Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona. Tuifurahie hii siku njema ambayo sio wote walioweza kuiona.

Unaweza kutafuta ukweli wa jambo usiupate kama unavyotaka/unavyohitaji, na unaweza kukutana na watu ambao mpo pamoja ila hawapo tayari kukupoteza. Kwa kukutana nao watakueleza vitu ambavyo vinaendana na mapokeo yenu, na si yanayoendana na Neno la Mungu.

Kujitafutia maarifa mwenyewe kuna faida nyingi sana, kujitafutia ninayoizungumza hapa ni ile kuzama ndani ya biblia yako mwenyewe. Maarifa yaliyo ndani ya biblia hayajui dhehebu lako, Neno la Mungu linaeleza iliyo kweli hata kama dini/dhehebu lako linapitia pembeni.

Yapo mambo ambayo ki ukweli ukianza kuchimbua mwenyewe utaanza kuona uzito wake. Ambapo huenda siku zote uliyachukulia kawaida, ama hukujua kabisa kama yamebeba umaana mkubwa kiasi kile.

Kuishika biblia yako na kuanza kuisoma hakuna gharama yeyote, ni wewe kuamua kutoka ndani ya moyo wako. Huhitaji matangazo, huhitaji kujionyesha kwa kila mtu, huhitaji kugombana na watu, ni kujifungia chumbani kwako, ofisini kwako au kazini kwako, ukapata maarifa ya kutosha.

Usiishie kusimliwa, usiishie kusikia, usiishie kukataa unayoambiwa, usiishie kupingana na kauli mbalimbali zinazokulenga wewe moja kwa moja. Ifanye biblia kuwa rafiki yako, amua sasa kujua yaliyomo ndani yake yanaendana na unayosikia, yanaendana na kile unaamini, yanaendana na kile unakitolea jasho kuhakikisha hakuna mtu anaokuondoa kwenye mstari.

Haijalishi kila mtu anasema mahali ulipo ni sahihi, ujue usahihi wake ni upi kupitia Neno la Mungu. Usipofanya hivyo utaendelea kutikisa kichwa, na kufurahi moyoni, na wakati kuwa na ujasiri mkubwa.

Uzuri wa kuijua kweli ya Neno la Mungu, ni rahisi kukaa chini na kuelezana mnayoamini hayapo sawa sawa kwa mjibu wa maandiko matakatifu. Mkishaelewa ni rahisi kwenu kuondoa misimamo yenu ya kidini.

Wakati mwingine sio lazima kuhamahama madhehebu kama mnaweza kurekebisha yale mlikuwa hamyafanyi iwapasavyo. Hii inakuwa na nguvu kubadilisha kama kila mmoja atakuwa anasoma Neno la Mungu, kwa mtu mmoja inaweza kumchukua muda sana kueleweka katikati ya kundi kubwa la washirika.

Nakueleza haya ili ujue umhimu wa kujichimbia mwenyewe kwenye Neno la Mungu, unaweza kuona ni ngumu na wakati mwingine unaweza kuona kuelewa ni ngumu. Nikutie moyo kwamba, Roho Mtakatifu yupo atakusaidia kuelewa kadri ya uwezo wako unaopaswa kupokea.

Mungu akusaidie kutambua umhimu wa hili, ukishatambua usiishie tu kwenye maneno, hamishia kwenye matendo.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

chapeo@chapeotz.com

www.chapeotz.com

+255759808081