Haleluya,

Katika safari kuna mahali utahitaji msaada wa wengine, ndipo uweze kufika mahali ulikuwa unataka kufika. Na hutoweza kupata msaada pasipo kuuliza mahali unataka kwenda, haijalishi umefuata njia nzuri, kama haikupeleki mahali unatakiwa kufika, hutoweza kufika.

Siku moja kuna watu wawili wakawa wanabishana kuhusu kufika mahali ambapo hawajawihi kufika, yaani ni mara ya kwanza kwao kusafiri kwenda maeneo yale. Wa kwanza akawa anasema, vizuri kuuliza watu au ukaomba msaada wa mtu akupeleke mahali unataka kufika, ila mwenzake akamkatilia hilo na akawa na hoja yake pia.

Huyu mwingine akawa anasema, mi siwezi kuuliza mtu yeyote kama nitakuwa na simu. Nitatumia simu yangu kumuuliza mwenyeji wangu, huyu mwenzake akamuuliza sio kila jambo utaweza kuuliza kwa simu, kuna mahali utahitaji msaada wa mtu unayemwona mbele yako.

Nikawa nasikiliza mvutano ule, ukweli kabisa wote walikuwa sawa, kwa sababu hii, sio kila jambo unaweza kuuliza mtu unayemwona barabarani. Mambo mengine unaweza kuuliza kwenye simu kwa mtu anayefahamu mahali pale, basi ukafanikisha jambo lako. Pia sio kila jambo utaweza kupiga simu ukauliza, mambo mengine unahitaji kupata mwenyeji akakusaidia lile unahitaji.

Sasa hawa watu wawili wakati wanabishana, huyu wa kusema atatumia simu mahali popote bila kuhitaji msaada wa mtu anayemwona, alikuwa anaonyesha hawezi kuhangaika kutafuta msaada mwingine isipokuwa wa simu tu. Ukirudi kwenye uhalisia sio kweli, mfano akitaka kuulizia hata sehemu inayotoa msaada/mahitaji fulani anayohitaji, lazima aulize wenyeji wa eneo lile.

Kwanini nakupa haya yote, nina sababu nzuri kabisa kukuleta kwenye somo nililoanza nalo kwa kichwa chake hapo juu. Nikiwa na maana nzuri kabisa kukupa mfano huu hai.

Tunapokuwa tunataka kusoma Neno la Mungu, tunaweza tukapata wakati mgumu sana namna ya kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali. Lakini katika kukabiliana na hayo yote, inafika mahali tunapata mtu wa kutuelekeza namna ya kufanya.

Huyo mtu anayetuelekeza na kutupa mbinu za kuweza kufikia mahali tunahitaji kufika, sio kila mahali mtaweza kuwa naye. Na sio kila mahali utakapouliza utapata nafasi ya kukufikisha mahali unahitaji kufika, kuna mahali panaonekana unahitaji msaada mdogo wa kuelekezwa.

Usitegemee kila wakati kusukumwa ufike mahali ulikuwa unahitaji kufika, umeonyeshwa namna ya kufika. Na aliyekuonyesha naye anakuwa na majukum yake, huwezi kumwambia nipeleke hadi mwisho, wakati umemkuta ana kazi zake au ana safari zake.

Muhimu ni kuangalia mazingira, ukiona unaweza kupotea, panda usafiri wa kukufikisha hadi malangoni. Kufanya hivyo inakusaidia usipotee na usiendelee kuzunguka bila msaada.

Tukija kwenye kusoma Neno la Mungu, utakutana na maelekezo mengi ya namna ya kuweza kusoma Neno la Mungu. Katika maelekezo yale unaweza kuyaelewa ila ikawa ngumu kuyatekeleza kwa vitendo, utahitaji msaada zaidi wa kusimamiwa hadi ufikie lengo lako.

Pamoja na kusimamiwa hadi ufikie mahali unataka, sio kila wakati utakuwa na yule anayekusimamia. Utapaswa kujisimamia wewe mwenyewe kwa miguu yako na si kusubiri usukumwe, njia umeonyeshwa, uzuri wake hukuonyeshwa tu hadi mahali ulipotakiwa ufike umepata msaada wa kufikishwa.

Juhudi zako za kufanya kile kilikufanya usukumwe kujifunza Neno la Mungu, bila kuweka juhudi binafsi utaanza vizuri ila baada ya muda mchache utapoteza mwelekeo. Ile bidii yako ya awali hutokuwa nayo tena, na utabaki kujipa siku, mara kesho, mara wiki ijayo… unashangaa siku zinakatika bila mafanikio yeyote.

Ambatana na wenzako wenye kuelekea mahali unahitaji kufika, ila isiwe ndio kila kitu wakusaidie. Madam wamekupa mwanga namna ya kufika mahali unataka, weka Bidii yako binafsi, nenda nao. Huku unashika vizuri njia waliyokupitisha ili ikija kutokea haupo nao, uwe na uhakika wa kwenda mwenyewe.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.