Atukuzwe Yesu Kristo aliye hai sasa na milele, anayetupa kushinda siku zote za maisha yetu, kwa wale wamwaminio na kuyatenda mapenzi yake. Ashukuriwe Mungu mwenza wa yote, ametupa siku nyingine tena mpya kabisa, ambapo ni fursa kwetu kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.

Yapo mazingira unaweza kukutana na maneno mabaya, ukafikiri yanayosemwa ni kweli na hakika, kumbe sivyo ilivyo. Maana inawezekana hayo yasiyo ya kweli yanazungumzwa sana na kuaminiwa na baadhi ya watu wanaoaminika mbele ya jamii.

Kama unavyojua maneno ya uongo yana nguvu kuliko maneno ya ukweli, hii inatokana na ukweli mara zote huwa huna chumvi sana. Wengi wetu huwa tunaamini haraka uongo kuliko mtu anayekuambia ukweli, mtu yule anayesema ukweli huwa tunamwona ni adui kwetu au anatunyima kitu fulani.

Pia yapo maneno mengi ya watu waovu, yanayoweza kumpotosha mtu akayaamini na kuyatendea kazi. Ndipo unakuta mtu alikuwa yupo vizuri, baada ya kupewa maneno mabaya anabadilika kabisa tabia yake. Hii unaweza kuikuta hasa kwa wale wachanga, na wasio na maarifa ya kutosha ndani ya mioyo yao.

Jambo la furaha na kuleta tumaini jipya zaidi, ni yule mtu mwenye maarifa sahihi Bwana humlinda na maneno ya watu waovu. Mtu aliye na mwelekeo ulio sahihi, ndio mtu aliye na elimu/maarifa sahihi ya kiMungu. Huyo mtu yupo salama sana, na kila elimu iliyo kinyume na mapenzi ya Mungu, Mungu mwenyewe atasimama kuhakikisha mtu wake hapotoshwi.

Inatupa hamasa ya kuendelea kumpenda Mungu, inatupa hamasa Zaidi ya kuendelea kujaza maarifa sahihi ya Neno la Mungu. Sio tu Mungu anamlinda yule aliyeliamini jina la Yesu, Mungu huwalinda na wale walio na maarifa ndani yao.

Hebu tuone maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu hili, huenda umeanza kupata shida kuhusu hili. Na kuanza kujiuliza inawezekana vipi Mungu kumlinda mwenye maarifa sahihi.

Rejea:Macho ya BWANA humhifadhi mwenye maarifa; Bali huyapindua maneno ya mtu haini. MIT. 22:12 SUV

Je wewe usiye na maarifa inakuwaje? Bila shaka ulinzi wako haupo kwenye elimu zisizo sahihi. Maana kinachowalinda wenye maarifa, ni yale maarifa yao huyapindua yale maneno ya watu potovu/waovu.

Unafikiri wewe unayesema umeokoka alafu hutaki kusoma Neno la Mungu, wala huna muda wa kupata mafundisho sahihi ya Neno la Mungu. Watu wabaya wakija kwako, unafikiri utabaki salama?

Hebu tafakari hili kwa kina, eneo lolote lile la maisha yako, linahitaji maarifa. Kitabu pekee kilichobeba maarifa makubwa ya kumsaidia mwamini, ni biblia yenye Neno la Mungu. Ukishakuwa na Neno la Mungu, atakayekushawishi na imani potofu yeyote, uwe na uhakika kitachokusaidia kufanya mchujo wa maneno yale potofu ni maarifa sahihi uliyonayo.

Unaonaje kuanzia leo ukalichukulia Neno la Mungu kwa sura ya tofauti kabisa, ikiwa linaweza kutupa maarifa sahihi ili tusitoke nje ya mstari sahihi. Si ndio fursa kwetu kuanza kusoma Neno la Mungu kwa nguvu zote pasipo kusitasita?

Unajua nimeshangaa kuona huu mstari unavyozungumza maneno mazito namna hii, kumbe wengi wetu tunaingizwa kwenye uovu au upotovu kwa kutokuwa na kinga yeyote ya maarifa sahihi.

Rejea;Macho ya BWANA humhifadhi mwenye maarifa; Bali huyapindua maneno ya mtu haini. MIT. 22:12 SUV

Hapa Neno la Bwana linasema linamhifadhi aliye na maarifa, rudi sasa kwa yule asiye na maarifa inakuwaje? Bila shaka unaweza kuona anaweza kuchotwa na maneno ya mtu mwovu, potovu, na mdanganyifu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081