Haleluya,

Kila mmoja anaishi ila sio kila mtu analiishi kusudi lake alilotiwa na Mungu hapa duniani, wengine tupo ilimradi tumeiona siku tunafurahi na maisha yanaendelea.

Kila mmoja akianza kutafuta kusudi lake la kuzaliwa, dunia itapunguza idadi kubwa ya watu wasiomzalia Mungu matunda, dunia itapunguza idadi kubwa ya wafanyakazi wanaofanya kazi wasizozipenda, dunia itapunguza idadi kubwa ya watumishi wanaotumika maeneo yasiyo yao.

Kutafuta maarifa sahihi ni kutaka kufahamu mambo, kadri unavyozidi kujifunza ndivyo unavyozidi kufunguka zaidi, haijalishi ni kwa pole pole au kwa haraka. Kadri Mungu alivyokupa uwezo wa kupokea mambo ndivyo unavyozidi kufahamu mengi zaidi.

Kukaa tu tukijipa matumaini tunafahamu vitu, haiwezi kutufanya tufahamu kwa kufikiri tunafahamu. Kufahamu kunakuja pale tunapotoa muda wetu kujifunza kwa wengine kupitia vitabu vyao, na kwa kuhudhuria semina zao za mafundisho.

Kuchota maarifa mengi na sahihi ni bidii ya mtu mwenyewe, hatufanani katika hili. Yule mwenye bidii sana ya kutafuta maarifa, ndio atakayekuwa na maarifa ya kutosha kwenye ufahamu wake na ndiye atakayefanya vizuri zaidi kwenye eneo lake.

Tunasoma biblia ili iweje? Tunapenda kujua yale aliyotuahidia Mungu wetu, maana ndani ya Neno la Mungu kuna kila kitu ambacho Mungu alimwahidia mwanadamu. Tunapojua yale tunapaswa kuyaishi, ni rahisi sana kumwambia Baba yetu aliye mbinguni kutupa haja ya mioyo yetu.

Wakati mwingine tumepungukiwa na hekima kwenye eneo fulani katika maisha yetu, tunakazana kuomba Mungu atupe hekima. Kumbe haikuhitajika maombi, ilihitajika maarifa sahihi ili uweze kuelewa namna ya kuenenda katika eneo hilo unaloonekana umepungukiwa hekima.

Fanya bidii sana kila iitwapo leo, bidii yako ya kusoma Neno la Mungu sio kazi ya kutuanga maji kwenye kinu. Ni kazi inayokuzalishia faida kubwa sana hata kama usipoiona kwa sasa, wakati unavyozidi kwenda utajua zaidi ulichokuwa unafanya.

Hasara hakuna kwa kutafuta maarifa sahihi, japo wengine wanaweza wasione usahihi wake kutokana na jinsi walivyolelewa. Pamoja na kutokujua kwao hakuwezi kuwafanya wakabadili ukweli wa jambo isipokuwa kuchukua hatua.

Usichoke kujifunza Neno la Mungu, ndio maarifa mengi yalipolalia pale, unaweza kujifahamu upo kundi gani, unaweza kujua Mungu amekupa huduma gani ya kuwasaidia wengine na ukamzalia matunda, na ukamletea sifa na utukufu yeye.

Unaweza kujua kwanini unapaswa kuendelea kuishi na usife haraka kabla ya wakati wako, utajuaje? Utajua pale utakapotambua nafasi yako aliyokuitia Mungu wako. Maana ndani ya Neno lake amekuahidia mambo mengi, ambayo ukiyajua vizuri ni rahisi kwako kumdai haki zako za msingi pale unapoona kuzikosa.

Ifanye biblia rafiki yako wa kweli, bora ukose mambo mengine mazuri ila usikubali ukose Neno la Mungu. Siku yako usiruhusu iishe bila kusoma Neno la Mungu, shabaha yako kuu ni kupata maarifa, kutaka kujua zaidi ili uweze kufanya vizuri zaidi katika huduma yako, na katika maisha yako ya wokovu.

Kwa sababu kiu yako ni kutaka kumjua Mungu wako na kuishi maisha matakatifu, tafuta maarifa sahihi ambayo ni Neno la Mungu. Haya ndio yatakusaidia kujenga uhusiano wa karibu zaidi na Mungu wako, hakuna siku utatamani kumkosea yeye kutokana na changamoto yeyote ile itakayosimama mbele yako.

Kila siku utamwona Mungu akiwa upande wako, utaona uzuri wa Mungu katika maisha yako, kwa sababu una ufahamu wa kutosha kuhusu Mungu. Tofauti na yule anayesema ameokoka lakini hana Neno la Mungu moyoni mwake, wakati mwingine anakosa ujasiri mbele za watu wa kulitaja jina la Yesu Kristo kutokana na hali yake ya udhaifu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

chapeo@chapeotz.com

www.chapeotz.com

+255759808081