Haleluya,

Nimekuwa nikiwahamisha sana watu kwa muda mrefu sasa kuhusu umhimu wa kusoma Neno la Mungu, na nimekuwa nawapa njia mbalimbali na rahisi za kuweza kusoma Neno la Mungu. Walio wengi wanaonekana wanapenda sana kusoma Neno la Mungu, ninapowapa njia ya kuonyesha kupenda kwao kusoma la Mungu binafsi nakosa kabisa kuuona huo upendo wao.

Kila mmoja anaweza kusema nimeokoka na nampenda Yesu Kristo, Lakini ukija kutazama matendo yake yanamkataa kabisa kuwa yeye ameokoka. Wokovu wetu haupo tu mdomoni, kinachoweza kututhibitishia kuwa tumeokoka ni matendo yetu.

Wengi wanaisomea biblia mdomoni kwa kubaki kusema wanapenda kusoma Neno la Mungu, ila ukija kwenye vitendo unaukosa kabisa ule upendo wao wanaouzungumza.

Tutabaki kuwa waongo hadi lini? Tutaendelea kujidanganya hadi lini? Tunafikiri tukisema tunapenda sana kusoma Neno la Mungu. Alafu tukawa hatulisomi, ndio litaweza kukaa mioyoni mwetu kwa kuzungumza mdomoni tu? Hapana haitawezekana pasipo kuchukua hatua ya kulisoma.

Ni upendo upi huo usio na matendo yanayoonekana kwa nje, hivi tunaweza kusema tunampenda Mungu alafu tunafanya matendo maovu. Upendo ni kufanya yaliyo kinyume na Mungu, au upendo ni kufanya yale yanayompendeza Mungu? Bila shaka ni kutenda yale yanayompendeza Mungu.

Unaweza kusema unampenda mke wako, na wakati kila siku unakimbizana na wanawake wengine huko nje. Ni upendo gani ulio kwa mke wako na wakati unachepuka nje ya ndoa, mbona maneno yako hayafanani na matendo yako. Sawa huna tabia mbaya ya kutoka nje ya ndoa, mbona kila siku ngumu na makofi/vibao haviishi kwa mkeo? Huo ndio upendo? Ukitoka nje unaonyesha kwa watu kuwa unamjali mkeo!!

Unasema unampenda mume wako, na wakati unafanya vitu vya kumkomoa na kumzalilisha mbele ya ndugu zako. Ni upendo gani huo usioweza kukuzuia kusema yasiyostahili kuyasema kwa ndugu zako?

Nikitoa tangazo la kujiunga group la whatsApp kwa ajili ya kusoma Neno la Mungu, yaani mtu atakavyokuja kwa mbwembwe utafikiri huyu kweli alikuwa na kiu ya siku nyingi ya kusoma Neno la Mungu. Ila alikuwa hajui aanzie wapi, baada ya kuwa pamoja naye tu anaanza sababu zake nyingi za kushindwa kusoma Neno la Mungu.

Sababu zenyewe ni sina muda wa kutosha wa kusoma Neno la Mungu, anasema hana muda wa kutosha ila unamkuta kwenye magroup ya whatsApp anachati. Anasema hana muda ila unamkuta instagram anapitia kila kinachoendelea, anasema hana muda wa kusoma Neno ila Facebook humkosi online.

Yule ambaye hana simu yenye uwezo wa kuingia mitandao ya kijamii, anakwambia anapenda kusoma Neno la Mungu ila hajawahi kusoma. Ukimpa mbinu za namna ya kusoma, anaanza kweli kusoma ila akienda sana wiki au mwezi au miezi miwili, baadaye anakwambia hana muda anabanwa sana na shughuli. Ila muda wa kukaa vijiweni anao, ila muda wa kukaa na marafiki zake wakiongea upo, ila muda wa kuzunguka mtaani huku na kule upo.

Kupata nusu saa tu mtu anakwambia hana huo muda, ila ukimgusa anakwambia anampenda Mungu. Anampenda Mungu alafu hataki kukaa alijaze Neno lake moyoni mwake, ni upendo wa maneno matupu.

Hatutaweza kuepukana na kumtenda Mungu dhambi kwa kukosa Neno lake, hofu inakosekana kwa kukosa maarifa ya Neno la Mungu. Unakuta mkristo kabisa ana miaka ya kutosha kanisani ila anashindwa kusamehe, anachofanya analinganisha kosa alilotendewa anaona ni kubwa sana hataweza kusemehe kamwe.

Hebu tubadilike, kusema unapenda sana Neno la Mungu alafu hutaki kulisoma, huo ni uongo. Kama unapenda kweli Neno la Mungu hebu onyesha basi kwa vitendo, tuone basi kwa vitendo, maneno matupu tumechoka kuyasikia. Hatuhitaji ukae barabarani uanze kusoma Neno la Mungu ili tukuone, jifungie chumbani kwako ila matendo yako yatatujulisha kuwa huyu ni msomaji wa biblia.

Shahidi mwaminifu ni wewe mwenyewe, hata ukijidanganya unasoma alafu ukawa husomi, uwe na uhakika dhamiri yako itakushitaki. Epuka kuongea tu kuonyesha kupenda alafu upendo wenyewe ni wa mdomoni tu.

Chukua hatua leo, kuna eneo lolote unaona kukwama kwenye usomaji wako wa Neno la Mungu, naomba tuwasiliane kwa namba hizo chini nitakusaidia.

Mungu akubariki sana.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Tovuti: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.