Haleluya,

Wakati najiuliza nitaandika nini leo, huu ujumbe ukanijia kwa nguvu sana, nikaanza kutafakari kwanini tufanye vitu kwa bidii alafu inakuwaje hatuelewi tunachokifanya.

Wakati najiuliza hivyo nikumbuka shule, wakati tu watoto wadogo, wengi wetu huenda hatujawahi kujua kwanini tunapaswa kwenda shule. Ndio maana tulikuwa tunaamshwa kwa kulazimishwa, na wengine tulikuwa hatulazimishwi ila tulikuwa na bidii ya kwenda shule kuepuka adhabu ya fimbo.

Nikatoka kwenye watoto wadogo, nikaja kwa watu wazima namaanisha waliofikisha miaka 18 na kuendelea, wengi sana shuleni/vyuoni, ukimuuliza kwanini anasoma. Anaweza kukujibu ila sio ile inatoka moyoni mwake, au anaweza akashindwa kabisa kukupa sababu ya msingi. Ila cha kushangaza ana bidii sana darasani na wakati mwingine anakuwa wa kwanza.

Hili linakwenda mbali zaidi, leo dada ana hamu kweli ya kuolewa, ila pamoja na kuwa na hamu ya kuolewa. Hajui kwanini anaolewa, ndio hajui kwa sababu ukimuuliza majibu anayokupa unaona kabisa haelewi kwanini anataka kuingia kwenye ndoa.

Leo hii kaka anakwambia nahitaji kuoa, ukimuuliza sababu haswa za yeye kuoa ni nini, utakuta sababu kuu ni kutaka kujiepusha kufanya ngono ovyo. Zaidi ya hapo anakuwa hana sababu nyingine ya kumfanya yeye kuwa na mke, ndio maana wengi wanakuja kuanza kujuta mapema kwanini waliingia kwenye mahusiano ya ndoa.

Tunakwenda kwenye mahudhurio ya ibada kanisani, wengi wetu tunaenda kanisani ila uhalisia kabisa wa kutufanya sisi tuwe ibadani. Unaweza kutufanya tukashindwa kuelewa kwanini tunaenda, huenda tunaenda kanisani kwa sababu tumezaliwa tukakuta wazazi wetu wanatuhimiza tuende kanisani.

Huenda tulivyookoka tuliambiwa tusiache kwenda kanisani, tukashikiliaga hivyo mpaka sasa. Ila tukija kwenye uhalisia wa mtu mmoja kwanini anaenda kusali, kati ya watu 100 tunaweza kupata watu 10 wanaoweza kukueleza sababu ya msingi ya kumfanya yeye aende.

Sijui kama tunaelewana hapa vizuri, we chunguza hata makazini, watu wangapi wanajua nini maana ya kile wanafanya. Wapo wanafanya ilimradi mwisho wa mwezi ufike wapewa mshahara wao basi, utakuta mtu yupo mwaka wa kumi kazini lakini haelewi anachofanya.

Hebu jirudie mwenyewe ujiulize, mangapi unayafanya kwenye maisha yako na unaelewa kabisa unachofanya. Uwe mwaminifu katika kujichunguza, kama hutokuta mengi unafanya kwa sababu unaogopa adhabu fulani.

Labda Nikurahishie zaidi ili uweze kunielewa vizuri, unawahi kazini kwa sababu unapenda kuwahi au unawahi ili kukwepa kukutana na mstari mwekundu wa wachelewaji. Unawahi kanisani kwa sababu unaelewa umhimu wa kuwahi au unawahi ili kukwepa kiti cha nyuma na wewe umezoea cha mbele au unawahi kwa sababu umepangwa zamu ya kuhubiri au kuongoza ibada.

Hadi hapo majibu utakuwa nayo kama unatambua unachokifanya, au ulikuwa unafanya tu ila hujawahi kabisa kujua kwanini unafanya. Huenda mambo mengi umekuwa na bidii kufanya kwa sababu ya kuepuka usumbufu ila ukweli kutoka ndani ya moyo wako, hufanyi hivyo kwa kujua unafanya nini.

Hili tatizo la kutojua kwanini tunafanya, lipo hadi kwa wasomaji wengi wa biblia. Asilimia kubwa tunasoma tu kwa sababu tulisikia mchungaji akituhimiza kufanya hivyo na akatupa maneno fulani kutufanya tuogope. Ila uhalisia kabisa tunasoma lakini tunaona kama giza tu na kutimiza wajibu.

Tunakuwa na hamu kweli ya Neno la Mungu, ila tunachokifanya tunaona kama hatukielewi vizuri. Hata tunapoacha kusoma, hatuoni shida sana kwa sababu tangu mwanzo hatukuwahi kujua kwanini tunasoma Biblia.

Sawa na mtu aliyeokoka, wengi wanaanza vizuri mwanzoni, asipopata mafundisho mazuri ya kujitambua vizuri kwanini ameokoka. Labda akawa ameokoka kwa sababu tu aliona mtoto wake, mume wake, mke wake, ndugu yake akiponywa na ugonjwa fulani. Anaona na yeye aokoke, au alikuwa na shida ya mahusiano ya ndoa akapata mtu akamwambia bora kuokoka hayo yote yataisha.

Uwe na uhakika atarudi nyuma upesi sana, ni sawa na kijana aliyeacha uzinzi kwa muda ili apate mke/mume. Lakini ndani ya moyo wake ni mzinzi bado, japo kwa nje anaonekana ameokoka.

Ukweli ni kwamba, mwanzo unaweza usijue sana kwanini unasikia msukumo wa kufanya jambo fulani, ila kadri unavyozidi kufanya ndivyo unazidi kuelewa kwanini ulikuwa unasikia msukumo wa kufanya. Ila sio wote wanafikia mwisho wakaelewa kwanini walikuwa wanafanya.

Jifunze kumwomba Mungu akufungue ufahamu wako uweze kuelewa kwanini unafanya, ukielewa kwanini unasoma Neno la Mungu nakwambia haijalishi litakuja jambo gani katika maisha yako. Hutokaa uache kamwe, vinginevyo utakuwa unaanza leo, unajisukuma kwa muda fulani mfupi na kuacha.

Huenda hata hapa unasoma ila huelewi kwanini unasoma au huelewi kabisa ninachokisema, pamoja na hayo ni ombi langu kwa Mungu uelewe haya ili uweze kutengeneza mahali unaona umekwama.

Kuelewa kile unafanya inakupa nafasi zaidi ya kufanya vizuri bila kusukumwa na mtu yeyote, isipokuwa wewe mwenyewe utajisukuma kufanya bila kuangalia nani anakuona/anakutazama.

Mungu akusaidie kutambua kile unafanya.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Tovuti: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081