Haleluya,

Tunapookoka, siku za kwanza huwa tumejaa ujasiri na nguvu kubwa sana. Ujasiri huu huwafanya hata wale ambao bado hawajamjua na wale ambao tayari wamejua Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wao, waanze kututazama kwa umakini.

Kasi ile inaweza kwenda vizuri sana kwa sababu muda mwingi tunakuwa tunautumia kumtafakari Bwana mahali ametutoa, muda mwingi tunakuwa tunautumia kuomba Mungu, muda mwingi tunakuwa miongoni mwa watu wanaopenda kusikia Neno la Mungu kuliko mengine.

Kadri unavyozidi kujituma kwa kusikiliza watumishi wa Mungu, jinsi unavyojisukuma kuomba Mungu. Inakuweka kwenye uwepo wa Mungu na kujiona upo salama zaidi, muda mwingine hata changamoto ikija mbele yako unaiona sio kitu.

Tunavyozidi kwenda mbele zaidi, kuna mambo mengi sana tunakutana nayo, zipo habari za kutuonyesha hatukufikiri vizuri sana kuokoka. Zipo habari zinatujia na kutuonyesha tunakosa mengi tunapokuwa ndani ya wokovu.

Na kweli ukijitazama unaona kuna uhuru unakuwa huna, kama ni kijana unaona umejinyimwa uhuru mwingi wa kujiachia kwenye mambo yako. Kama ulikuwa mtu wa wanawake/wanaume unaona hiyo nafasi huna tena, maana watakuwa wanakuchokoza kila wakati lakini wanaona umefunga milango. Pamoja na kufunga milango unaona hawachoki kukuchokoza, yaani ni kama vile wanajua ule wakati unajisikia mpweke hapohapo wanakutafuta.

Ukijitafakari vizuri unaanza kuona una vitu unavitaka ila huwezi kuvirudia tena, na wakati mwingine ukikaa tena na kujitafakari unaona huvipendi kabisa moyoni mwako ndio maana uliamua kuokoka.

Nikufungue macho leo, hayo mawazo yote machafu unayoyapata na mengine unayokutana nayo mtaani. Ukafika wakati ukaanza kusema ila ni kweli unakosa mengi, ujue uchanga wa kiroho unakupelekesha wakati huo.

Usipokuwa makini wakati upo mchanga kiroho, inaweza kukupelekea ukarudia matapishi uliyoyaacha zama za ujinga. Ndio maana nikaanza kichwa cha somo, kuokoka tu haitoshi, unapaswa kuchukua hatua zingine zaidi kukufanya uwe imara.

Hatua moja wapo ni kusoma Neno la Mungu, Neno la Mungu linauwezo wa kukufinyanga vizuri sana. Zile tabia zako zote za kale zitaondolewa kabisa, kadri unavyozidi kulijaza Neno la Mungu moyoni mwako ndivyo na ujinga unauondoa kwako.

Hakuna jambo lolote hasi linaweza kukaa moyoni mwa mtu anayetumia muda wake mwingi kujaza maarifa sahihi, ni ngumu sana kumpata mkristo aliyeamua kuokoka na kuachana na mambo ya dunia. Alafu mkristo yule akawa na tabia ya kusikiliza sana mafundisho ya Neno la Mungu, na kulisoma mwenyewe Neno la Mungu. Huyu mkristo lazima awe na stamina za kuhimili mambo mazito yanayotaka kumrudisha nyuma.

Wokovu sio mteremko kama wengi tunavyofikiria, tena ukiokoka ndio umetangaza vita na shetani maana tayari unakuwa kinyume na kazi zake. Uzuri ni kwamba vita hivyo huvipigani wewe mwenyewe, yupo Yesu Kristo anaweza kukusaidia. Shida unaweza usijue uwezo na nguvu za Mungu juu ya maisha yako, kutokana na kutopenda kusoma Neno lake unashangaa badala ya kushinda unashindwa.

Uzuri wake kila mtu aliyeokoka anacho kibali mbele za Mungu, cha kumwomba Roho Mtakatifu amsaidie kuelewa maandiko matakatifu. Kama Roho Mtakatifu anaweza kuwa mwalimu wetu, tuna mashaka gani kuhusu kulielewa vyema Neno la Mungu?

Shida yetu tunachanganya uvivu ndio tunaona hatuwezi kulielewa Neno la Mungu, yaani mtu anaanza kusoma kidogo anaona haelewi sana anaamua kuacha. Kumbe kilichomfanya ashindwe ni uvivu wake na mawazo yake potofu aliyoyajaza moyoni mwake, anaona ugumu kabla ya kujua kilichoandikwa ndani yake.

Tufike mahali tuache kulichukulia Neno la Mungu kwa kawaida, ukawaida huu umetupelekea wengi kushindwa kuhimili Changamoto za maisha yetu. Kawaida hii imetufanya wengi kuanguka dhambini, kwa kukosa maarifa sahihi ambayo yangetusaidia kujiepusha na mitego ya mwovu shetani.

Mama wa mambo yote ni Neno la Mungu, Neno la Mungu limebeba kila kitu kwenye maisha yako, zipo huduma ambazo zinafufuliwa na Neno la Mungu. Ambapo hizo huduma zisingeweza kuonekana kirahisi kwa mtu kama asingekuwa msomaji mzuri wa Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Tovuti: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081