Haleluya,

Kila mmoja anaweza kuonekana ana bidii kwa mambo ya Mungu, ila sio kweli wote wana bidii ya mambo ya Mungu. Wengine wanakuwa na bidii kwa sababu fulani wanazoona wao, ila ndani yao hakuna kabisa ile hamu ya mambo ya Mungu.

Wengi wetu pia tunamwomba Mungu atusaidie jambo fulani ila ukweli utabaki ndani ya mioyo yetu, ile imani kwa tuliyoomba, inakuwa haipo kabisa. Kinachotufanya tusiwe na imani, ni kile kiwango cha Neno la Mungu kilichopo ndani ya mioyo yetu.

Hamu ya kuendelea kumpenda Mungu bila kutazama nani anatutazama, inaletwa na uelewa wa mtu anayeanza kumjua Mungu wake. Na kumjua Mungu haiji kwa ghafla, ni ile bidii ya mtu anayeifanya yeye kama yeye kila siku.

Ile hamu inampelekea kuwa na bidii au bidii yake inampekelekea kuwa na hamu, hayo yote yanamfanya kiwango chake cha imani kinazidi kuongezeka siku hadi siku. Wakati mwingine anaweza asijue mwanzo ila kadri anavyozidi kusogea hatua fulani mbele anakuwa na uelewa kwa kile kimemfikisha pale.

Hichi kinachoonekana ni kidogo leo, ndicho kinamfanya mtu kupata kikubwa zaidi. Na Wengi wetu huwa tunadharau sana hizi hatua ndogondogo, tunataka kufikia hatua kubwa kwa wakati mmoja, bila kujua mpaka ufikie hiyo hatua kubwa. Unahitajika kuanza kwa hatua ndogo sana na inayoonekana ni dhaifu kwa akili za kibinadamu.

Hamu ya kuendelea kumpenda Mungu bila kuchoka, inatengenezwa na mtu mwenyewe, na kutengenezwa huko ni vile anavyozidi kumjua Mungu wake, kupitia usomaji wake wa Neno la Mungu.

Neno la Mungu linaamsha vitu vingi sana vilivyolala ndani mwa mwamini, unaweza kufika mahali ukakosa tumaini kabisa. Ila kupitia Neno la Mungu, ukaletewa mstari mmoja tu wa kukupa nguvu za kusonga mbele.

Watu wanaweza kukuona umechoka sasa hivi, wakitegemea huyu ndiyo mwisho wake leo wa kumtumikia Mungu. Kesho wakija kukuona wanaweza kushindwa kuelewa vizuri maana watakuona jinsi walivyokuona jana ulivyokuwa umeumizwa moyo wako. Leo ukaamka ukiwa na nguvu, na furaha, na hamu ya kuendelea na kile ulikuwa unafanya.

Asikuhangaishe mtu kwa jinsi unavyotenga muda wako kwa ajili ya kusoma Neno la Mungu, inaweza kuonekana hakuna unachokifanya. Ila nakwambia muda sio mrefu utajua ulichokuwa unafanya au watajua kile ulikuwa unafanya.

Nakueleza vitu halisi ninavyoviona kwenye maisha yangu, hatua niliyoanza nayo ya usomaji wa Neno la Mungu, sio hatua niliyonayo sasa hivi. Ipo hatua kubwa iliyozaliwa kwa kuanza na hatua ndogo, yale maarifa machache ninayopata kila siku yananifanya niwe imara kila iitwapo leo.

Kuelewa haya ni mpaka uamue mwenyewe ndani ya moyo wako, bila kusukumwa na mtu yeyote. Maana ukifanya kwa kusukumwa sana unaweza kujenga chuki na mtu, ukashindwa kupokea kile ulipaswa kupokea. Lakini ukifanya kwa moyo hata kama unakumbushwa na, kuhimizwa haiwezi kukupa shida kwa sababu ipo ndani ya moyo wako.

Usijikatishe tamaa katika usomaji wako wa Neno la Mungu, na wala usiruhusu mtu yeyote akuvunje moyo kwenye eneo hili la usomaji wa Neno la Mungu. Nakuambia hivi kwa sababu utakutana na watu wa kukuvunja moyo, na huenda umeshakutana nao sana, na huenda wamechangia kukupunguzia kasi ya usomaji wako wa Neno la Mungu.

Umevunjwa moyo na kudharau hatua zako ndogo kwa sababu kuna vitu ulikuwa bado hujavielewa, ila kwa sababu umevielewa kuanzia sasa kuwa imara. Asikuyumbishe mtu yeyote wala changamoto yeyote isikutoe kwenye mpango wako wa kusoma Neno la Mungu.

Zile hatua ndogo wanazozipuuza wengine, wewe tumia nafasi hiyo kuonyesha udhaifu wao upo wapi. Mungu atukuzwe kupitia wewe, maana watakapotazama matunda yako watagundua makosa yao.

Mungu akubariki sana kwa muda wako uliotoa kusoma ujumbe huu. Kupitia ujumbe huu, Mungu akakupe kiu mpya kabisa ya kusoma Neno la Mungu.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Tovuti: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081