Haleluya,
Marafiki wana mchango mkubwa sana, marafiki wengi tabia zao zinaendana kimatendo na kimtazamo. Marafiki walioshibana haswa, hawawezi kuwa tofauti sana kimtazamo, wote huwa wanakuwa sawa kimawazo na jinsi ya kutazama mambo.
Marafiki walioshibana haswa, ukiachana na ule urafiki wa mdomoni ila kwenye matendo haupo. Ule urafiki haswa ambao wahusika wameshibana, hata mmoja wao akipatwa na shida wapo tayari kusimama naye mpaka mwisho. Huo urafiki una mchango mkubwa sana kumbadilisha mtu.
Ukiwa na urafiki na mtu, hasa wewe ukimpenda awe rafiki yako, zipo tabia nyingi sana utazichota kutoka kwake. Japo kumkubali mtu sio lazima uige tabia zake zote, ila hii ni tofauti na marafiki wanaoenda pamoja kila siku.
Ndio maana wazazi wenye akili na wanaotazama haya mambo kwa kina, hawawezi kuruhusu mtoto wake acheze na mtoto fulani, kutokana na mtoto yule kuwa na tabia mbaya zisizoendana na mtoto wake.
Rafiki anaweza kumwambukiza mwenzake tabia njema au tabia mbaya, inategemeana na marafiki wale wana tabia gani kwa kila mmoja wao. Lakini mpaka watu waitwe marafiki uwe na uhakika kuna vitu vingi sana wanaendana.
Binafsi nimejifunza hili, nikiona mtu anakuwa rafiki yangu alafu nikaja kugundua kuna tabia hatuwezi kuendana na mwenzangu hawezi kukubali kuziacha. Huwa namwondoa kabisa kwenye kundi la marafiki ninaoweza kushirikishana nao mambo ya ndani zaidi, ninachofanya nambakisha rafiki wa kawaida tu.
Kila mtu anaweza kuwa rafiki yako, wala hatupaswi kuwa maadui kwa watu, wala hatuwezi kujitenga kabisa na watu. Kushirikiana na ndugu au jamii inayokuzunguka ni mhimu sana, ila hatuwezi kuwaweka kwenye ule urafiki wa ndani.
Wakati mwingine tukiona watu wapo pamoja sana huwa tunafikiri ni marafiki, wakati mwingine inaweza ikawa hivyo, na wakati mwingine inaweza isiwe hivyo.
Nasema hivi, si kila mwana ndoa ni rafiki wa mwenzake, wapo wanandoa mpaka leo wana mwaka wa kumi kwenye ndoa ila hawajawahi kuwa marafiki. Pamoja na kuishi kama mke na mume, ila kuna mambo nyeti hawawezi kushirikishana kutokana na kutoaminiana. Na sifa mojawapo ya marafiki walioshibana ni kuelezana vitu vya ndani ambavyo mtu mwingine asiye rafiki hawezi kuvijua.
Kuna mambo huwezi kumweleza rafiki yako kama ilivyo kuna mambo huwezi kumweleza mzazi wako, ila unaweza kumweleza mke au mume wako. Usije ukanielewa vibaya hapa katika eneo hili la urafiki, usije ukaanza kutoa vitu vingine ambavyo haipaswi kutolewa.
Ninaposema marafiki walioshibana wanaweza kuelezana mambo mengi sana ya ndani ambayo mtu mwingine hawezi kuelezwa, simaanishi kwamba kila kitu watakuwa wanaambiana. Zipo siri zingine za kikazi/kiofisi, rafiki hapaswi kujua kabisa, zipo siri zingine za chumbani kati ya wanandoa hazipaswi kuelezwa kwa rafiki wa nje.
Nikija kwenye moyo wa somo hili, tunapaswa kuambatana na marafiki wanaopenda kusoma Neno la Mungu. Hawa marafiki wana mchango mkubwa sana kutusaidia kuendelea kuwa wasomaji wa Neno la Mungu pasipo kutamani kurudi nyuma.
Kuna wakati tunajisikia kuchoka sana, kuna wakati tunajisikia kukata tamaa, kuna wakati tunajiona hatuelewi tunachosoma. Lakini tunapokuwa na marafiki tunaoendana nao, tunaowasikiliza mashauri yao mazuri, marafiki ambao wakizungumza jambo kwetu tunawaelewa na kuwatii bila kujali umri wao ni mkubwa au mdogo. Wanaweza kuwa na mchango mkubwa sana katika usomaji wetu wa Neno la Mungu.
Tunaweza kuwa na marafiki wa kazini, biashara zetu, huduma zetu, mashuleni, vyuoni, mtaani. Ila lazima tuwe na kikundi cha marafiki wanaotuhimiza kusoma Neno la Mungu, kwa sababu unaweza kuwa na rafiki ambaye ni wa kikazi/kibiashara tu na asiwe hata mkristo. Huyo hawezi kukuambia soma Neno la Mungu, yupo rafiki anayeweza kukuambia hivyo.
Ushauri wangu kwako, hakikisha unakuwa na marafiki wa kusoma Neno la Mungu kama unapenda kuwa msomaji mzuri wa biblia. Zaidi ya hapo utakuwa unajaribu kuanza na kuacha kila siku, lakini ukiwa nakwenye marafiki unaoweza kuwasikiliza kile wanakuambia, utafanikiwa katika hili.
Neno la Mungu linasema hivi;Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia. MIT. 13:20 SUV
Ukienenda na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima, na ukienenda na wapumbavu utaumia. Ndivyo ilivyo na kwenye kusoma Neno la Mungu, ukienenda na wanaopenda kusoma Neno la Mungu, nawe utakuwa msomaji wa Neno la Mungu. Na ukienenda na marafiki wasiopenda kusoma Neno la Mungu, nawe utakuwa sio msomaji wa Neno la Mungu hata kama ulikuwa na ka moyo cha kufanya hivyo.
Mungu akupe marafiki wengi wenye tabia njema ili ujifunze mambo mazuri kutoka kwao.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Tovuti: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081