Ndugu yangu katika Kristo, nakusalimu katika jina lipitalo majina yote, jina la Yesu Kristo aliye hai. Aliyekufa na kufufuka, jina tulilo na ujasiri wa kulitamka mahali popote pale bila kuwa na hofu yeyote. Karibu sana tuanze siku hii ya leo kwa maneno ya kujengana.

Siku umejisikia umechoka kutafuta maarifa, ndio siku utakapopoteza mwelekeo wako. Maarifa hayachokwi, hata usome sana vitabu mbalimbali, bado utajisikia kusoma zaidi na zaidi. Mtu anayependa maarifa hana kuridhika, hana kiburi cha kujiona amesoma sana hahitaji tena kupata maarifa mengine.

Ukianza kumwona mtu wa namna ya kujiona ana maarifa mengi hawezi kuongeza mengine tena, uwe na uhakika mtu yule anaelekea kupotea au ameshapotea kabisa siku nyingi.

Maarifa hayakinai hata siku moja, kadri unavyozidi kujifunza ndivyo unavyozidi kupata hamu zaidi ya kwenda mbele. Hakuna siku utaona imetosha, utajisikia kupata zaidi, yaani ni kama chakula chako cha kila siku.

Hasa maarifa ya Neno la Mungu, ladha zinazopatikana ndani ya biblia, kama ni chakula basi hakijawahi kutengenezwa kwa mara moja kikamalizika. Maana kila ladha unayoipenda utaipata ndani ya biblia yako, tofauti na chakula cha kawaida unaweza kukutana na ladha ile ile kila siku.

Na tabia ya chakula chenye ladha ile ile kinakinai ukikila sana, Biblia takatifu haina hicho kitu, kila eneo la maisha yako limezungumzwa na Neno la Mungu. Hakuna siku utasema mambo ni yale yale, ukiona hivyo uwe na uhakika umeanza kupotea mwelekeo au umeshapoteza kabisa.

Mtu yeyote anayependa kumcha Mungu katika roho na kweli, lazima atalipenda Neno la Mungu, bila kujalisha hali na mazingira aliyopo. Acha ile kupenda ya mdomoni alafu kwenye matendo hakuna, nazungumzia kumpenda Mungu kwa msukumo wa kukupeleka kwenye matendo safi.

Upendo unaokusukuma kufanya kinyume na mapenzi ya Mungu, huo sio upendo wa kiMungu. Mtu anayetamani kufanikiwa kiroho na kimwili pasipo kumkosea Mungu wake kwenye eneo lolote lile la maisha yake. Lazima atatafuta maarifa kwa gharama yeyote ile, wakati mwingine anaweza kupenyeza kwenye mazingira hatarishi ili tu atimize haja ya moyo wake.

Dalili mbaya sana kuona Neno la Mungu ni lile lile kila siku, tangu nianze kusoma Neno la Mungu sijawahi kuona biblia iko hivyo. Kwanza ukisoma leo sura ile ile ukaja kurudia kesho, unapata kitu kipya kwa upana zaidi. Hata kama utarudia sura ile ile kwa wiki nzima, kama unasoma na kupata muda wa kutafakari utaona vitu/mambo makubwa zaidi, kadri unavyozidi kutafakari ndivyo unavyozidi kufunguka mengi zaidi.

Vizuri kuwa na tahadhari hii, hasa pale unapojiona huhitaji tena kusoma Neno la Mungu, kwa sababu umesoma biblia nzima. Ukaona haina haja tena kurudiarudia kusoma, hakuna siku utasema jana nilikula sana chakula sihitaji tena kula. Ukijiona huhitaji tena kula ujue umejichoka, na unataka kufa.

Ndivyo ilivyo kiroho, ukiacha kuulisha moyo wako Neno la Mungu, kuna vitu vingi sana vitadhoofika na mwisho wake vitakufa kabisa ndani yako. Maana tayari huna dira inayoweza kukuongoza njia iliyo sahihi, kuna mambo mengine unaweza usifundishwe moja kwa moja kanisani. Ila kupitia kusoma kwako Neno la Mungu ukayapata, au unaweza kufundishwa ukawa umesahau, kupitia Neno la Mungu ukakumbushwa.

Sifa moja wapo ya mtu mwenye hekima ya kiMungu ndani yake anapenda sana kujifunza, na hii ipo moyoni mwake na sio kwamba anajifanyisha. Ukiona umeanza kuona kujifunza Neno la Mungu hakufai au kunachosha, ujue umeanza kupungukiwa na hekima ya kiMungu ndani yako.

Usitamani kukaukiwa na Neno la Mungu, na wala usikubali upoe ila kasi yako ya usomaji wa Neno la Mungu. Kila siku ione ni fursa kwako kupata maarifa mengine mapya na sahihi, kwa mtazamo huo hata kama unajisikia kuchoka sana utajilazimisha tu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081