea na zoezi lako la kila siku usingekwama kama ulivyokwamishwa sasa.

Usiwe na bidii kwa mambo ya Mungu ukiwa na furaha tu, hata wakati wa huzuni uwe na moyo uleule wa kumpenda Mungu. Unaumia kweli, ila fahamu unayemtegemea ndiye mwenye vyote hivyo, akisema ndio hakuna wa kusema hapana, na akisema hapana hakuna wa kusema ndio.

Kipo kitu umejifunza kupitia ujumbe huu, nikusihi tena usirudi nyuma kwa namna yeyote ile. Komaa hivyo hivyo hata kama kuna wakati unaona giza mbele yako, usije ukaacha bidii yako kwa mambo ya kiroho na kimwili.

Mungu akubariki sana.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Tovuti: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081